Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
INAHITAJI akili ya kiuwendawazimu kuaminishwa na kuamini kuwa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza mvuto. Kwamba vinavyokubalika ni Chadema,
CUF, NCCR Mageuzi, NLD, TLP na vinginevyo, ambavyo kwa udhaifu wao, wameona
waungane baada ya kukosa dawa ya kukiangusha chama tawala.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ni mmoja wa makada wa CCM, wanaotajwa kuwa na ndoto za kuwania Urais, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, nchini Tanzania.
Si kweli, maana vipo viashiria vingi vinavyoonyesha kuwa
chama hicho kikongwe Tanzania, kipo imara na kinaungwa mkono na watu wengi,
wakiwamo watoto, wazee, vijana na wake kwa waume. Bado wapo watu wanaoamini kuwa mtu mtu anayepitishwa kugombea
katika nafasi yoyote ndani ya CCM, basi huyo ndiye mshindi. Na yapo maeneo
mengi ambayo watu wake hawajui chochote kuhusu vyama vya upinzani, isipokuwa
CCM.
Kuelekea katika Uchaguzi Mkuu, kumekuwa na kauli za hapa na
pale zinazoshiria kuwa baadhi ya Watanzania wenzetu, hususan wanaotoka katika
Chama Tawala wamedhamiria kuchukua fomu za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Ingawa wapo wengine wenye nia hiyo ya kutaka urais, ila ndani
ya CCM hali hiyo imezidi. Ndani ya CCM kuna joto na mchuano mkali. Takribani
miaka mitatu sasa tumeshuhudia mivutano ya kila aina.
Wataka urais huo wamekuwa na vikao na safari za kutunisha
makundi yao, bila kusahau kasi ya kuongeza ushawishi kwa vijana wao
wanaoshindana katika mitandao ya kijamii kwa kujiita majina ya kila aina,
kuashiria wapo kwenye msafara huo. Haya yote yanadhihirisha nguvu ya chama tawala. Kila mtu
anaangalia nani ana mvuto zaidi ya mwenzake ndani ya CCM. Kila jina linalotajwa
zaidi mtaani, basi linatokana CCM.
Wapo wanaomtaja Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, kwamba anayo haiba na uwezo wa juu ya kurithi kiti
cha urais, kitakachoachwa na Rais, Profesa Jakaya Mrisho Kikwete, baadaye mwaka
huu. Wanaoamini Membe anafaa wanafanya kila wawezalo ili jamii
iwaelewe, bila kusahau wanaojiita wapo kwenye safari ya matumaini, nao
wakichagiza Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani aliyejiuzulu na Mbunge wa
Monduli arithi mikoba ya JK.
Si Lowassa au Membe tu, bali wapo wana CCM wengine kede kede
walionyesha nia ya kutaka urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiamini
uwezo na vigezo wanavyo.
Vipi kuhusu January Makamba, Samuel Sitta, William Ngeleja,
Emmanuel Nchimbi, Profesa Sospeter Muhongo, Dkt Asha Rose Migiro, Augustino
Ramadhan, Stephen Wassira na majina lukuki yanayotajwa katika ndoto hizo za
urais.
Ingawa wenyewe hawajatangaza nia hiyo hadharani, lakini
mwenendo wao, harakati zao na pengine matamshi kadha wa kadha yanaonyesha kiu
hiyo ya kutakaa kuongoza taasisi nyeti na kubwa nchini Tanzania, kwa kofia ya
urais. Kuwa na ndoto ya urais ni jambo moja na kuwa rais ni jambo
jingine. Hii ni kwa sababu kunahitaji mipango na ridhaa ya kuaminiwa na
Watanzania wote kwa kupitia sanduku la kura.
Kura zitakazochanganya wagombea kutoka CCM na wale wa
upinzani, huku kwa mara ya kwanza katika historia ya siasa za Tanzania,
ikidaiwa kuwa vyama vine vya siasa vitasimamisha mgombea mmoja kwa mgongo
uitwao UKAWA. UKAWA ni msamiati ulioasisiwa katika Bunge la Katiba, ambapo
vyama vine vya vya Chadema, CUF, NCCR MAGEUZI NA NLD, viliamua kuungana,
muungano ulioendelezwa pia katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji
Desemba mwaka jana, wakisisitiza pia utaratibu huo utaendelea kwa madiwani,
wabunge na urais.
Pamoja na kuungana kwa vyama hivyo vine, bado hawakaribii
nguvu inayotoka CCM. Wagombea wawili, Dk Willbroad Slaa kutoka Chadema na
Profesa Ibrahimu Lipumba kutoka CUF ndio wenye kudaiwa wanao uwezo wa kusimama
kwa upande wa Bara. Upande wa Visiwani Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ndiye
atakayesimama kwa upande wa CUF ama UKAWA, kwa madai chama hicho ndicho chenye
nguvu na ushawishi wa kuaminiwa na watu wa Zanzibar. Sawa, lakini vipi wanao uwezo wa kuitingisha CCM? Lipumba
aliyegombea urais zaidi ya vipindi viwili Tanzania Bara na akaonekana kachokwa,
anaweza kuitikisa CCM?
