Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
HATA vitabu
vya dini vinatueleza binadamu tuzitii mamlaka halali tulizochagua wenyewe ili
zituongoze. Ndio, inapotokea mtu anakwenda kinyume na maandiko hayo, ni dhahiri hatufai, hastahili kuchekewa.
Kambi Mbwana, mwandishi wa makala haya.
Na kutii
huko hakupo kwa mwananchi wa kawaida tu. Maadamu ni mamlaka halali, hapana
shaka kila Mtanzania wa nchi yetu anapaswa kutii hilo bila kujali dini yake au
itikadi yake ya kisiasa. Kwa bahati
mbaya, tangu kuanzishwa kwa sheria ya vyama vingi, mwaka 1992, kumekuwa na
kasumba ya baadhi ya viongozi wa upinzani, kufanya mambo ambayo ni kinyume,
wakiwa na malengo yao binafsi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli pichani.
Malengo ya
kutafuta sifa ya kuungwa mkono na wafuasi wao bila kujali wanafanya kitu kizuri
au cha kijinga. Bahati mbaya mfumo huo kadri unavyozidi kupewa nafasi na
wapinzani hao, dalili za wazi za kutowesha amani ya nchi yetu inazidi kuonekana.
Kwanini isionekane? Utawekeje tone moja la damu kwenye nguo nyeupe na bado
ukajindanganya kwamba nguo hiyo itaendelea kuvutia? Pamoja na
dalili ya machafuko inayozidi kuonekana, bado hakuna juhudi zinazochukuliwa na
wanasiasa kutoka mlengo wa upinzani, wakiamini siasa za kumwaga damu za
wananchi wao ndizo zinazoweza kuwaweka juu.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pichani.
Hili
haliwezi kukubalika. Watanzania
tusikubali. Tumeshahudia mara kadhaa damu za Watanzania wenzetu zikimwagika
bila soni wala haya. Machafuko ya kisiasa yanayoanzishwa na wanasiasa kama
Arusha, Morogoro na katika maeneo mengine yameendelea kuonekana, huku chanzo
chake kikiwa ni siasa chafu, nyepesi, zisizokuwa na tija kupewa nafasi hususan
na chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kwa mfano,
Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania (Chadema), kwa kupitia mwenyekiti wao Freeman
Mbowe JUZI wametangaza kufanya maandamano na mikutano nchi nzima katika siku ya
Novemba Mosi. Na mikutano
hiyo itafanyika bila kuangalia imeruhusiwa na jeshi la Polisi au itazuiwa.
Inawezekana kuandamana ni halali kwa mujibu wa Katiba, lakini pia busara na
usalama lazima ziimarishwe kwa faida ya nchi yetu.
Kufanya
maandamano yenye viashiria vya uvunjifu wa amani hakuwezi kuruhusiwa hata kama yamewekwa
kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni kwa
sababu si Watanzania wote wanapendezwa na siasa za upinzani. Wapo ambao
hawaungi mkono agizo lolote la upinzani. Na wengine si wafuasi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wala CUF. Isipokuwa wote ni Watanzania. Hivyo endapo hayo
maandamano yatafanyika bila kufuata sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea,
ni wazi kutakuwa ni kupoka haki ya kuishi na kulindwa kwa wengine watakaoathiliwa
na maandamano hayo yasiyokuwa na kichwa wala miguu, kama wanavyotaka kufanya
viongozi wa juu wa Chadema.
Ndio maana
kunakuwa na taratibu. Nani asiyejua kuwa siasa za namna hiyo zimepelekea kifo
cha Mtanzania mwenzetu, mwandishi wa habari Daud Mwangosi kule mkoani Iringa?
Ingawa
Chadema wanasema mauaji hayo yamesababishwa na Jeshi la Polisi, lakini chanzo
kikuu ni ghasia zilizoendeshwa na wao na wakiwa na nia waliyojua wenyewe,
ikiwamo hii ya kujulikana kwa lazima bila kujali athari kutoka kwa baadhi ya
Watanzania wasiokuwa na hatia. Licha ya kifo hicho au machafuko yaliyotokea
katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, wapinzani wameendelea kutembea katika
njia ile ile, wakiamini ndio mtaji wao wa kisiasa ulipo. Hii
haikubaliki. Watanzania tusikubali siasa za kumwaga damu zinazofanywa na
kuhubiriwa na wanasiasa wa upinzani kwa sababu hazina faida kwetu. Tunachafua
tunu ya Taifa letu.
