Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
JOTO la kisiasa limezidi kupamba moto. Hii ni kutokana na harakati za kuimarisha kambi za wagombea wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu nchini kote.Wameanza mchaka mchaka wa udiwani, ubunge bila kusahau urais. Kwa nafasi ya urais, tumeshuhudia watu wanaojiandaa kuvutana na kustawisha makundi yao ili iwe chachu yao ya kurithi kiatu cha Rais wa Awamu ya nne, Profesa Jakaya Mrisho Kikwete.
Ingawa nafasi za ubunge na udiwani zinawaniwa pia na watu kutoka kwenye vyama vya upinzani, lakini ni wazi kuwa joto na mtifuano mkubwa upo katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kila chama kina taratibu zake. Hata hivyo, kutokana na maridhiano yao waliyopa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vyama vinne vya upinzani vikiongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi CUF, NCCR Mageuzi na NLD vimetangaza kusimamisha mgombea mmoja kila jimbo la uchaguzi au kata.
Huo ndio msimamo wa wapinzani. Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanaamini kuwa vyama vya upinzani mwaka huu watafanya vizuri katika Uchaguzi Mkuu, endapo CCM haitajisahihisha na wafalme wake majimboni.
Ni kutokana na hilo, nadiriki kusema kwamba, uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mgumu. Katu CCM isitarajie mteremko. Ili iweze kujua namna gani inafanya vizuri katika uchaguzi huo, ni lazima iwapime wabunge na wagombea wake hususan kwa nafasi za ubunge.
Licha ya kuwapo katika Bunge litakalomalizika baadaye mwaka huu, bado wana ndoto za kuingia kwenye uchaguzi wa mwaka huu kutetea nafasi zao, bila kuangalia jinsi walivyochokwa na wananchi wao.
Hii ni kwasababu baadhi ya wabunge wamechokwa. Na hata kama wanakubalika, haina haja ya kuendelea kuwavumilia ili waendelee kutawala katika majimbo yao, maana hakuna umuhimu huo.
Yapo majimbo yenye changamoto na shida nyingi. Wananchi hawajui nini hatma ya maisha yao. Shida ya maji, afya duni, elimu duni na kilimo kisichokuwa na tija ni mtihani mzito kwao.
Wakati wabunge hao wakijigamba kama wanapendwa au wanakubalika, wananchi wao hawana cha kujivunia. Wameendeleaa kupiga miayo na kudanganywa kila ufikapo uchaguzi. Mtazamo wa wabunge hao utaleta madhara makubwa kwa CCM.
Wananchi watapiga kura za chuki. Wana uwezo wa kuwaondoa wabunge hao mizigo na kuwapa wapinzani kwa njia ya sanduku la kura. Watafanya hilo bila kuangalia heshima ya CCM iliyojiwekea tangu mwaka 1977.
Hili si sahihi. Na linapaswa kupingwa vikali. CCM Makao Makuu bila kusahau viongozi wake waliosambaa Tanzania nzima, lazima wajipange ili kulinda hadhi ya chama hiki mbele ya hadhira.
Iwaite wabunge wake na kuwahoji nini wamewafanyia wananchi wao. Iwahoji kwanini wanataka kugombea tena ubunge. Kwa wale waliokaa madarakani kwa miaka mitano, walau wanaweza kuonewa haya, ukizingatia kuwa vipindi viwili ni halali, tukiamini upo uwezekano wa kusimamia yale aliyoanzisha.
Wale waliokaa madarakani miaka 10 kuendelea, wasichekewe. Kama walishindwa kufanya kwa miaka yote waliyokaa madarakani, watawezaje kutekeleza kwa miaka mitano ijayo?
Huu si muda wa kupotezeana muda. Wabunge mizigo na wanaotawala kwa manufaa ya matumbo yao na familia zao wasionewe huruma. Kwa bahati mbaya, CCM ina mfumo mzuri, ila unaharibiwa na rushwa na kuoneana haya.
Makatibu wa CCM wa Mikoa na wilaya ndio wanaoweza kumpitisha mbunge mzigo asiyekuwa na jipya kwa uongozi wake.Badala ya makatibu hao kusimamia sheria, kanuni na maadili ya chama, wamebakia kuhujumu wengi na kunufaisha wachache wao.
Katibu anashindwa kusimamia hata yale yaliyokuwa kwenye ilani ya chama chake kwa kumuogopa mbunge aliyekuwa madarakani kwa zaidi ya vipindi viwili, huku anachojua ni kuunda mtandao usiokuwa na tija.
