https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, December 07, 2016

MGODI UNAOTEMBEA: Nina hamu ya kuiona CCM ya Dr Magufuli

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NAAM! Macho na masikio ya wengi katika nchi yetu kwa sasa ni namna gani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaingia kwenye mabadiliko makubwa kutokana na aina ya utendaji wa Mwenyekiti wake, Dr John Pombe Magufuli.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dr John Pombe Magufuli, pichani.

Dr Magufuli ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anajulikana kama kiongozi asiyependa ujinga na mtumbua majipu, aliyerithi mikoba ya Uenyekiti wa CCM Taifa kutoka kwa Mwenyekiti Mstaafu, Dr Jakaya Mrisho Kikwete. 

Dr Kikwete alikuwa mwenyekiti wa CCM Taifa huku akitawaliwa na huruma, tabasamu kiasi cha watendaji wake kutumia mwanya huo kuwa wala rushwa, wachumia tumbo na ‘majipu’ yanayostahili kutumbuliwa bila ganzi. Ndio ni majipu. Tena majipu makubwa kuliko hata yale ya watendaji wa serikali, ukizingatia kuwa kushamiri kwao wengi wao wamezalishwa na kuchochewa na mfumo mbovu wa upatikanaji wa viongozi wa CCM kwa miaka ya hivi karibuni.
Dr Magufuli akiwasalimia wajumbe wa CCM.
Hakuna asiyefahamu majipu hayo. Hata alipokuwa anahutubia wajumbe mjini Dodoma wakati anakabidhiwa nafasi ya uenyekiti wa CCM Taifa, Dr Magufuli alilizungumzia kwa kina, akionyeshwa kukerwa na aina watendaji na mfumo wa chama chake. Mwenyekiti huyo alifahamu kati ya matatizo mengi ya kupata viongozi wasiokuwa wasafi, wala rushwa, wasiokuwa na uchungu na Taifa lao, baadhi yao wanatokea kwenye chama chake.

Naye ni muathirika mkubwa baada ya kupata wakati mgumu katika mchakato wa kuomba wadhamini alipochukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama cheke kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia CCM, huku baadhi ya makada wake wakituhumiwa kumwaga fedha kama njugu ili kuongeza ushawishi kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanachama katika vijiji, kata, wilaya na mikoa mbalimbali ya nchi yetu.

Licha ya ukongwe wake, CCM ilianza kupoteza sifa na imani kwa wananchi wengi wa mijini huku wa vijijini nao wakianza kuangalia uwezekano wa kuongozwa na wapinzani. Wakaiona CCM ni chama cha mafisadi, wala rushwa na watoa rushwa.

Viongozi wakaanza kupatikana kwa ukwasi wa fedha. Nafasi zote za uongozi ndani ya CCM na zile za ubunge na udiwani ziliuzwa kwa fedha nyingi. Walalahoi wachache walipita. Tena kwa kufanya kazi ya ziada ama kulazimika kuwa kwenye mtandao wa wenye nazo. Kuweka mamilioni ya fedha ili kuongeza ushawishi wa kupata madaraka ndani ya CCM kilikuwa mazoea. Na kila mtu alijua hilo. Mgombea anaulizwa, “Mzee unatuachaje”?
Wakati huu tunapoelekea kwenye matazamio ya kuundwa upya kwa chama cha CCM, nashawishika kusema Dr Magufuli ana kazi kubwa ndani ya chama chake. Wengi wanaomzunguuka hawastahili kuachwa waendelee kuwapo ndani ya nafasi zao, haswa makatibu wa wilaya, mikoa na watendaji wengine ndani ya chama hiki.

