NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM
INASHANGAZA na kustaajabisha mno. Maisha ya Watanzania
yanapotaka kuingizwa mtegoni kutokana na tamaa za watu wachache walioungana kwa
ajili ya kuitafuna nchi. Hii ni hatari zaidi ya hatari ya kukutana na simba
mwenye njaa kali. Ndivyo unavyoweza kusema unapotaka kuelezea aina ya siasa za
Mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Edward Lowassa.
Lowassa anayeonyesha kuwa ana njaa kubwa ya kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa kushoto akiigiza kutoa nauli ya daladala alipokuwa kwenye ziara yake jana jijini Dar es Salaam.
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli akizungumza katika ufunguzi wa kampeni zilizofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Si dhambi kuwa na kiu ya kuwa mtawala, ila mbinu
zinazotumika ndio zinazotia mashaka. Wajuzi wanajiuliza bila kupata majibu
sahihi. Tangu alipokuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lowassa amekuwa
akitumia nguvu kubwa. Haswa nguvu ya kifedha. Amekuwa akinunua makundi ya watu ili wamuunge mkono. Ingawa
wapo wanaomuunga mkono kwa mapenzi yao, lakini robo tatu ya hao wenye mapenzi
nao, hakika wanavutwa na mbinu nyingine, zikiwamo hizo za fedha.
Hilo ndio tatizo lake. Na ili kuonyesha kwamba anakubalika,
vikundi hivyo vinavyomuunga mkono, ndivyo vinavyokaa na kutunga hadithi, filamu
za kuaminisha kukubalika kwake. Mapema wiki hii, siku ya Jumatatu, Lowassa
aliibukia kwenye daladala za Gongolamboto.
Eti amekwenda kujifunza jinsi maisha ya Watanzania wengi wa
jijini Dar es Salaam wanavyoishi katika suala zima la usafiri. Ndio, watu
wanaishi kwa tabu. Na pengine suala la usafiri jijini Dar es Salaam ni tatizo
kubwa. Wengi wanapoteza muda barabarani. Foleni zisizoeleweka au hata kuingilia
dirishani kwa wingi wa wawahitaji wa daladala hizo.
Hata hivyo Lowassa ameshindwa kupata uhalisia wa adha hizo.
Hii ni kwa sababu kwanza amekaa kwenye kiti cha daladala na kusubiri apigwe
picha. Hii inaonyesha ni tukio la kupangwa na pengine hata hao wenye daladala
walijua kinachoendelea na walimuwekea mazingira mazuri bwana mkubwa wao huyo
anayependa ujiko, sifa. Kama huu ni uongo, basi upo karibu na ukweli. Najiuliza tu,
huyu mtunzi wa filamu ya Lowassa juu ya daladala aliyokwea, hakujua kwamba adha
kubwa ipo alfajiri na zaidi daladala za Mbagala, Kimara, Mbezi? Nashawishika
kusema kwamba dereva wa daladala lenye usajili T 917 CWS pengine na konda wake
walijua kila kinachoendelea na wao walilipwa ujira wao.
Haya ni maigizo yanayoendelea kuwatokea Watanzania. Ziara ya
Lowassa au kupanda kwake daladala kunatafsiriwa kwamba alikuwa akijifunza adha
ya usafiri jijini Dar es Salaam. Sawa, lakini vipi ajifunze kwenye kampeni?
Leo? Mbona kama amechelewa? Sisi tumeshazoea shida zetu, dhiki zetu, ajabu wapo
wanaoanza kujifunza shida zetu leo!
Sawa anajifunza, vipi hajachelewa mtu huyo? Anajifunza
wakati ameshawahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Rais Jakaya Mrisho
Kikwete kabla ya kujiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond iliyomuweka katika
uchafu mkubwa. Uchafu uliopaliliwa kwa kiasi kikubwa na wanasiasa kutoka vyama
vya upinzani. Wanasiasa ambao leo uchafu huo wameuweka kando na badala yake
wanahubiri mazuri yake bila haya wala soni juu ya kigogo huyo wa zamani wa CCM.
Watanzania hawahitaji mtu anayejifunza shida zao leo. Hawezi
kuzijua zote. Hatakuwa na uchungu nazo kamwe. Tunahitaji mtu aliyejifunza shida
za watu kabla ya kipyenga cha urais. Tunahitaji kiongozi makini, mchapa kazi na
mwenye afya tele. Hatuhitaji kiongozi atakayetupa hofu ya utendaji kazi wake na
pengine kutia shaka juu ya utawala wake.
Ukijiuliza mengi juu ya Lowassa, utapata jibu sahihi kuwa
wanaomzunguuka hawajui wanachokitenda. Huyu anayemuandalia matukio, mtunzi wake
wa filamu hafahamu uhalisia na tabu zetu tunazokutana nazo Watanzania. Watuache
kama tulivyo.
Unaweza kujiuliza swali dogo tu, ziara ya Lowassa itakuwa na
majibu gani akifanikiwa kuuupata huo urais anaouhangaikia kwa udi na uvumba?
Je, atawanunulia magari kila mtu? Ninachokiona ni mwendelezo wa safari za
kuwadhihaki Watanzania. Hadaa!
Watanzania wamepoteza Imani. Kwa bahati mbaya, mtu anahaha
katika vijiwe vya daladala, masokoni kuwaaminisha kwamba anaguswa na shida zao,
wakati anamiliki utajiri wa kutupwa. Watoto wao, maswahiba zao na wana mtandao
wenzao wanaishi kitajiri huku wakiwa na ndoto za kuwa viongozi wakubwa endapo
mwana mtandao mwenzao ataukwaa urais!
