https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, August 29, 2015

MGODI UNAOTEMBEA: Lowassa haaminiki, haeleweki, hafai kuwa rais wetu

NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM
UNAPOTAKA kuzungumzia jambo zito kama Uchaguzi Mkuu wa nchi, katu hupaswi kutanguliza ushabiki. Ushabiki ni mbaya mno. Unachochea kuaminisha watu ukweli wakati ni uongo. Kutafutwa rais wa nchi si kama mchezo wa kumbolela. Mchezo wa kombolela unaweza kuvunjwa wakati wowote na kuanza upya. Lakini si kupatikana rais, au kiongozi wa kuongoza taasisi nyeti kama Ikulu ya Tanzania.
Mgombea urais wa Chadema Mheshimiwa Edward Lowassa, pichani. Makamu wake ni Juma Duni Haji.
Tukifanya makosa katika kuchagua mtu mwenye weledi na nguvu ya kuitumikia nchi yetu na watu wake, hakika tutajilaumu kwa miaka mitano hadi 10 ijayo. Tutalia na kusaga meno. Ni kutokana na hilo, napinga kwa nguvu zote wote wanaochukulia kwa ushabiki Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, wakiamini kuwa yule wanayemshabikia wao anapaswa kuwa rais. Si sahihi hata kidogo. Kwanini nasema hivi? Kwa miaka kadhaa sasa kumekuwa na vikundi vya watu vinavyofanya kila wawezalo kuwaaminisha kwamba Edward Lowassa, anapaswa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Pombe Magufuli akiwa pichani katika moja ya mikutano ya kampeni inayoendelea nchini Tanzania. Makamu wa Rais wa Magufuli ni Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Vikundi hivyo vilianzia harakati zao tangu akiwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Vikundi hivyo vilisumbua mno. Vilichanganya wengi na kuwaaminisha kutokana na ushabiki wao na nguvu ya kimkakati, sanjari na uwezo wao wa kifedha, hivyo kutaka aungwe mkono kwa udi na uvumba. Pamoja na ushabiki huo, lakini mgombea wao Lowassa hajaweza kuvuka viunzi vya NEC ya CCM, mjini Dodoma. Bila kuangaliwa usoni, Lowassa alikatwa. Siku moja baada ya kukatwa, vikundi hivyo hivyo vikaanza kubadilisha wimbo wa nguvu ya mtandao wa CCM na kuihamishia kwenye upinzani, ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Nguvu hiyo ikawashinda akina Freeman Mbowe na wenzake waliokuwa wakipita huku na kule kuaminisha watu kuwa Lowassa ni fisadi, hapaswi kuachwa atembee barabarani kwa matao hali ya kuwa ameifisadi nchi yetu.

Hatimae wimbo wa ufisadi wa Lowassa ukazimwa, ukaanza kuimbwa mwingine wa mfumo mbovu wa CCM. Ati mfumo ndio tatizo. Tatizo si la Lowassa tena. Wimbo huu wa mfumo ndio unaoimbwa sasa. Kila mtu anaimba huo, ukianzia kwenye vinywa vya wana mtandao wake. Hata hivyo, bado haiwezi kukwepeka kusema kwamba kama tatizo ni mfumo, Lowassa hawezi kukwepa lawama hizo. Hii ni kwa sababu aliitumikia nchi kwa miaka zaidi ya 35. Alikuwa ndani ya chama cha CCM na Waziri Mkuu pia. Hizo ni nafasi nyeti na kubwa mno zilizokuwa kwenye mfumo huo huo.
Kama hajaweza kuufanyia kazi mfumo huo, basi bado hana sifa ya kuwa Rais wa Tanzania. Kuna mengi ninayoweza kuyasema juu ya Lowassa. Kubwa ni kuona mgombea huyo wa UKAWA hana sifa na hafai kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lowassa haaminiki, haeleweki na hafai kuwa rais. Kama aliweza kuondoka kirahisi tu ndani ya chama chake eti kwa sababu hakijamteua kugombea urais, anaweza pia kuondoka ndani ya Chadema. Atawaacha watu wake kwenye mataa. Atafanya apendavyo.

Ikitokea bahati mbaya akaukosa urais wa Tanzania, Lowassa anao uwezo wa kuaminisha mashabiki wake kuwa ameonewa, ameibiwa, hivyo wana mtandao wake wapinge matokeo hayo. Na kwa kuwa mgombea huyu ana usaka urais kwa udi na uvumba, uwezo wa kuwadanganya watu wake juu ya matokeo hayo hasi ni mkubwa mno. Vyema watu wakajiandaa kisaikolojia. Endapo mgombea wao atashindwa, wawe tayari kukubali matokeo.

