Na Mwandishi
Wetu, Dar es Salaam
HALI imezidi
kuwa tete katika Uchaguzi wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea Ubunge, Jimbo
la Handeni, wilayani Handeni, mkoani Tanga, baada ya kubainika mapendekezo
yaliyofikiwa na Kamati ya Siasa na Maadili hayajafikishwa kwenye Kamati Kuu,
kwa sababu ya kuwabeba baadhi ya wagombea waliokuwa kwenye mchakato huo.
Wagombea wa Ubunge CCM jimbo la Handeni, Dr Seif Mhina, John Salu, Chifu Msopa, Mboni Mhita, Ahmed Bwanguzo, Ramadhan Mahiza na Kambi Mbwana mwenye koti, walipokuwa kwenye kampeni hizo Handeni.
Katika
matokeo yaliyotangazwa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Handeni, Salehe
Kikweo, yalionyesha kuwa mgombea John Salu, aliongoza, lakini alikiri kuwa hayo
si matokeo halisi kwa sababu kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa kanuni pamoja na
wagombea watano kupita njia za panya, vikiwamo vitendo vya rushwa kwenye
mchakato huo wa Ubunge Handeni.
Akizungumza
kwa hisia kali, mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, Ramadhan Mahiza, aliuambia mtandao huu kuwa ofisi ya CCM Handeni, imeidanganya Kamati Kuu, chini ya
mwenyekiti wake wa CCM Taifa, Mh Jakaya Mrisho Kikwete, kutokana na ripoti na
mapendekezo ya vikao halali kutofika mezani kwa ajili ya kujadiliana juu ya
kumpata mtu anayekubalika kwa wananchi wote.
Alisema
katika mchakato huo wa ubunge Handeni, wapo wagombea walioguswa moja kwa moja
kutoa rushwa na kugawa madera ambayo waliokamatwa walikiri, hivyo suala hilo
kumalizwa kwa kutoa mapendekezo ya kuwaengua wagombea watano wa nafasi hiyo ya
ubunge Handeni.
“Katibu
Kikweo alitueleza kwamba hakuna haja ya kuweka mgomo wowote, kwa sababu mshindi
halali atajulikana baada ya vikao vya Kamati ya siasa na maadili kukaa, kamati
ambazo kwa maslahi makubwa ya kulinda hadhi ya chama ilipendekeza watu hao
waunguliwe,” alisema Mahiza na kushangazwa na matokeo ya kurudiwa kwa uchaguzi
huo kwa majimbo matano ambayo ni Ukonga, Busega, Kilolo, Makete na Rufiji, huku
Handeni ikiwekwa kando.
Naye Ahmed
Bwanguzo, alisema kwamba kimsingi uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki, huku
ikishangaza kwanini Katibu wa CCM wa wilaya Handeni, ametumia nguvu kubwa
kuwabeba baadhi ya wagombea mchana kweupe pamoja kushindwa kutumia haki ya
msingi ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa.
“Huwezi
kuwapeleka washindi ambao hawana uwezo wa kujenga hoja jukwaani, wakiwamo wale
waliotumia nguvu kubwa ya kifedha ili washinde katika uchaguzi huo, hivyo sisi
kama miongoni mwa wagombea hao hatukubaliani na matokeo hayo na kila aliyeguswa
na tuhuma haki itendeke,” alisema Mtemi.
Mgombea
mwingine Kambi Mbwana, aliyesema kuwa haoni
kwanini uchaguzi huo umesiginwa kwa makusudi, hali inayoweza kukiangusha chama
tawala katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
“Kimsingi
hakuna mgombea anayejua amepata kura ngapi na wapi amekosa, maana hata huyo
Salu anayedaiwa ameshinda amepewa ushindi wa jumla na hakuna anayejua namna
gani mchakato huo umefanyika, ndio maana ofisi ya CCM wilaya iliamua kufanya
siri, huku kila mgombea akiambiwa jambo la kumpa moyo,” alisema Mbwana.
Naye Chifu
Msopa alisema kwamba hawawezi kukubali mtu mmofa afanye mambo kwa maslahi yake,
hivyo wagombea wote wa ubunge watasusia mchakato wa kampeni katika jimbo la
Handeni, kama hali ya kubebana itaendelea dhidi ya Katibu na washindi wake
aonao wanafaa kuliko wengine.
“Hatutaki
kuendelea kuwa waoga huku wachache wakiendelea kuiharibu CCM yetu, uchaguzi huu
urudiwe au kufuata maagizo ya Kamati ya Siasa ya wilaya na ile ya Maadili
ambayo kwa bila kujua kwanini, Katibu aliyaweka kando mapendekezo hayo na
kufanya anavyotaka mwenyewe,” alisema Msopa.
Kwa kipindi
cha wiki moja sasa jimbo la Handeni limekuwa kwenye mgogoro mkubwa kati ya
viongozi wa CCM wilaya ya Handeni na wagombea ubunge ambao kwa kiasi kikubwa
wameonyesha kuchukizwa na mwenendo mbovu wa katibu wa CCM handeni, ambaye
ameendelea kuwabeba wagombea, wakiwamo wale waliotajwa kwenye kashfa za rushwa.
No comments:
Post a Comment