Leo Mbowe
anatangaza maandamano au mikutano isiyokuwa na ruhusa, lakini sidhani kama
katika matukio hayo ataambatana na familia yake. Si ajabu watoto wake watakuwa
wakiendelea na maisha yao iwe ndani ya nchi au nje, huku watoto wa masikini
wakitaabishwa. Kuna vitu
vingi vya msingi ambavyo wapinzani wanaweza kuvifanya kama karata yao katika
siasa za nchi yetu. Nzuri zaidi, wamefanikiwa kuwa katika majimbo kadhaa
wakiongoza kama wabunge, madiwani au mameya. Wakae chini watafute
namna ya kufanya siasa zenye chembechembe za huruma, uzalendo na uwajibikaji
ili iwe njia ya kupaisha gurudumu la maendeleo ya nchi.
Ni wazi
wanayofanya hayana tija. Wanazalisha dalili za ghasia. Ghasia zinazoweza
kutowesha amani ya nchi yetu. Nchi ambayo kila mtu ana haki ya kuilinda na kuidumisha
amani ya Taifa letu kama wajibu wa kila mwananchi.
Kwanini tusijifunze
kutii mamlaka? Kama wapinzani leo hawataki kutii mamlaka na ushauri wowote
kutoka kwenye serikali iliyochaguliwa na Watanzania wengi, hata wao kesho
wakichaguliwa ni wazi wengine hawatawatii. Jana akiwa
mkoani Singida, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli
amewaeleza kuwa vitendo vyao vyovyote vibaya havitavumiliwa. Na pia akasema,
kama wanataka kufanya siasa, basi wafanye kwenye majimbo yao, kwa wale
waliofanikiwa kuwa wabunge.
Kauli ya
Magufuli imekuja baada ya Chadema kutangaza maandamano yao na kuyapa jina la
UKUTA wakisema yatafanyika nchi nzima Novemba Mosi, kama njia ya kupinga vitu
walivyoviita ni udikteta kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye
pia ndio Amri Jeshi Mkuu wa nchi yetu.
Ukiangalia
kwa haraka utagundua kuwa lolote linalosemwa na rais ni agizo kwa watu wa
chini. Ni wazi vyama vya upinzani, ama Chadema mahitaji yao yatakwama.
Yatakwama
kama wataendelea kutumia nguvu badala ya kuweka busara kwa faida ya nchi,
ukizingatia kuwa siasa yoyote iwe ya upinzani au chama tawala inategemea uwepo
wa nguvu kazi ya wananchi. Watanzania
ndio wanaolipa kodi kiasi cha kuvifanya vyama vya siasa vipate ruzuku na
kulipwa mishahara wanasiasa wao. Hivyo badala ya kutaka wamwage damu yao, ni
bora wakawekewa mfumo mzuri wenye tija ili waendelee kufaidi raha ya
uwajibikaji wao.
Ndio maana
nasema wapinzani watii mamlaka. Wamtii Dr Magufuli na chama chake. CCM haikujiweka
yenyewe madarakani. Imechaguliwa na wananchi wengi kutoka mijini na vijijini,
huku wakiamini kuwa mgombea wake, ambaye ni Dr Magufuli ataivusha nchi yetu
salama. Dalili njema
zinaonekana. Utendaji wa Rais Magufuli na safu yake yote imeonyesha wazi kuwa
nchi yetu itapiga hatua kubwa kimaendeleo. Tuitunze amani yetu. Watanzania tuwe
makini na matamko ya wanasiasa mfano wa Mbowe na wenzake kwa sababu hayana nia
njema.
Wakisema
tuwasikilize lakini tuyachuje maneno yao kabla ya kuwafuata kikondoo ili
tusiiweke nchi yetu rehani. Nchi yetu ina kila zuri linaloweza kuifanya iwe
tajiri. Lakini hilo zuri haliwezi kupatikana kama hakuna amani.
Amani
inayotaka kuchezewa na wanasiasa hawa wanaotegemea damu ya wananchi kama msingi
wa maendeleo yao kisiasa na vyama vyao. Vyama vingi vya siasa havijaanzishwa
ili vilete uhasama, chuki na vita kwa wananchi, ila kusaidia kuikosoa na
kuishauri serikali ili viharakishe maendeleo yaliyokusudiwa kwa nchi yetu. Japo nao
wana ndoto za kuishika dola, lakini zipo njia nzuri ambazo kutokana na uongozi
wao, washauri wao wanaweza kukaa na kutafakari njia bora na kuacha njia ya
mkato kwa sababu hazitawasaidia wananchi wao.
Si Dr Magufuli
tu, ila hata angekuwa nani, asingekubali kuona kuna kikundi cha watu kinataka
kutibua uongozi wake, hivyo lazima atakishughulikia tu. Inawezekana Dr Magufuli
ni dekteta kama wasemavyo wapinzani, lakini hakuna sehemu nzuri ya kupambana
naye hadi maandamano? Mbona lipo
Bunge? Bunge ambalo tumeshuhudia hao hao wapinzani wakitoka nje mara nyingi
kuliko siku walizokaa ndani katika mijadala mbalimbali. Sasa kama wanakimbia
ndani ya jengo lenye kazi ya kutunga sheria (Bunge) na wao wakiwa ndio
watungaji wenyewe wa sheria, huku mtaani maandamano yatasaidia kitu gani?
