https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, November 09, 2012

Wanamuacha adui, wanapigana wenyewe





 Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
JUHUDI za kukiangusha Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeishiwa nguvu badala yake tunashuhudia wapinzani, wakianza kuvutana wenyewe. Wapinzani wameanza kuvutana, kutukanana au kurushiana makombora ya kila aina.

Jambo hilo ni baya. Sidhani kama wataweza kweli kutimiza azma yao. Zaidi wataipa ushindi wa kishindo CCM katika chaguzi zake zote zinazokuja mbele yake.

Nasema hivyo maana wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekuwa wakiwadharau wenzao wa Chama cha Wananchi (CUF), wakisema wameishiwa.

Sawa, huenda ni kweli CUF wameishiwa, lakini hizo kejeli, zingefaa kutolewa na wafuasi wa CCM, wasiopenda kuona chama chao kinatoka madarakani.

Kinyume chake, kejeli na masimango zinatoka kwa Chadema, chama kinachojiita kuwa ni namba mbili baada ya CCM.

Wakati haya yanaendelea, ni vigumu sana kuamini kweli CCM inatong’oka. CCM kung’oka ni ngumu. Haitang’oka kamwe. Kwanini nasema hivyo? Wapinzani wamemuacha adui yao na wameanza kupigana wenyewe.

Kwa bahati mbaya, muunganiko wa vyama vya upinzani umekuwa mgumu mno kufanikiwa. Hii ni kuonyesha kuwa wote wana malengo ya kuongoza. Inaonyesha dhahiri nao wana kiu ya kujinufaisha wao na sio Watanzania wao.


Julius Mtatiro, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara

Haya pia yaangaliwe. Kwa mfano, kila kinachofanywa na CUF leo, lazima kisemwe na kusimangwa na
wapinzani wenzao. Ni ajabu. Hawa wanapigana na CCM au CUF? Ama nao wameona CUF ni adui yao namba moja?

Kama ni kweli CUF ni adui ya Chadema, basi wanapaswa wapigane kwanza wao kwa wao, kabla ya kuigeukia CCM ambayo ipo madarakani. Haya yasemwe bila kuficha, hata kama yatapokelewa kwa shingo upande na wenye vyama vyao.

Sote tunajua siasa za Tanzania. Lakini, ukiangalia utagundua kwamba msigano zaidi unahamia CUF na Chadema, hivyo nguvu zao kwa chama tawala ni ndogo mno.

Jambo hilo linaipa ushindi zaidi CCM, ingawa wakati mwingine porojo, propaganda hutungwa kwa umahiri wa aina yake kuaminisha wanachotaka wao.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, baadhi ya watu wa Chadema walikuwa wakipita katika maeneo mbalimbali ya Bagamoyo wakisema kuwa mgombea wao amejitoa, hivyo wahamie Chadema.

Sawa hizi huenda ni mbinu za kampeni, lakini zinaashiria kuwa kama ni kweli, basi wapinzani kwa wapinzani wameamua kukomoana na kuiacha CCM iendelee kutesa kileleni.

Na mfumo huo umeifanya CCM iibuke kidedea katika kata nyingi zilizofanya Uchaguzu Mdogo na kuwaacha wapinzani wakigawana viti sita tu.

Huu ni ushindi wa kishindo. Watu walitarajia labda CCM ingeanguka zaidi katika uchaguzi huo, lakini Watanzania haswa wale wapenzi wa CCM wakishuhudia mafanikio makubwa katika Uchaguzi huo mdogo.

Chadema wamekuwa wakipita huku na kule kusema kuwa CUF wanaiga kila wanalofanya, ikiwamo harakati zao walizozipa jina la Movement for Change (M4C), vugu vugu la mabadiliko katika harakati zao za operesheni Sangara huku wapinzani wao nao wakizindua zao zilizokwenda kwa jina la Vision for Change (Dira ya Mabadiliko).

Mvutano ulikuwa mkubwa mno. Hadi viongozi wa CUF walipotolea ufafanuzi suala hilo, wakisema harakati zao walizindua rasmia mwaka 2010 huku Chadema wao wakizindua kwa mara ya kwanza mwaka 2012.

Sitaki kusema nani yupo sahihi katika vita hiyo, maana nashangazwa na nguvu kubwa ya kudharauliana juu ya vyama hivyo vya upinzani.