Wabunge hao na makatibu ndio wanaokiweka chama katika nafasi ngumu kwenye chaguzi zake. Unawezaje kumshawishi mwananchi ampigie kura mbunge aliyekaa madarakani miaka 10 bila kutatua shida za wapiga kura wake?
Wanaona jinsi akina mama wanavyotumia muda mwingi kutafuta maji kwa umbali mrefu, hali ya kuwa mbunge amechimba kisima karibu na nyumba yake. Katika shida zote walizokuwa nazo, hakuna hata moja inayomuhusisha mtoto wa mbunge, mke au familia yake ya karibu.
Kwani wapiga kura ndio wameumbiwa shida? Hawana haki ya kuishi vizuri kutokana na serikali yao makini iliyochaguliwa kwa mapenzi makubwa? Inakera na kuumiza kichwa. Kwa akili zao wameamua kuidhalilisha CCM.
Viongozi wetu wawe na haya na huruma pia. Ubunge usitumike kama mradi wa mtu mmoja, hali ya kuwa hana uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi wake. Wanaoongoza kwa kutegemea busara ya kiti cha katibu na viongozi wenzake wa CCM katika jimbo husika.
Ni zaidi ya ujinga na upuuzi. Tanzania si shamba la bibi. Tunahitaji kuwa na viongozi na si watawala tu. Mfumo mbovu usiokuwa na dhamira ya maendeleo ya watu wao, huchochea chuki kwa Watanzania dhidi ya CCM, moja ya chama kikongwe barani Afrika.
Tujipimae na kujisahihisha pia. Viongozi wa CCM wa matawi hadi Taifa waangalie mbinu ya wabunge mizigo wa muda mrefu na waliochokwa.
Wakati nasema haya, natambua wapo Watanzania wenye uwezo wa kuongoza kwa kushirikiana na wananchi wao.
Lakini wanashindwa kwasababu ya ghiriba, chuki za kimtandao dhidi ya wafuta viatu wa mabwana wakubwa walioyafanya majimbo ni kampuni zao binafsi.
Fanya ziara katika mikoa mbalimbali ujionee hali ilivyokuwa ngumu. Wapo Watanzania ambao hata mlo wao wa siku ni tatizo. Watoto wao wanakwenda shuleni wakiwa na nguo zenye matobo.
Na yapo maeneo ambayo wanafunzi wetu wanakaa chini. Pamoja na kukaa chini kwa wanafunzi, kukosa huduma bora za afya, ajabu wapo wabunge wanaojiandaa tena kugombea ubunge.
Huu ni zaidi ya ujinga. Tunapaswa kujitafakari upya kwa ajili ya kuunda Tanzania yenye neema. CCM iangalie hawa wabunge waganga njaa. Wabunge wachumia tumbo wasioridhika na madaraka.
Ngazi za kiuongozi zinajulikana. Ukishafikia ngazi ya ubunge, ukakaa madarakani miaka 10 ni dhahiri unapaswa kuachia ngazi na kupisha wengine waendeleze yale uliyofanya. Vinginevyo labda urais maana ndio nafasi iliyobakia.
Huo ndio ukweli wa mambo. Maana yapo majimbo kwenye wilaya yanayoonekana ni vichaka. Hakuna dhamira ya kuwaletea maendeleo wananchi wao. Hasira zinawapanda wananchi hao na kuamua kusimama kidete kubadilisha viongozi na kuwapitisha wapinzani, wakiamini ndio sehemu ya kuwapunguzia kero zao zilizochosha watu.
Ifikie wakati wabunge na viongozi wao wa CCM wajitafakari upya. Wajipime kama wanayo shauku ya kuwatumikia wananchi wao. Ikiwa wameona ni ngumu, basi wakae pembeni kwa maslahi ya chama tawala.
Ikiwa hawataki kwa ridhaa yao basi walazimishwe ili kupunguza chuki kwa wananchi waliopania kubadilisha mfumo wa uongozi katika maeneo yao. Wananchi wasilazimishwe waamini kuwa adui wao ni CCM. Adui yao ni viongozi wabovu waliokuwapo kwenye CCM.
Na viongozi hawa wanaweza kuiondolewa na CCM ikaendelea kuheshimika ndani na nje ya nchi.
kambimbwana@yahoo.com
+255712053949
No comments:
Post a Comment