Na Mwandishi Wetu, Handeni
MWANDISHI wa kitabu cha Dira na Tumaini Jipya Handeni, Kambi Mbwana, amemjia juu mbunge wa Handeni, mkoani Tanga na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Abdallah Kigoda, kwa madai kuwa anajaribu kumziba mdomo ili wananchi waendelee kuwa vipofu wasiweze kuwawajibisha wananasiasa mizigo wasiokuwa na faida kwa wilaya hiyo kongwe yenye rasilimali lukuki.

Mbwana aliyasema hayo jana mjini hapa, ikiwa ni siku chache baada ya Dkt Kigoda kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika Handeni Mjini katikati ya wiki iliyopita kuwataka wananchi wapuuze kitabu hicho, jambo lililoibua mvutano kwa wasomaji wa kitabu hicho na wanaoamini maneno ya Kigoda, ambaye ni mbunge wa jimbo la Handeni kwa miaka 20 sasa.


Akizungumzia hatua hiyo, Mbwana alisema kitabu chake hakijaandikwa kwa lengo la kumuonea wala kudhalilisha upande mmoja, ingawa alikiri kuwa mtu asiyekuwa na malengo ya kuwakomboa wananchi wake, kamwe hawezi kupata nafasi ya kukisifia kitabu hicho pekee kinachotoa dira na tumaini jipya kwa wananchi wa wilaya hiyo kongwe nchini Tanzania.


“Kwanza namshangaa Dkt Kigoda kwa sababu amedhihirisha upeo wake wa kufikiria umekuwa mdogo ndio maana anajaribu kuingilia kitabu hiki kinachoelimisha jamii sit u watambue changamoto zao, bali pia wajue namna bora ya kujikwamua kiuchumi.


Hii inakera na kuhuzunisha maana kama watu kama akina Kigoda wanaoaminiwa ni wasomi wazuri katika nchi hii wanashindwa kushirikiana na jamii yao ili kuwakwamua wananchi wao, ni kuonyesha kuwa uwezo wao kiakili na malengo ya kuwatumikia wananchi wao yamefikia ukingoni,” alisema Mbwana.


Akielezea kitabu hicho, Mbwana alisema Dira na Tumaini Jipya Handeni kimegusia mambo ya migogoro ya ardhi, shida ya maji, ukosefu wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya na mengineyo yanayoendelea kuwaumiza wananchi wa Handeni na Watanzania kwa ujumla, huku wakikipokea kitabu hicho kama mkombozi wao kutokana na aina ya kilichoandikwa ndani ya kitabu katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.


Kwa mujibu wa Mbwana, kitabu hicho kinapatikana sehemu mbalimbali za mkoa wa Tanga, kama vile Handeni, Korogwe, Tanga Mjini na baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam, huku kikionekana kupokewa kwa shangwe na wananchi waliopenda hoja na suluhisho zake zilivyoongelewa kwa kina ndani ya kitabu hicho cha aina yake.