https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, December 09, 2016

Wapenda gwaride jijini Dar es Salaam ‘kilio’

Na Rahim Kambi, Dar es Salaam
NI kilio kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli kuwatangazia wakazi na wananchi wa jiji la Dar es Salaam kuwa sherehe za Miaka 55 ya Uhuru zinaweza kuwa za mwisho kufanyika jijini hapa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi waliojitokeza katika sherehe za miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli alisema kuwa tamko lake kwa Watanzania linakuja kutokana na kuazimia sherehe kama hizo miaka ijayo zitafanyika mkoani Dodoma ambapo serikali yake itakuwa imehamia huko ikitokea jijini Dar es Salaam.

Dr Magufuli aliyasema hayo katika Maazimisho ya Miaka 55 ya Uhuru zilizofanyika katika Uwanja wa Uhuru na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, ambapo majeshi ya Tanzania yalionyesha uwezo mkubwa katika kuonyesha umahiri wao.

“Naweza kusema kwamba sherehe kama hizi katika jiji la Dar es Salaam zitakuwa za mwisho kwa sababu mwaka ujao zitafanyika Makao Makuu ya nchi yetu, mjini Dodoma, hivyo tukio kama hili litakuwa rasmi kwa ajili ya kuwaaga wana Dar es Salaam,” alisema Rais Magufuli.

Mbali na kuhama kwa sherehe hizo, Rais Magufuli pia alitumia muda huo kuwapongeza Watanzania wote kwa kuazimisha miaka 55 ya Uhuru, akisema nchi imeendelea kupiga hatua kubwa ya kiuchumi, kielimu na kiutamaduni.

Aliwataka Watanzania wote kumuunga mkono yeye na serikali yake pamoja na watumishi wake ili kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa nguvu zote ili kurahisisha maendeleo.


Aidha Rais Magufuli alitumia muda huo kuwaasa watu wanaoendelea kuendekeza vitendo vya rushwa na ufisadi akisema kuwa ataendelea kula nao sahani moja ili kuhakikisha kwamba nchi yake inaondokana na adha hiyo inayochelewesha maendeleo.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...