Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKWELI unauma. Na ili ufahamu hilo, mara nyingi watu
wanaosema ukweli huwa hawapendwi. Watazushiwa na kusemwa mno kutokana na
misimamo yao ya ukweli wanayosema mbele ya hadhira.
Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia ni mbunge wa Handeni, kwa miaka 20 sasa, Dkt Abdallah Omary Kigoda, pichani.
Wakati nasema haya, najipa moyo kuwa hata kama wapo
watakaochukizwa na ukweli wangu, ila ipo siku jamii itaishi vizuri kutokana na
kukombolewa na harakati za ukweli zinazoweza kupingwa na wachache wao waliokuwa
kwenye nafasi mbalimbali za kiutawala.
Ndio, bora niseme tu Dkt Abdallah Omary Kigoda anastahili
kupumzika kuongoza kama Mbunge wa Handeni, mkoani Tanga. Kigoda ni mbunge wa
Chama Cha Mapinduzi CCM kwa miaka 20 sasa.
Kigoda aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kama mbunge
mwaka 1995. Watoto waliozaliwa miaka ya 1995 mwaka 2015 wametimiza miaka 20. Ni
kipindi kirefu mno kuongoza katika nchi inayojipambanua kuwa inaongozwa kwa
misingi ya kidemokrasia.
Aidha, watoto hao waliozaliwa miaka ya 1995 na kukuta kero
nyingi kama vile kukosa maji safi na salama, umeme vijijini, elimu duni, afya
na mengineyo wanashangaa kama hadi leo kero hizo hazijatatuliwa ipasavyo licha
ya kuongozwa na mbunge aliyekaa madarakani kwa muda mrefu.
Kwanini Kigoda anastahili kupumzika? Licha ya Handeni kuwa
wilaya kongwe na kubwa mno, lakini wananchi wake wanaishi maisha magumu na
kuvumilia shida mbalimbali, jambo lililowachosha.
Wilaya hii haina maji. Wananchi wake wanalazimika kununua
ndoo ya maji kwa Sh 700 hadi 1000 yanapotoka mbali zaidi. Kwa mtu mwenye
familia ya watu wanne, atalazimika kununua ndoo tatu hadi tano.
Endapo atanunua ndoo tano, basi atalazimika kulipia Sh 3500
kama atayanunua kwa Sh 700. Lakini kama atanunua kwa Sh 1000, basi mwananchi
huyo atayanunua maji kwa Sh 5000. Je, pato lake kwa siku lipoje?
Mbaya zaidi, licha ya kuwa wilaya kongwe, lakini Hospitali ya
wilaya ya Handeni haina chumba cha kuhifadhia maiti. Watu wanalazimika
kupelekwa Hospitali ya wilaya Korogwe (Magunga) kuhifadhiwa kabla ya kuzikwa au
kusafirishwa kwa wale wenye utaratibu huo.
Aidha wilaya pia haina gari la kuzimia moto. Ulipotokea moto
uliowatia hasara wananchi wengi, msaada ulizimika kutoka Korogwe. Hadi gari
hilo lilipofika Handeni, moto huo ulishateketeza nyumba nyingi na kuwapa hasira
wananchi kiasi cha kulipopoa kwa mawe gari hilo.
Huduma za afya ni mbovu. Na yote hayo yamesababishwa na
utawala mbovu usiokuwa rafiki kwa wananchi dhidi ya mbunge Kigoda, ambaye pia
ni Waziri wa Viwanda na Biashara.
Kumbuka Kigoda sit u ni mbunge wa muda mrefu, bali pia
amewahi kuwa Waziri wa wizara tofauti kwa vipindi tofauti. Wakati yeye ni
Waziri wa Viwanda na Biashara, lakini wakulima wake wa matunda wilayani Handeni
wanapata hasara kubwa mno.
Maeneo ya Michungwani, Segera na kote wanapolima machungwa
hawana kwa kuyapeleka na mara kadhaa wanayouza si yale yanayozaliwa. Hii ni
aibu kubwa mno. Wilaya ya Handeni ipo ipo tu. Hata elimu ya sekondari ya kidato
cha tano na sita ni mtihani mzito.
Licha ya ukongwe huo lakini hakuna cha kujivunia. Wakulima
wanadhulumiwa mashamba yao na wenye nacho. Watu wachache wamegawana maeneo
makubwa ya ardhi, hali kadhalka uwapo wa dhahabu na madini mengine hakuonekani
dalili njema za kuwakomboa wananchi wa Handeni, wanaoishi kwa kupiga miayo.
Ni mifano hii michache tu kati ya mingi ninayoweza kuisema
hapa, nadiriki kusema Mbunge Kigoda hana cha kumfanya agombee tena jimbo hilo
kwa kipindi cha tano kijacho.
