Joachim Mushi, Arusha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kikifanikiwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kitahakikisha mgambo wa halmashauri ya jiji hawawasumbui kwa kamatakamata za wafanyabiashara ndogondogo ambao wengi wao ni akinamama pamoja na vijana.
Kauli hiyo imetolewa leo na mgombea mwenza nafasi ya urais tiketi ya CCM, Bi. Samia Suluhu alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika mkutano uliofanyika uwanja wa Kilombero Jimbo la Arusha Mjini na kuhudhuriwa na umati wa wanaCCM na wananchi wengine.
Akinadi ilani ya CCM alisema chama hicho kimeandaa utaratibu mzuri wa fursa kwa akinamama na vijana wanaofanya biashara ndogondogo hivyo itakuwa ni marufuku kwa mgambo wa jiji kukamata biashara za akinamama na vijana wanaojitafutia ridhiki mjini.
"Iwapo CCM itafanikiwa kuingia mjini naomba wale mgambo ambao uishi kwa kutegemea kukamata kamata bidhaa za akinamama watafute kazi nyingine ya kufanyanya...hatutaki mgambo wa kufanya kazi hizo ni marufuku," alisema mgombea huyo mwenza wa CCM, Samia Suluhu.
Alisema Ilani ya CCM imepanga kujenga viwanda vya kuchakata madini ili kuhakikisha vijana wanapata ajira na kuweza kukuza vipato vyao, na kufufua viwanda vilivyosimama kikiwemo cha 'General Tyre' ikiwa ni mpango wa kumaliza tatizo la ajira kwa vijana.
Aidha alisema mpango mwingine ambao upo kwenye ilani ya CCM ni kushughulikia tatizo la mikataba ya ajira ya madereva wa magari madogo na makubwa, "Tukifanikiwa kuingia Ikulu kazi ya kwanza tutakayoipa Wizara ya ajira ni kuhakikisha inafanya kazi ya kushughulikia mikataNa ba ya ajira kwa madereva wa magari madogo na makubwa," alisema Bi. Suluhu.
Aliongeza Serikali ya CCM itaunda ufuko wa maji kuhakikisha huduma za maji zinakuwa za uhakika kwani Mkoa wa Arusha unashughuli nyingi na idadi ya watu inakuwa kila uchao. Serikali ya CCM imepanga kushughulikia suala la rushwa na vitendo vya ufisadi, uzembe ili kuhakikisha kasi ya maendeleo inaongezeka.
Awali kabla ya mkutano wa Arusha Bi. Suluhu alifanya mikutano katika majimbo ya Hai, Siha na Arumeru yaliyopo mikoa ya Kilimanjaro kabla ya kuingia Mkoani Arusha. Akiwa katika majimbo hayo mgombea aliinadi ilani ya CCM pamoja na kuwanadi wagombea ubunge na madiwani wa CCM wa maeneo hayo.
Ambapo alisema Serikali ya CCM imepanga kuboresha huduma za afya, elimu, uwezeshaji wa vijana na akinamama ikiwa ni pamoja na kutenga shilingi milioni 50 kwa kila kijiji kwa ajili ya kuwainua akinamama na vijana.
No comments:
Post a Comment