Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KIUNGO wa timu ya Coastal Union, John Mahundi amechaguliwa kuwa
mchezaji bora wa mwezi Disemba 2014 wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea
kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Baraka Kizuguto, alisema kwamba Mahundi alitoa mchango mkubwa kwa timu yake ya Coastal Union mwezi
Disemba mwaka jana na kuchaguliwa na jopo la makocha linalofanya kazi ya
kuchagua mchezaji bora wa kila mwezi.
Aidha mshambuliaji wa timu ya Polisi Morogoro, Said Bahanuzi
amechaguliwa kuwa mchezaji bora mwezi Januari 2015 wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
inayoendelea kutimua vumbi mzunguko wa 15 kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Bahanuzi anayechezea timu ya Polisi Morogoro kwa mkopo akitokea
timu ya Young Africans amekua na mchango mkubwa kwa timu yake tangu kujiunga
nayo mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom nchini.
Kwa kuibuka wachezaji bora, Mahundi na Bahanuzi watazawadiwa fedha
taslimu sh. milioni moja kwa kila mmoja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo
kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.
Jopo maalumu la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika
kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua
mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, na baadaye
alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.
No comments:
Post a Comment