Lowassa yeye kuhamia Chadema si kwa sababu anakipenda, ila anachopenda ni urais tu. Na ndio maana hata kuvaa sare za Chadema anaona shida. Hataki kuvaa mavazi hayo yaitwayo magwanda.  Angeweza kuhamia hata kwenye chama kinachoitwa mti, kama angehakikishiwa urais. Mara baada ya kukutana wachuuzi wa kisiasa, hawawezi kukataa lifti hiyo. Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, anachoangalia ni namna gani Lowassa atakijenga chama chao, hata kama atashindwa kuwa rais wa Tanzania, kama mwenyewe anavyohaha kuupata. Pamoja na yote hayo, kila Mtanzania anapaswa kujua urais ni mipango ya Mungu. Kama Mungu hajakuandikia, hata ufanye nini, huwezi kuipata nafasi hiyo.

Hivyo lazima tuwapime hawa wataka urais. Kwangu mimi Lowassa hastahili kuwa rais wa nchi hii. Si mvumilivu. Anachoangalia yeye ni maslahi yake ya urais tu. Katika mfululizo wa makala zangu, niliwahi pia kukosoa washauri wa Lowassa. Nilisema hawajielewi. Ni baada ya kuona wanamuandalia matukio ya kukutana na wananchi, wakati wanajua fika mtu wao amezuiwa na chama chake, kama ilivyokuwa kwa akina Bernard Membe, January Makamba na  Fredrick Sumaye. Lowassa aliendelea. Hii ni dharau na pengine alijiona yeye yupo juu zaidi ya viongozi wa CCM.
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa waliizungumzia hali hiyo kama sababu moja wapo itakayomfanya Lowassa akatwe. Na kweli alikatwa. Alikatwa licha ya kuaminisha watu kuwa ana nguvu kubwa ndani ya CCM. Kwamba anaweza kuyumbisha chama kama atakatwa. Hakuna kilichotokea zaidi ya marafiki zake akina Hamis Mgeja walioamua kumfuata UKAWA.

Hatuwezi kuutafsiri uchaguzi huu kishabiki. Tutaiweka nchi yetu katika mashaka makubwa. Mtu anafanya bidii kubwa kuingia Ikulu. Anatumia bajeti kubwa, wengine wananuliwa ili waingie kwenye mkumbo wa kushabikia mtaka urais bila kuangalia athari wanazoweza kuipatia nchi yao. Hii haikubaliki na haivumiliki pia. Tuwe wazalendo na tuwe makini na wasaka urais hawa. Kama kweli tunataka mtu wa kuongoza nchi yetu, basi Dr John Pombe Magufuli anafaa. Na kama tunahitaji chama, CCM ndio chama kilichojiweka kitaasisi  na kujiitofautisha na vyama vingine vya siasa. Kama kweli unayo nia thabiti na mawazo na Tanzania, katu huwezi kuifananisha CCM na Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD ambao kwa maslahi yao wameamua kuungana ili eti waisumbue CCM katika Uchaguzi Mkuu. Hawatafanikiwa.

Ni muungano wa vyama vinne vinavyojiita UKAWA, lakini havina hadhi ya kupewa nchi yetu. Wanajiendesha kwa matukio. Hawaeleki kichwa wala mguu. Huu ndio ukweli. Tuhubiri ukweli ili kila mtu afahamu. Hii ni kwa sababu tunatafuta viongozi wetu na si viongozi wa familia zetu. UKAWA ni muungano wa kisanii. Wapo kwa maslahi yao binafsi na vyama vyao. Kama wangekuwa na maslahi na Taifa hili, katu wangetafakari mara mbili juu ya kuwachukua makada wa CCM waliyokatwa kwenye mbio za urais. Sina maana kwamba ni dhambi kwa mtu wa CCM kuhamia upinzani, ila hatuwezi kuwa na wanasiasa vigeu geu na kuwaamini haraka kiasi cha kuwapa nchi yetu kama inavyofanywa kwa Lowassa.