Bali anastahili kupumzika na abaki kuwa mshauri tu. Watu
wanaishi kwa tabu kwenye wilaya yao yenye kila aina ya matunda. Wananchi wa
Handeni wataendelea kutaabika hadi lini?
Hili ni jambo la kuliangalia. Mfumo wa kiutawala wilayani
Handeni umekufa na hauna mwamko tena. Mbaya zaidi, kitu chochote ambacho mbunge
hakitaki aidha kwa woga wake kisiasa au vinginevyo hakubali kifanyike hata kama
kina manufaa na wananchi wake.
Katika hali ya kushangaza na kuogopesha, hakuna mtu yoyote
anayeweza kutoa sauti yake kumkemea au kumkosoa mbunge. Hii ni mbaya. Kumuogopa
huku kunasababisha hasara kwa wilaya.
Haiwezekani mbunge akawa anajua yote. Lakini pia haiwezekani
kuona mbunge analalamikiwa bila sababu za msingi. Ingawa baraza la madiwani
ndio lenye mamlaka ya kisheria ya kupanga bajeti na kuisimamia, ila mbunge naye
ni mjumbe kutokana na kofia yake.
Na kwakuwa tumekuwa na utawala wa kuogopana, madiwani hawa
wameshindwa kupaza sauti yao kusimamia mambo yenye manufaa na wilaya ya
Handeni.
Leo hii ni aibu iliyoje? Ukongwe wa Handeni na rasilimali
zote ilizokuwa nazo, hakuna chuo chochote kinachoweza kuwapa elimu ya juu
wanafunzi wanaotokea kidato cha nne au sita.
Lini Handeni itakuwa na mwangaza? Mwangaza huo utakuja siku
Kigoda atakapoamua kwa ridhaa yake au kulazimishwa kupumzika kwasababu
ameshindwa kuwaongoza watu wake.
Kwa bahati mbaya, leo hii wananchi wamekuwa wakali. Wamekuwa na
mtazamo chanya wa kuhoji maendeleo yao na wale wanaochelewesha mikakati
inayoweza kuwakwamua kiuchumi.
Wakati nasema haya, nadiriki kuona hatari ya kudhalilika juu
ya mbunge huyu, hasa kama ana ndoto za kutetea kiti chake. Wananchi wamekuwa
wakihoji udhaifu wake hadharani.
Mengi yanayosemwa ni kama matusi kwake. Mbunge aliyekaa
madarakani miaka 20, anapoambiwa ameshindwa kufanyia kazi hata chumba cha
kuhifadhia maiti ni aibu isiyokuwa na kifani.
Ni budi kwa viongozi wa juu wa CCM kuvuta taswira halisi ya
ugumu wa maisha ya wana Handeni. Lakini pia viongozi hao lazima wajuwe chama
chao kipo rehani kwasababu ya kumng’ang’ania mtu mmoja.
Yeye ni nani? Hakuna mwingine? Mfumo wa upatikanaji wa
viongozi wa CCM hususan wa kuangalia asiyependwa ndiyo anayepita umepitwa na
wakati kwa Dunia ya leo ya Sayansi na teknolojia.
Tunachokiona sasa ni tatizo kubwa la kimfumo kama
nilivyojaribu kulieza hapo juu kwenye makala haya. Kama leo tunawaza namna gani
ya kuleta maji, umeme vijijini, afya jua tumeshindwa.
Na udhaifu huu utachukuliwa kama tahadhari katika Uchaguzi
Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu kuhakikisha kuwa mgombea wa CCM, hasa
kama akiwa Kigoda aenguliwe. Na kama watashindwa basi hata wale wasioaamini
upinzani watashawishika na kupiga kura za chuki dhidi ya Kigoda na chama chake
CCM.
Bora ukweli useme bila woga. Ukweli usemwe ili watu
wajirekebishe katika harakati za kuikomboa wilaya ya Handeni ambayo si wote
wanaiheshimu kutokana na kiwango kibovu cha viongozi wake, wakiongozwa na
mbunge wa miaka 20 madarakani jimbo halina maji, huduma za afya mbovu, elimu ya
kusua sua, malalamiko ya wakulima na kadhalka.
Ajabu, wanaopita pembeni wakimsifia mbunge ni viongozi
wachache wa CCM wilayani, ambao kwa namna moja ama nyingine wana manufaa naye,
aidha kuwekwa wao madarakani katika Uchaguzi wa ndani wa CCM, hivyo kuendelea
na sera ya kulipana fadhira.
Hilo haliwezekani. Tunahitaji kuzaliwa upya kwa wilaya ya
Handeni, tukianzia na kuona namna gani mfumo uliooza chini ya Kigoda
unaondolewa kwa ajili ya kuibua ari mpya, kasi mpya na vitendo vyote vya
kupigania maendeleo kwa jimbo hili linaloonekana la mwisho kimaendeleo.
+255712053949
No comments:
Post a Comment