Wengi wao waligeuka kuwa madalali wa wataka uongozi ndani ya CCM. Kamwe hawaangalii sifa yoyote isipokuwa fedha, urafiki, undugu na ujirani kama karata ya kupata viongozi wao. Hata wale waliokuwa chaguo halisi la wananchi, hawapewi nafasi na walijikuta wakikanyagwa wakati wote. Hawakuwa na haki yoyote ndani ya chama chao. Viongozi wao wa chama ngazi ya wilaya na mikoa walicheza kamari mchana kweupe.

Mtindo huo na mingineyo iliiweka CCM katika wakati mgumu kwenye chaguzi mbalimbali nchini kwetu. Na utafiti usiokuwa rasmi ulionyesha kati ya wagombea wengi walioangushwa katika majimbo au kata, ni wale waliopitishwa kwa hila bila kuwa chaguo halisi la wengi.

Wagombea wa nafasi za ubunge ama udiwani wakabaki kuwa chaguo la kikundi kidogo cha watu, wanapitishwa bila kuangalia mtaji wao kwa wapiga kura mitaani. Hili linakatisha tamaa. Matokeo yake watu wanapiga kura za chuki dhidi ya chama tawala. CCM kinaonekana ni chama cha wachache. Aliyetaka kugombea nafasi yoyote kwanza angeangaliwa fedha zake. Angeulizwa juu ya mtaji wake kifedha alionao.

Na kama hana fedha, jua angeonekana si lolote katika siasa za chama kwa wakati huu. Ni tofauti na CCM ya wazee wetu, akina Julius Kambarage Nyerere na wenzake. Wao waliijenga CCM ya Watanzania wote, wengine wameifanya ya wachache wenye nazo. CCM kilikuwa chama cha walalahoi. Wote walijivunia nacho bila kujali dini zao, ukabila wao na maeneo watokayo.

Inashangaza kuona umeundwa mfumo mbovu wa nafasi za uongozi ndani ya chama hiki kikongwe. Viongozi hawajui wajibu wao. Si Katibu wa wilaya, mwenyekiti wala MNEC anayefahamu wajibu wa kusimamia sheria, taratibu wala maadili ya uongozi. Kazi yao ikabakia kuwa wapambe wa wabunge katika maeneo yao. Hakuna jingine walilojua zaidi ya hilo. Kama walisema juu ya utendaji mbovu wa Mkurugenzi wa Halmashauri, basi mtendaji huyo atakuwa hayupo kwenye mtandao wa mbunge wake.

Mfumo huu ulichelewesha maendeleo. Wakageuka Bendera, wapambe ama makatibu wa wabunge majimboni mwao. Wataalamu kama walimu, afya na wengineo nao wakalazimika kutii matakwa ya wabunge hao, wakielekezwa kufanya hata yale yasiyokuwa na tija katika nafasi zao kwa mujibu wa sheria.
Wasiofanya hivyo wakanyanyasika na wengineo kujikuta wanahamishwa kwingine bila sababu za msingi. Viongozi wa chama wilaya na mikoa hawajui wajibu wao wala ufahamu wa kusimamia watendaji wa serikali kama chama tawala.

Wakajikuta wao ndio wanasimamiwa na wengine. Hakuna hata anayeweza kuinua mdomo wake kumkemea mbunge, Mwenyekiti wa Halmashauri ama Meya. Watawezaje wakati walinunuliwa katika mchakato wa kura za maoni? Uwezo wa kusema wautoe wapi? Ndio CCM ilivyokuwa kabla ya Dr Magufuli kupewa nafasi ya kuwa Mwenyekiti Taifa. Sasa ana kazi ya kuitoa CCM katika mikono ya wajanja na kuileta panapostahili. Kuirudisha CCM kutoka kwa walioiendesha kwa mbinu za kimtandao.

Vipi hii ya Magufuli? Ataiweza? Atawaweza wajanja hawa? Katika kuangalia kama ataweza au atashindwa ni budi kwa wanachama wote kuhakikisha kwamba mwenyekiti wao anaweza. Na kwanini ashindwe? Kazi anayoifanya kurudisha nidhamu serikalini ni ishara kuwa uwezo huo anao. Aungwe mkono. Kila mwanachama wa CCM atimize wajibu wake, awe mlinzi kwa mwenzake.