Katika ufunguzi wa kampeni za CCM zilizofanyika viwanja vya Jangwani, rais mstaafu, Benjamin William Mkapa, aliwaita wapumbavu, malofa wote wanaosema kuna vyama vitawakomboa. Hoja ikabadilishwa. Wakaanza kuzusha kuwa Mkapa amewatukana Watanzania. Wameshindwa kujua kwamba neno upumbavu si tusi. Mtu ambaye alikuwa akiongoza mashambulizi ya kumtusi Lowassa akiwa CCM, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, aliwahi kutoa neno kama hilo akiwa Bungeni Dodoma.
Kwa kauli yake akatafsiri neno hilo kuwa, namnukuu Sugu. "NAOMBA TAIFA LIELEWE UPUMBAVU SIO TUSI, NI STUPIDITY, LACK OF KNOWLEDGE OF UNDERSTANDING," mwisho wa kunukuu. Kwakuwa wanajiendesha kimatukio, Chadema na UKAWA wote wakajifanya hawajui kauli hii ya Sugu. Kwa tafsiri isiyokuwa rasmi katika lugha ya Kingereza, upumbavu ni mtu asiyeelewa hata akielimishwa. Hata vitabu vya dini vimetumia neno upumbavu bila kificho. 

Kama kuna watu wanawaaminisha wenzao kuwa kuna vyama vya upinzani vitawakomboa, hali ya kuwa wanajua fika ni TANU na ASP pekee ndio wamewakomboa Watanzania, kwanini neno upumbavu lisitumike? Mkapa hana makosa. Na wajinga, wapumbavu hawawezi kuisha duniani. Leo hii mtu kwa kuwa anautaka urais, ndio anawatembelea mama lishe, wajasiriamali wa Tandale, miaka yote akiwa Waziri Mkuu alikuwa wapi? Unawajazia mafuta bodaboda ili wafanye maandamano yasiyokuwa rasmi, ikitokea umeshindwa, utawajua? Haya ni mambo yanayoshangaza mno. Na yanaendeshwa kishabiki.


Na mashabiki hao hawataki kujiuliza maswali haya ambayo ni muhimu mno kwa mustakabali wa Taifa lao, Taifa linalojivunia amani na upendo. Mtu waliyemnadi kila kona wakimuita fisadi, leo wanawezaje kumsafisha kwa haraka haraka kiasi hiki? Muungano wa UKAWA ulikuwa ni kuhusu Katiba Mpya, je ilikuwaje waingize hadi kwenye urais, ubunge na udiwani ambao kwa bahati mbaya yapo majimbo, kata ambayo wagombea wa vyama hivyo wamechukua fomu bila kuangalia makubaliano yao? Jimbo la Mwanga, Ubungo, Segerea na kwingineo wameshindwa kutambua muungano huo. Wanawezaje kupambana na mfumo wa CCM kwa kutumia viongozi waliolelewa na mfumo huo huo wa CCM?  Wamesahau vipi kashfa za Lowassa kwa kipindi cha siku moja? Ikiwa viongozi wa Chadema, walimwambia Lowassa kama anabisha yeye sio fisadi aende mahakamani, inakuwaje UKAWA hao hao wawatake Watanzania wenye ushahidi wa ufisadi wa Lowasa waende mahakamani na kusahau kuwa waliutangazia umma kwamba wanao ushahidi juu ya Lowassa?


Maswali haya yanasikitisha na kuumiza kichwa. Hii ni kwa sababu mashabiki hao wanaendelea kuaminisha watu kwamba Lowassa ndio anafaa. Si kweli. Angekuwa anafaa angeupata urais ndani ya CCM. Na kwakuwa hafai na anajiaminisha anafaa, ndio hapo anapohama kwa kujivunia watu anaokubaliana nao na wenye uchu wa madaraka. Watanzania waliangalie hili mara mbili mbili. Tusichague mtu kienyeji tu au kwa kuhadaiwa na wenzetu. Na tusiamini vikundi vya watu wanaoaminisha uongo kwamba CCM imechokwa, haiwezi tena kuwatumikia Watanzania. CCM bado ina nguvu na mvuto wa kuwaongoza Watanzania. Changamoto zinazojitokeza wanachama wenyewe na Watanzania wataendelea kuzifanyia kazi.

Kuhusu upepo wa mabadiliko, mabadiliko mazuri ni ya kubadilisha viongozi ndani ya CCM na si nje ya CCM. CCM ina uwezo mkubwa wa kuisimamia nchi yetu, kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano ambao wapinzani, hususan wa UKAWA hawawezi kuutumikia kamwe. Magufuli na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Tanzania Bara ndio machaguo halisi, huku upande wa Zanzibar, Dr Ali Mohammed Shein akiwa na mvuto wa kuwatumikia Wana Zanzibar. Huo ndio ukweli. Wanaopita pita majumbani mwetu, mitaani kwetu, tuwape msimamo wetu kuwa chaguzo letu ni Magufuli na CCM ni chama chetu na kwa maendeleo ya nchi yetu.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema enzi za uhai wake; “Bila CCM imara nchi itayumba”.
+255 712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...