Ni bora
wapinzani wakafahamu kwamba; nchi yetu Tanzania ina mahitaji mengi kuliko hata
kujua kuwa Dr Magufuli ni dekteta au la kama wasemavyo. Ila sisi wananchi
tunajua nchi yetu sasa imenyooka. Hakuna mtumishi mwenye sauti kuliko mwananchi.
Wananchi tunahitaji afya bora, dawa ziwepo mahospitalini, tunaziona, watumishi
hewa wanaendelea kutimuliwa, wawekezaji wanaotesa wananchi wanashughulikiwa,
bajeti bora imetengwa ili kuifanya nchi yetu isonge mbele. Nini tena
tunahitaji? Kuna njia moja nyeti ambayo wabunge, madiwani na baadhi ya mameya
wa upinzani wanapaswa kuipita na si nyingine, haiwezi kuwavusha. Njia yenyewe ni
kushirikiana na serikali kusimamia maendeleo katika maeneo yao katika kipindi
hiki, kuliko kusimamia ajenda ya vurugu na machafuko katika nchi yetu.
Mameya
wawasimamie madiwani na wakurugenzi bila kusahau wabunge, maana ndio kusudio la
wananchi kuwachagua kama viongozi wao halali kwa kipindi cha miaka mitano,
sanjari na kupinga rushwa na ufisadi kwa vitendo maana ndio unaokwamisha
maendeleo ya nchi yetu. Unaweza
ukajiuliza mengi juu ya malalamiko ya wapinzani, mwisho wa siku ukajiona ni mjinga.
Angalia, jana Mahakama Kuu ya Tanzania iliyokaa Morogoro imetupilia mbali kesi
za kupinga matokeo ya ubunge wa majimbo mawili ya Kilombero na Mlimba,
iliyofunguliwa na wagombea wa CCM, dhidi ya wabunge wa Chadema.
Katika kesi
hiyo, aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM jimbo la Kilombero, Abubakary Assenga,
alipinga matokeo ya ushindi wa mgombea wa Chadema, Peter Lijualikali kwa madai
kuwa alitumia lugha za kashfa, huku Godwin Kunambi naye akipinga matokeo ya
mbunge Susanne Kiwango wa jimbo la Mlimba kwa madai ya kutoridhishwa na kampeni
za mbunge huyo. Bado najiuliza, inakuwaje Dr Magufuli ni rais wa Tanzania,
anashindwa kutumia udikteta wake kuwapoka wabunge wote wa upinzani ambao
wamewekewa pingamizi mahakamani kutoka kwa wanachama wa CCM kama wapinzani wanavyoeneza
sumu hiyo ya udikteta ya rais kipenzi cha Watanzania wote?
Badala yake rais
amekuwa kimya, akisuhubiri ama kuheshimu uamuzi wa mahakama. Waswahili wana
msemo wao; ukiwa mwongo, usiwe msahaulifu. Mbali na kuendesha siasa zenye
kuhitaji damu za Watanzania zimwagike, bado wapinzani pia wana sifa mbaya ya
uongo na usahaulifu. Lakini
kwanini tusikubali tu kuwa huu ni muda wa kazi? Hivi vikao vya maandamano na
malalamiko hatuoni vinachukua muda wetu mwingi wa kuipatia maendeleo nchi yetu?
Kwanini vyama vya siasa vyote visivae viatu vya kuhamasisha uwajibikaji,
usisimamiaji na mikakati ya kuipatia nchi yetu maendeleo badala ya kuwaza
vurugu na ghasia?
Inawezekana
upeo wangu wa kufikiri ni mdogo, lakini pia sitaki kuamini kuwa serikali halali
iliyochaguliwa na wananchi wengi, inaweza kukubali kikundi cha watu wachache
waandamane hata wasiporuhusiwa na vyombo vya ulinzi na usalama. Ndio kusema
wenye mamlaka na ulinzi na usalama watajidhatiti si tu watu hao waandamane,
bali pia itasambaratisha hata mkusanyiko wao, jambo linaloweza kuhatarisha
usalama wa wananchi wengine wasiokuwa na hatia. Kamwe tusikubali vurugu.
Tusikubali maandamano batili.
Chadema
wanataka nini? Na kwa faida ya nani?
Ndio maana nawataka Watanzania tuwapuuze
kwa nguvu zote wanasiasa wenye mlengo usiokuwa na tija, wanaotaka nchi yetu iwe
kiota cha vurugu badala ya amani, kama Dunia inavyotambua kwa sifa yetu hiyo
inayovutia wengi duniani.
Simu 0712
053949 au barua pepe
No comments:
Post a Comment