Mwana CCM asikubali kununuliwa wala asinunue mwenzake. Atakayeonekana anahonga ili achaguliwe katu hastahili kuachwa badala yake amulikwe na awajibishwe. Kitendo cha kununua uongozi kinachelewesha maendeleo. Watu hawafanyi kazi kwa moyo badala yake wanawaza kurudisha fedha walizotumia kwenye chaguzi zao.

Watoa rushwa waone sasa mwisho wao umefika. Mwisho wa kuondosha makapi na kuleta watu wanaokubalika kwa sifa zao umewadia. Wana CCM wasioneane haya. Waambiane ukweli na ikiwezekana watumbuane.
Hii itawezekana kama watakubali kubadilika. Isiwe CCM ya wajanja tena ila iwe ya walalahoi na Watanzania kwa ujumla. Mapambano haya yaanzie kwenye uchaguzi wa nafasi za ndani kuanzia shina, tawi, kata, wilaya na Taifa mwaka 2017.

Asitokee wa kupitishwa kwa ghiliba. Ili jambo hili lifanikiwe, Dr Magufuli na safu yake ya juu ya CCM anapaswa kuwahamisha kama sio kuwafukuza kazi baadhi ya watendaji wa chama ngazi ya wilaya na mikoa ili aisuke upya kwa kuwa wao ndio tatizo kubwa. Hawa wakiachwa kwenye nafasi zao haswa Makatibu wa Wilaya na Mikoa watamuangusha Mwenyekiti. Hii ni kwa sababu wengi hawajui wajibu wao. Wanalalamikiwa kila kona ya nchi yetu.

Ni wachache waliofanya kazi zao kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa. Ikiwa Dr Magufuli ataanza kuisuka CCM huku akiwabakiza kwenye nafasi zao niliowataja hapo juu ni wazi atachelewa kutimiza malengo ya kuisuka upya. Afanye uchunguzi wa kina. Watendaji mizigo watimuliwe. Wateuliwe wengine watakaokubali kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa na kutoa haki kwa watu wote.

Lazima lifanywe jambo nyeti na lenye tija kwa mustakabali wan chi yetu kama njia ya kukifanya kiendelee kuheshimika kwa miaka 50 ijayo.
Sisemi kama wenyeviti waliopita ukiwamo uongozi wa Dr Jakaya Mrisho Kikwete haukufaa. Kikwete alifanya mengi ya msingi, hata hivyo mkazo na mabadiliko zaidi yanahitajika.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulikuwa mgumu. Isingekuwa juhudi za ziada, huenda mambo yangekuwa mabaya kwa chama hiki. Pia tulishuhudia jinsi Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Abdulrahaman Kinana na timu yake walivyohangaika kufanya mikutano katika Kata, Wilaya na Mikoa mbalimbali kwa ajili ya kujua kero na kusimamia watendaji wa juu wa serikali, hususan mawaziri.

Ziara za Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi ambaye ni Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni wa serikali ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Nape Nnauye zilizaa matunda. Huu si wakati wa kuchekea ujinga unaokihujumu chama. Utakiangamiza. Kila mtu atimize wajibu wake. Viongozi na watendaji wa chama waifanye kazi yao wakati wote na si kusubiri Uchaguzi Mkuu kama njia za kusaka pesa kutoka kwa wagombea.

Watendaji, Makatibu na Wenyeviti wacheza kamari wakati wa kura za maoni hawahitajiki tena. Waondoshwe. Kwa mfano, wapo Makatibu wa CCM na wana mtandao wenzao wanaomba rushwa kutoka kwa wagombea ili watoe ushindi ama nafasi nzuri ya kura. Nazungumzia nafasi ya kwanza hadi ya tano, ambayo kiuhalisia makada watatu wanaofikishwa Kamati Kuu mmoja wapo anaweza kuteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM.