Hatuwezi kwenda hivyo. Wakati huu wa kuelekea kwenye
uchaguzi mkuu, ni vyema tukawahoji na kuwachunguza watu wa aina hii.
Tuwachunguze ili tuone hayo machungu yao kwetu yapo kwa kiasi gani. Haiwezekani
upande daladala leo baada ya kukatwa kwenye mbio za urais wa CCM! Usingekatwa
je? Na huko kote uendapo, unahubiri madudu ya CCM, chama
kilichokupa nafasi ya juu kiasi cha kuwa Waziri Mkuu wa nchi. Huo uchafu wa
chama chako cha zamani umeanza leo? Usingekatwa ungethubutu kukikosoa chama
chako? Najionea filamu isiyokuwa na uhalisia inayochezwa na
Lowassa. Pengine huu ni wakati muafaka sasa wa kuiboresha filamu hiyo ili iuzwe
sokoni kama zinavyouzwa zile za akina Vicent Kigosi ‘Ray’, Jacob Stephen na
wasanii wengine nyota.
Nalisema hili kwa uchungu kwa sababu katika kadhia hii, wapo
watu wanaoendelea kuamini porojo za filamu hii, wakiamini kuwa watu hao au
vikundi hivyo vina uchungu nao. Si kweli. Kama uchungu huo upo kweli, basi
angeuonyesha wakati ni waziri mkuu. Kama uchungu huo upo kweli, angeonyesha alipokuwa mbunge.
Watanzania wasilishwe uongo. Hatukatai kumpenda au kumheshimu mtu, lakini
katika suala la urais hatuwezi kulipeleka kwa mazoea tu. Tujiulize sisi na
tuwaulize wao wanaotaka kutuongoza.
Kwanini unasaka sana Ikulu? Kwani huwezi kuishi bila kuwa
rais wetu? CCM walipokukata umeondoka, vipi Chadema ukishindwa utahamia wapi?
Katika kuisaka kwako Ikulu umekuwa ukitumia gharama kubwa, fedha hizo unapata
wapi? Ukishakuwa rais utazirudishaje? Maswali ya aina hii ni muhimu mno. Hii ni kwa sababu
tunaowauliza wakishatujibu tutajua uhalisia wao. Inashangaza mno! Kama kweli
una uchungu na shida za Watanzania, fedha hizo unazomwaga kwa wanaokuunga mkono
kwanini usizipeleke kwenye miradi ya maendeleo ili wananchi waishi vizuri na si
kutoa kwa wachache ili wakusafishe kwenye mbio zako za urais?
Huu ni wakati wa kusema ukweli. Kuelimishana na kusemezana
bila woga. Ikulu ni mahala patakatifu. Hatuwezi kuifanyia mzaha taasisi nyeti
kama Ikulu. Mwenendo wa Lowassa juu ya mbio zake za kuwania urais zinashangaza
na kutia mashaka! Ni tofauti na wengine, akiwamo Dr John Pombe Magufuli,
ambaye kiuhalisia anaonyesha ukomavu na uhitaji kweli wa Watanzania. Chuki hizi
au hamu hii kwanini isiwe pia kwa makada wengine kama vile Bernard Membe,
Samuel Sitta, Makongoro Nyerere, January Makamba, Mwigulu Nchemba na wengine
ambao ingawa wameikosa nafasi hiyo, lakini wamevunja makundi yao na kumuunga
mgomnbea wao wa CCM, Magufuli. Ndio uungwana. Ndio demokrasia tunayoijifunza
kuisema kila tunapokatiza.
Tena wengine wamekubali kushindwa huku wakikikosa kabisa
nafasi ya kuja kuwa rais wa Tanzania kwa miaka 10 ijayo, hususan wale ambao
umri wao umeonekana kuwa mkubwa, ukiacha wale vijana kama vile Mwigulu, Dr
Khamis Kigwangwala na wengineo. Wakati nasema haya, naungana na Rais Mstaafu wa Awamu ya
Tatu, Benjamin William Mkapa, aliyewapasha wapinzani hususan wa wanaoitwa UKAWA
kuwa ni wapumbavu na malofa. Ndio, maana wanachokifanya mitaani kinaonyesha
ulofa wao, upumbavu wao.
Na wale wanaopigia makofi kila kinachosemwa au kufanywa na
viongozi wao wa UKAWA na kuona ni sahihi nao ni wale wale. Waswahili wamesema,
ndege wafananao ndio wanaoruka pamoja. Kuruka huko pamoja kwa watu wa UKAWA na
wafuasi wao bado hakutupi woga wa kusema kwamba filamu ya Lowassa haina
uhalisia. Mtunzi wa filamu hizo iwe ni daladala, kula magengeni au
kutembea kwa miguu kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, anapaswa kuweka uhalisia
na ajibu maswali ya Watanzania kuwa kwanini ni mtu huyo anayafanya hayo kwakuwa
anaitaka Ikulu?
Kwa kumalizia tu, ni bora Watanzania wakajiridhisha na
mwenendo huu. Watanzania wasiwe watu wa kusikiliza na kuamini. Kuangalia na
kuamini. Hilo ni jambo baya linaloweza kuwagharimu katika miaka 50 ijayo. Watu hao wanapopita kwenye mitaa yao
wakiendelea na maaigizo yao, wao wasiamaini moja kwa moja kwamba wameguswa na dhiki
zao, huenda wamekwenda kuwasanifu wakati huu wa kuomba kura. Huo ndio ukweli. Na ndio maana nasema; filamu ya Edward
Lowassa haina uhalisia kwa Watanzania masikini.
+255 712053949
No comments:
Post a Comment