By Godfrey Dilunga, Dar es Salaam
Asante Bwana Mdogo wa Mwl. Nyerere,
Komandoo Fidel Alejandro Castro Ruz
Komandoo Fidel Alejandro Castro Ruz
PUMZIKA Komandoo Fidel Alejandro Castro Ruz, Waziri Mkuu wa kwanza wa Cuba ambaye pia ni Rais wa Kwanza wa Taifa hilo. Komandoo uliyenusurika kuuawa mara 638 na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA). Na moja ya jaribio lililoshindwa ni lile la kukuua kwa kutumia unga wa sumu uliowekwa kwenye sigara ulizokuwa unapenda kuvuta. Majaribio makubwa manane ya kukuua yanatajwa kufanyika dhidi yako Fidel kati ya mwaka 1960 na 1965.
Fabian Escalante, jasusi mstaafu wa Cuba aliyepata kuwa mlinzi wako ewe Fidel anaamini CIA walifanya majaribio hayo 638 ya kukuua, japokuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa CIA, Richard Helms, Machi 5, mwaka 1972, alikanusha CIA kuhusika iwe moja kwa moja au kupitia mawakala wa shirika hilo lenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi zake kwa siri mno.
Majaribio yote ya mauaji dhidi yako Fidel yalishindika lakini, sasa, kwa mapenzi ya Mungu, Fidel umeondoka duniani. Pengine unakwenda kukutana na kaka yako, kwa umri wa kuzaliwa, Julius Nyerere. Naam, Nyerere ni mkubwa kwako Fidel kwa miaka minne hivi – hili unalijua vyema na nchi zenu (CUBA na TANZANIA) zilikuwa marafiki wakubwa.
Fidel kawasalimie magwiji wenzako waanzalishi wa Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande wowote (Non-Aligned Movement - NAM), umoja mliouasisi mkiwa viongozi wa nchi tano kule Belgrade mwaka 1961, katikati ya kilele cha kelele za vita baridi chini ya Urusi kwa upande mmoja na Marekani kwa upande mwingine.
Heshima nyingi kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa India, Jawaharlal Nehru; Rais wa kwanza wa Indonesia, Sukarno; Rais wa Pili wa Misri, Gamal Abdel Nasser; Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah na aliyekuwa Rais wa Yugoslavia, Josip Broz Tito. Pumzika, Fidel, bwana mdogo wa Mwalimu Nyerere, shujaa katika safu ya mstari wa mbele vitani, kinara katika kupinga ubepari wa mabepari - mwanamapinduzi wa kweli, salaamu pia kwa Hugo Chavez.
Nani asiyejua kwamba Cuba ndio nchi mahiri duniani katika matibabu? Nani asiyejua Cuba ndio kisiwa cha madaktari bingwa na mahiri duniani? Diego Armando Maradona – mwanasoka aliyevuma mno duniani, anajua hili, na alifika Cuba kwa matibabu wakati fulani, licha ya kuwa na fedha nyingi za kumwezesha kupata matibabu nchi za Ulaya.
Fidel, bwana mdogo wa Mwalimu Nyerere, nimepata kusikia sauti yako ikitamka kile kilichoitwa Azimio la Havana la mwaka 1979. Katika azimio hilo uliweka bayana mantiki ya kuanzishwa NAM kwamba ni kupigania na kulinda hadhi ya uhuru wa mataifa wanachama (national independence & sovereignty) dhidi ya ukandamizaji wa aina yoyote. Buriani Komandoo Kijeshi na Komandoo wa dunia ya wanyonge
No comments:
Post a Comment