Hata kama akiitikisa, UKAWA watamuanini na kumpa nafasi hiyo,
huku akiwapo Dk Slaa, aliyeshika nafasi ya pili nyuma ya Rais Kikwete, katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010?
Hili na mengine mengi yanawafanya hata wale wasioamini CCM,
nao wanaingia kwenye wimbo wa nani bora kutoka chama tawala. Wanaamini huko
ndiko kwenye mvutano mkubwa zaidi. Na mvutano huo unatokana na nguvu ya chama hiki kikongwe.
Chama kitakachotoa rais mwingine baada ya Kikwete aliyeingia Ikulu huku
akiungwa mkono na makundi mengi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Ni dhahiri wanaotaka kujua nguvu ya CCM waiangalie namna
inavyoweza kumpata pia mgombea wake wa Urais. Ni jambo nyeti linalowekwa katika
utaratibu mzuri na wa kueleweka. Hii inaonyesha ukomavu wa juu wa chama hiki. Hawa wote wanaotajwa kutaka urais, wameibuliwa na kukomazwa
na chama hiki kikongwe. Waliaminiwa katika nafasi mbalimbali. Na pengine kila
mmoja ana uwezo huo wa kusimama kama mgombea urais, huku akishinda kwa
kishindo. Uzuri ni kwamba hadi mtu anapoweza kusimamishwa kama mgombea
urais kwa tiketi ya CCM, anakuwa amepita katika vikaango lukuki kwa ajili ya
kujiridhisha naye. Kwamba ni mtu safi? Ana nguvu na ushawishi mbele ya hadhira?
Anaweza kuaminiwa na Watanzania wote, ukiacha hawa wanaopiga
kelele kwenye mitandao ya kijamii, ambao ni dhahiri baadhi yao wanafadhiliwa na
majina hayo? Je, anauzika, hana kashfa? Sifa hizi na nyingine kadha wa
kadha zitaondoa wasiwasi na uwezekano wa kuungwa mkono na makundi yote nchini
Tanzania. Na hapo ndipo panapojibu maswali ya wale wanaoamini mtu anayetoka CCM
ndio kiongozi wao.
Huu ndio ukweli wa mambo. Ukweli huu wanaujua pia hata wale
walioibukia kwenye siasa za upinzani. Ndio hao hao wanaoanza kupiga porojo
kwamba kuna uwezekano mtu anayetoswa ndani ya CCM, atahamia upinzani. Kama hiyo ni kweli, ndio kusema kwamba wagombea na
wanaoapaswa kugombea nafasi hiyo ya urais wapo CCM. Na itaingia kwenye
kumbukumbu mgombea wa CCM aliyetoswa kwenye urais, amekimbilia upinzani.
Ataonyesha uroho wake wa madaraka.
Ataonyesha hafai kuungwa mkono na Watanzania. Ikumbukwe kuwa
urais ni nafasi moja inayotokea kwa Mtanzania mmoja kila baada ya miaka mitano
au 10 kwa vipindi viwili.
Hii inaonyesha kuwa Watanzania wote hatuwezi kuwa rais wa
nchi hii. Hivyo ili iendelee, lazima tuache tamaa zetu. Wote hatuwezi kuwa rais
kwa kipindi cha miaka mitano au 10.
Tuvumiliane, tuheshimiane na pengine tuwe na uzalendo halisi wa
chi yetu Tanzania. Uzalendo uliochochewa
kwa kiasi kikubwa na uwapo wa chama tawala CCM. Chama chenye nguvu na ushawishi
kwa Watanzania wote.
Ni nani anayeweza kusimama na kuthubutu kukisema chama hiki
kuwa hakina mvuto, hali ya kuwa ndicho kinachosikilizwa kimtaje mtu wa kusimama
kama mgombea urais?
Chama kilichokufa kitatoaje rais kila msimu wa uchaguzi? Hata
wale wanaosema hayo, nao hukaa chini na kusema fulani anafaa, yule akisimama
atasumbua na maneno nk. La kushangaza, wote wanaotajwa kwa mazuri au kwa mabaya
wanatoka CCM?
Hii ni dalili ya wazi wazi kuwa mwenye uwezo wa kugombea
urais wa Tanzania Bara na akaungwa mkono na Watanzania wote atatoka CCM na atakuwa
rais wa Watanzania wote.
Kama hivi ndivyo, basi ni jukumu la CCM wenyewe kuhakikisha
kwamba mtu anayeweza kupewa nafasi hiyo ya kugombea urais ni sahihi na pengine
asilazimike kusafishwa na dodoki ili aonekane msafi kwa Watanzania wote.
Mungu ibariki Tanzania.
+255712053949
No comments:
Post a Comment