Hayo na mengine mengi yaliwafanya makada wafanye kila wawezalo kuhonga wasimamizi wa uchaguzi wa chama katika majimbo, kila mtu akitaka nafasi za juu. Ni jambo la kusikitisha. Na hapo ndipo linapotokea swali la akiba ya fedha kutoka kwa mgombea husika. Mtoto wa mkulima, mlalahoi hata akubalike vipi jimboni kwao ni ngumu kupenya.

Hivyo kuibuka kwa Dr Magufuli na kuapa kuisuka upya CCM, aghalabu matumaini mapya yametokea. Matumaini ambayo wapo wasiyotaka, wakiamini ule ufalme wao unatoweka. Hata hivyo ifikie wakati tuseme imetosha. Chama kisukwe upya na wale wasiostahili washughulikiwe haraka kama walivyoshughulikiwa watendaji wa serikali.

Endapo kwenye CCM hakutakuwa na majipu, hata dhamira ya kuwa na watendaji wenye kujali maslahi ya Watanzania kwenye serikali itafanikiwa kwa vitendo. Hakutakuwa na njia za panya tena. Viongozi wababaishaji, wala rushwa, mafisadi na wasaka tonge watatoweka na kuifanya nchi iwe kwenye mstari mzuri wa kimaendeleo.

Si tu uongozi ndani ya CCM ulinunuliwa na wataka madaraka na kuuzwa na makatibu wa wilaya na mikoa, bali pia watu hao walishindwa kusimamia rasilimali za chama katika maeneo mengi hapa nchini. Kila kona ni ujanja ujanja tu. Mikataba isiyokuwa rafiki na isiyokuwa na tija kwa chama iliingiwa kila siku.

Wakaifanya CCM ya maslahi yao. Wakazichapa kadi feki za CCM ili mabwana wakubwa wao washinde. Kama hiyo haitoshi, wakapeleka mihutasari na ripoti feki ili kuaminisha ushindi huo. Mwisho wa uchafu huo ni kukataa kwa Watanzania juu ya wanaopitishwa katika kata na majimbo husika. Na ndio maana idadi ya viti vya udiwani na ubunge kwa upande wa upinzani inaongezeka maradufu nchini.

Nani wa kusema? Ni dhahiri wamedhamilia kukiangamiza chama hiki kikongwe hapa nchini. Hivyo anapotokea Dr Magufuli na kuamua kwa dhati kurudisha misingi na dira ya chama hiki, kwanini asiungwe mkono?
Ndio maana nasema nina hamu ya kuiona CCM ya Dr Magufuli. Mtu pekee atakayerudisha heshima ya CCM mitaani. Mabadiliko makubwa atakayofanya yataleta imani kwa Watanzania wote, mijini na vijijini.

Kwa bahati nzuri hakuna wakati mzuri wa kuisuka upya CCM kama mwaka ujao wa 2017, ambao chama kitafanya chaguzi zake katika ngazi zote, jumuiya zote. Hata hivyo narudia tena, mabadiliko hayo na dhamira ya kusukwa upya kwa chama hiki yaanzie katika kuwabadilisha ama kuwafukuza kazi watendaji wabovu, waliofanya kazi kwa matakwa yao binafsi haswa makatibu wa wilaya, makatibu wa mikoa na makatibu wa jumuiya za chama ili kuhakikisha kwamba CCM inazaliwa upya na inakuwa katika misingi ya kuongoza nchi kama chama tawala. Chama kikongwe chenye historia murua kwa Taifa letu.

Naamini Dr Magufuli na safu yake uwezo huo wanao. Kilichobaki ni kuombewa na kupewa ushirikiano kwa wanachama wote bila kuangalia vyeo vyao, majina yao, fedha zao na mengineyo.

+255 712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...