*Wafanya
Mkutano Mkuu wa 20 AICC Arusha
*Dkt Kimei
aanika mikakati ya kuipaisha CRDB
Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Arusha
NI kama vile uhai na mafanikio ya benki ya CRDB umejulikana
upya, baada ya menejimenti, Bodi ya Wakurugenzi na Wanahisa kukubaliana kwenye
Mkutano wao Mkuu wa 20 wa Wana Hisa uliofanyika Mei 9, mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB benki, Dkt Charles Kimei, akizungumza jambo katika Mkutano wa wanahisa wa benki hiyo jijini Arusha.
Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Simba, kwenye Kituo
cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC, huku ukifurika wana Hisa wengi kutoka
mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Mtangazaji mkongwe nchini Tanzania, Salimu Mbonde, akisikiliza kwa makini mkutano wa hisa wa benki ya CRDB, jijini Arusha.
Katika mkutano huo ulioanza saa 3 asubuhi, mengi
yalijadiliwa, ikiwamo ripoti ya wakaguzi na mwelekeo wa benki hiyo katika
kufungua matawi, bila kusahau tawi lao lililokuwa nchini Burundi.
Katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dkt Charles Kimei, anasema kwamba
kufanyika kwa amani na mafanikio mkutano huo, ni kama vile benki yao imezaliwa
upya.
Anasema biashara yoyote inayohusiana na wana hisa, kunahitaji
mipango ya kukubaliana kwa pande zote, jambo linalowafanya menejimenti, bodi na
wanahisa kuona ipo dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba bendi yao inapiga
hatua.
“Wanahisa ni watu muhimu na ndio maana tumekuwa tukifanya
mkutano wa mwaka kwa ajili ya kupitisha ripoti, kutaja vipaumbele na kuangalia
jambo gani la kufanya katika kuhakikisha kwamba benki yetu inakuwa bora zaidi.
CRDB ni kati ya benki bora nchini ambayo tumefanikiwa pia
kuwa na tawi letu nchini Burundi ambapo hata hivyo kumekuwa na hali ya sintofahamu
katika mambo ya kisiasa,” alisema.
Katika mkutano huo, baadhi ya wanahisa walitoa ushauri wao
juu ya mwenendo bora wa benki yao, ikiwamo taratibu za ufunguaji wa matawi
katika mikoa mbalimbali.
Awali, mkutano huo ulikuwa na dondoo kama vile kufungua
mkutano, Kuchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu, Kuridhia
ajenda ya mkutano, kuthibitisha kumbukumbu za Mkutano Mkuu uliopita, kujadili
yatokanayo na kumbukumbu za Mkutano Mkuu wa 19, kujadili na kupokea taarifa ya
Bodi ya Wakurugenzi na taarifa hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2014.
Dondoo nyingine ni pamoja na gawio kwa mwaka 2014, hesabu
zilizokaguliwa za mwaka ulioishia na Desemba 31 mwaka 2014, taarifa ya Bodi ya
Wakurugenzi, kuidhinisha ongezeko la mtaji kwa kutoa hisa stahili (rights
issue), kuidhinisha mapendekezo ya mabadiliko kwenye Katiba ya benki-Azimio
Maalum, kuidhinisha ada ya wakurugenzi, kuteua wakaguzi wa hesabu, kuchagua
wajumbe wa bodi, ikiwa ni pamoja na wajumbe wawili wa bodi watakaowakilisha
kundi la wanahisa wenye chini ya asilimia moja, bila kusahau mjumbe mmoja wa
Bodi atakayewakilisha kundi la wanahisa wenye hisa asilimia moja na kumi.
“Pia tulijadili dondoo kama vile kujadili mapendekezo kutoka
kwa wanahisa, mengineyo kwa idhini ya mwenyekiti, kupanga mahali na tarehe ya
mkutano ujao pamoja na kufunga.
“Kwa ujumla yote yaliyotajwa katika mkutano huo yalipitishwa
kwa nguvu zote na wana hisa wenyewe, ikiwa ni njia sahihi ya kuiweka juu benki
hii inayoheshimika sehemu mbalimbali za Tanzania, bila kusahau katika nchi
nyingine za Afrika, ikiwamo Burundi,” alisema.
