https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, November 13, 2012

Ulimwengu, Samatta ni dira ya soka la Tanzania

      


Mbwana Samatta kulia na Thomas Ulimwengu

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI dhahiri wachezaji wawili wa Kitanzania, Mbwana Samatta na mwenzake Thomas Ulimwengu wanaonyesha namna gani Watanzania wanahitaji kuwekeza zaidi kwenye soka la vijana, maana ndio matunda ya soka letu.

Wachezaji hao wawili wanachezea katika timu ya TP Mazembe ya nchini Kongo (DRC), huku nafasi zao zikiwa muhimu ndani ya timu hiyo. Ingawa katikati ya mwaka huu Ulimwengu alionekana kupwaya kidogo, lakini sasa amezinduka.

Labda ni kwa kuona mwenzake, Samatta anavyozidi kunga’ra ndani ya timu hiyo, jambo lililomfanya aone bado ana deni kwa Watanzania wenzake kwa kuona wanafika mbali zaidi na kucheza soka la kulipwa katika nchi nyingine.

Kabla ya kupata nafasi hiyo, Samatta alionyesha makali yake katika timu ya Mbagala Malket, kabla ya kununuliwa na Mohamed Dewji ‘Mo’ na kubadilishwa jina la African Lyon. Hata hivyo Samatta hakudumu kwenye timu hiyo.

Aliuzwa katika timu ya Simba SC na kufanya njia ya kumpeleka Kongo anapocheza hadi sasa na kuonyesha umahiri wake uwanjani.

Uwezo wake uwanjani na kucheza kwa akili, kumemfanya awe lulu katika timu zote alizochezea, huku juhudi zake zikichangia kuipandisha daraja Mbagala Malket na baadaye kuja kuitwa African Lyon inayocheza ligi ya Tanzania Bara.

Wakati yeye akipita katika njia hiyo, mwenzake Ulimwengu ametokea katika timu ya vijana, Serengeti Boys. Wote ni wakali wawili wanaofanya kazi kwa pamoja TP Mazembe. Wanaishi kama wafalme ndani ya timu hiyo.

Hakika vichwa hivyo viwili ni dira ya soka la Tanzania. Hakuna Mtanzania asiyependa kuona matunda ya vijana hao. Umuhimu wao katika timu hiyo ya nchini Kongo, ni nafasi ya kila mdau wa michezo kuona ana deni kwa vipaji vya Tanzania.

Kila mdau na kiongozi wa soka la Watanzania ajaribu kuvuta picha ya kuwakomboa vijana ili kuwaingiza zaidi katika soka, ukizingatia kuwa ndio ajira kubwa hapa duniani.

Leo hii Samatta anaishi kama mfalme katika timu ya TP Mazembe. Umuhimu wake unatokana na jitihada zake na mguu wake uwanjani. Kujituma kwake na kuweka malengo kumechangia mafanikio yake hayo.

Lakini, tunawezaje kuibua wachezaji wengine na kuwa kama akina Samatta na mwenzake Ulimwengu, ukizingatia kwamba vipo vingi na vimefunikwa na mfumo wetu na kuwafanya vijana waone kazi nzuri ni kukata mkaa vijijini?

Ingawa wapo wachezaji wengine wanaocheza soka la kulipwa, akiwamo Henry Joseph Shindika anayecheza katika timu ya Kongsvinjer ya nchini Norway, lakini hawa wenzake wanawika zaidi pale Kongo.

Uwezekano wa wachezaji hao wawili kusonga mbele zaidi upo. Wakati wowote wanaweza kuondoka Kongo, maana mchango wao ni mkubwa kiasi cha kuifikisha nusu fainali timu yao katika michuano ya Mabingwa Afrika.

Huu ni wakati wa kuthamini na kuangalia harakati zetu za soka. Hadi sasa, Tanzania haina jitihada za kuwekeza kwenye soka la vijana. Ndio maana hata wale wanaopata nafasi za kuonyesha uwezo wao, mara kadhaa ni juhudi zao binafsi.

Hata ligi yetu haina mvuto. Haina ushindani zaidi ya wadau hao kuangalia mechi mbili za Simba na Yanga, wakiangalia idadi kubwa ya mashabiki watakaoingia uwanjani hivyo kuingiza fedha nyingi kwa wakati mmoja.