CUF na Chadema hawatakiwi kufanyiana umafia, badala yake wasaidiane kila linalowezekana kama kweli lengo lao ni kuingia Ikulu na kuwaongoza Watanzania.

Ukisema hili watashangaa. Watasema hawana imani na CUF maana kuna dalili kubwa kuwa ndugu zao hao wameingia kwenye ndoa na CCM. Wanaogopa nao kuingia kwenye ndoa hiyo.

Ikiwa huo ni ukweli, ina maana sasa njia yao kuu ni kukikashfu kwa kila walivyoweza ili kukichafua zaidi kwa Watanzania? Silaha kubwa ya Chadema ni kuona mikutano yao mingi inahudhuliwa na wananchi wengi, hata kama sio wapiga kura.

Wanashindwa kujua kuwa wengi wanaoingia katika viwanja vya mikutano yao, sio wapiga kura na inapofikia wakati huo hukaa pembeni. Ni hujuma kubwa. Watanzania wengi wakiwamo vijana hawajui thamani ya kura zao.

Ni wepesi mno kuandamana lakini mifukoni mwao, majumbani mwao hawana vitambulisho vya kupigia kura. Utashangaa, mihemko yao, kurusha matusi au kufanya kila wanachoambiwa, wanapata wapi ujasili huo?

Mimi nilidhani CUF, Chadema na vyama vingine vya upinzani vingekaa pamoja kumjadili mpinzani wao, CCM na sio kuanza kuparuana wenyewe, kutumia nguvu kubwa kuhujumiana maana, ukizingatia kuwa dola ipo chini ya chama tawala.

Wafuasi wa vyama hivyo hawatakiwi kusemana, kutukanana au kuambiana lolote lisolojenga siasa za upinzani badala ya kubomoa zaidi. Kama wote nia yao ni kukiangusha chama tawala, kwanini sasa wanaona wao kwa wao ni maadui?

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba na viongozi wenzake, akiwamo Katibu Mkuu wake, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalimu Seif Sharif Hamad aone mpinzani wao ni CCM na sio CUF.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake waone kuwa adui yao si CUF bali ni CCM, hivyo kufanya mikakati ya pamoja kukiondoa madarakani.

Kulisema hili kunahitaji ujasili, maana baadhi yao lengo lao ni kuongoza tu, hata kama sera na mikakati yao ina matege.

Najua yapo mapungufu mengi ndani ya CUF, lakini pia ni kama ilivyokuwa kwa wenzao Chadema, wanaofanya mambo ambayo wakati mwingine yanashangaza. Hayo nayo ni mapungufu, ndio maana wanaona vyama vyote ni adui yao.

Wao wakifanyiana umafia, CUF kuwasimanga Chadema, CCM wanakuwa na kazi ndogo, ndio maana hata ushindi wao unaendelea kuwapo Tanzania.

Hata mwaka 2015, CCM itashinda kwa kishindo, ukizingatia kuwa imewaachia wenyewe wapinzani watoane roho na wao kumalizia kidogo tu ili wakubaliwe na Watanzania.

Ni rahisi CCM kuwaambia wapinzani ni waroho wa madaraka, hawawezi kuwaongoza pamoja na vita ya udini na ukabila inayowezwa kuenezwa zaidi kwa vyama hivyo vya upinzani na watu kuielewa na kuwaweka pembeni.

Huo ndio ukweli. Kwanza wanahesabu viongozi waliokuwapo Chadema na asili zao. Pili wanarudi kwa wale wanaosemwa na wenzao. Yani chanzo cha Chadema kuwadharau CUF na mengineyo mengi, hivyo jibu kuwa hawa ni wadini na wakabila.

Kama hayo yakienezwa na kusomwa na Watanzania, kila mwenye ndoto za amani, kuipenda Tanzania yake, kuona utawala wa haki na sheria, hakika hawezi kuikacha CCM zaidi ya kukichagua tena na tena katika chaguzi zake.

Vyama vya upinzani, vikiwamo CUF na Chadema waone kuwa malumbano yao, kufanyiana umafia ni karata turufu kwa kwa CCM na hawawezi kuindosha madarakani.

Vinginevyo, kazi wanayo.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...