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa CRDB Benki, Dr Kimei anasema moja
ya mambo yaliyoifanya benki yao ifanye vizuri ni kutokana na kuwa wabunifu na
kwenda na teknolojia, kama vile huduma ya SimBanking, Fahari Huduma na
mengineyo.
Anasema katika huduma ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya
simu imeshika hatamu ambapo watu wengi wameonekana kuvutiwa na ubora wa huduma
hiyo pamoja na urahisi wake kulingana na utaratibu wa matawi uliokuwapo zamani.
Dkt Kimei anasema pamoja na kuboresha huduma hiyo ya simu
banking, pia wanaendelea kuhakikisha kwamba wanafungua matawi mengi ili
kuifanya benki yao iwe rahisi kuwatumikia wateja wao.
Awali walikuwa na matawi 103, lakini
wamefika mbali zaidi kwa kufungua matawi 20, hivyo sasa watakuwa na matawi
123, mashine za kutolea fedha yani (ATM)
374, bila kusahau mawakala wa fahari huduma 1,067.
Aidha Dkt Kimei aligusia pia huduma ya Microfinance Services
Company Ltd, akisema kuwa uwapo wa kampuni hiyo tanzu ndani ya CRDB utazidi
kuongeza mapenzi na ukuaji wa uchumi kwa kuwahudumia wajasiriamali wadogo kwa
kupitia SACCOS.
Katika siku zijazo, huenda kampuni hiyo nayo
ikatoa huduma yenyewe kwa kujiendesha ili kutoa huduma bora na kukuza heshima
ya benki ya CRDB.
“Kauli mbiu yetu iwe ni mauzo, mauzo na mauzo, tukiamini kuwa
kwa ushirikiano huu mkubwa uliopo kati yetu sisi watendaji na watumishi wote wa
CRDB, Bodi ya Wakurgenzi, Wana Hisa, wateja wetu na serikali kwa ujumla,
naamini tutakuwa juu na imara.
“Pamoja jitihada zote hizi, bado tunaamini kwamba tunapaswa
kutumia gharama kubwa ili kuyaweka matarajio yetu katika mizania stahili, hasa
bejeti ya ufunguaji wa matawi mengine, ukizingatia kuwa tawi moja linahitaji
hadi Sh Milioni 700,” alisema.
Hata hivyo, muda wote huo wa Mkutano huo, wanahisa
walionyesha umakini, usikivu pamoja na kuhoji baadhi ya vipengele wakitaka
kujiridhisha na mwenendo wa benki yao.
Mwanahisa Gervas Ngikari, aliishauri Bodi na Mkurugenzi
Mtendaji kutafuta namna ya kubana matumizi ili fedha nyingi zisipotee hovyo ili
iwe njia ya kuiweka benki yao katika mafanikio makubwa, bila kusahau mapato ya
wana hisa, akitia hofu kuwa hesabu zinaonyesha kila Sh 100 inayoingia, 60 yote
inatumika, huku Sh 40 inayobakia ndio wanaogawana waliobakia, ikiwamo serikali,
benki na Wana Hisa.
Hata hivyo hoja hiyo ilifafanuliwa vizuri kwa jicho la
kiuchumi, kwamba yapo baadhi ya mambo yanayohitaji fedha, hususan ufunguaji wa
matawi na mahitaji mengine muhimu kwa mustakabali wa huduma za kibenki kama
sheria zinavyotaka, hivyo wanahisa wote kuridhia kila kilichosemwa katika
Mkutano huo.
Mwanahisa Joachim Tarimo yeye aliishauri menejimenti na Bodi
ya Wakurugenzi kuhakikisha kwamba benki yao inaingia nchini Kenya kufungua tawi
ili kwenda sambamba na soko la kifedha, akisema ndio njia sahihi ya kuikuza
benki yao.
Mwanahisa Anna David yeye aliishauri benki hiyo kubuni miradi
na fursa nyingine za kibiashara ili
kuingiza fedha kwa njia nyingine, akitoa mfano wa uwekezaji wa majengo na
mengineyo muhimu, akisema kuwa njia hiyo itaokoa pia fedha za gharama ya
upangaji majengo na mambo mengine muhimu.
No comments:
Post a Comment