Wale ndugu zangu wa African Lyon, Kagera Sugar wanapokutana uwanjani, hata madaktari hakuna na wakiwapo gari la wagonjwa (ambulance) hakuna. Juzi katika Uwanja wa Chamanzi, mchezaji wa Coastal Union, Nsa Job, alipoumia gari la wagonjwa halijakuwapo.

Haya ni mapungufu makubwa kwa wasimamizi wa mpira wa miguu, nazungumzia Shirikisho la Soka nchini (TFF), linaloongozwa na Rais wake, Leodgar Tenga.

Kama hivyo ndivyo, tunawezaje kutafuta suluhu ya soka letu? Kama hatuna ligi nzuri, vijana wengi zaidi wanapataje nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi? Kama hatuna ligi ya vijana iliyokuwa bora, vipaji vipya vya soka vinapataje nafasi?

Haya ni maswali ambayo majibu yake yapo katika meza ya Tenga na watu wake. Haya ni maswali ambayo majibu yake yataendelea kuwa kitendawili kigumu kwa watendaji wote wa TFF, maana juhudi zao ni kulipana mishahara na sio kukuza kiwango cha michezo.

Wakati mwingine najivunia mafanikio ya akina Samatta na Ulimwengu, lakini nikiona hakuna juhudi za kuwakuza wengine zaidi naishiwa nguvu. Hata hawa wakichoka, nao watarudi nyumbani kwakuwa hakuna mipango.

Ni wakati sasa wa wadau na timu zetu kuangalia namna gani wanawekeza katika soka la vijana ili wawe na nafasi ya kucheza muda mrefu. Kwa mfano, makocha wengi wenye mipango duniani huwekeza zaidi kwenye soka la vijana.

Pale Uingereza, kocha wa timu ya Arsenal anafikia wakati kushindwa kueleweka kwa kuangalia zaidi vijana ambao wakati mwingine hawana uzoefu. Lakini, kufumba kwake macho na masikio, wakati mwingine anaeleweka.

Lakini Tanzania mambo ni tofauti. Tunaangalia zaidi wazee. Watu ambao maisha yao ya soka ni mafupi mno, kulingana na umri wa wadogo zao. Timu kama Simba, Yanga na zote zinazoshiriki ligi ya Tanzania lazima ione umuhimu wa kuwapa nafasi vijana.

Wafanye hivi kwakujua kuwa hayo ndio matunda ya kuvuna soka lenye mvuto na kasi ya aina yake leo na hata kesho. Vijana nao waone wivu wa kimaendeleo kwa wenzao wanaoishi kwa furaha na amani kubwa nchini Kongo.

Wachezaji kama vile Rashid Gumbo, Mrisho Ngassa, John Bocco, Jerryson Tegete na wengineo waweke mkazo wanapokuwa uwanjani ili iwe nafasi ya kuwapatia maisha mazuri katika mpira wa miguu ulimwenguni.

Wanapopata nafasi ya kupangwa uwanjani, wacheze kwa bidii na kujiuza wenyewe, kama alivyofanya Samatta kwa TP Mazembe. Mechi moja aliyocheza katika Mabingwa Afrika, ilichochea uongozi kuona anafaa kuwamo kwenye timu yao.

Ukweli likatimia. TP Mazembe wakamsajili Samatta katika kipindi ambacho alihitajika bado katika timu yake ya Simba. Kwanini wasije akina Samatta wengine? Kwanini Ulimwengu mwingine asisajiliwe kwingine hata kama sio alipokuwa yeye?

Zipo timu nyingine zenye mvuto wa aina yake Afrika Mashariki na Kati au Afrika Magharibi. Zipo timu kama Al Ahly, Zamalek na timu za Tunisia ambapo wachezaji wao wamekuwa wakionekana sana duniani.

Haya yaangaliwe. Haya yapewe mkazo kwa ajili ya soka la Tanzania. Lazima watu wapambane kwa kutangaza soka la Tanzania, ili kukuza soka letu na kuwafanya wanamichezo wetu wavune fedha nyingi kwa kupitia mpira wa miguu.

Kwa hili la Samatta, Ulimwengu ni somo kuwa mpira unalipa na lolote linaewezekana endapo kila mmoja atafanya kazi kwa malengo.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...