https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, June 18, 2015

Stephen Wassira asema hana majina ya washukiwa wa ufisadi Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Rukwa
MGOMBEA anayeomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Steven Wasira, amesema hana majina ya washukiwa wa ufisadi, ingawa uovu huo umo ndani ya vyama vya siasa ikiwamo CCM.
Stephen Wassira, akizungumza katika mkutano wa kuomba kudhaminiwa kwa ajili ya kupitishwa na CCM kuwania urais, mwezi Oktoba mwaka huu.

Wasira anayeongozwa na kauli mbiu ya Uadilifu na Umoja wa Watanzania; Safari ya Uhakika, alisema hayo wakati akizungumza na wana-CCM waliomdhamini katika mikoa ya Rukwa na Katavi jana.

Alisema CCM na serikali yake ni taasisi zilizo na misingi ya uadilifu, ingawa ndani yake kuna uwezekano wa kuwapo watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu huo.
Alisema ufisadi na rushwa na miongoni mwa matatizo makubwa yanayoiathiri jamii na kwamba taifa linamhitaji kiongozi asiyekuwa na kashfa inayomfanya atiliwe shaka katika kukabiliana na kadhia hiyo.

“Hapa sina majina ya mafisadi lakini ninaamini kwamba si ndani ya CCM pekee, bali hata katika vyama vingine vya siasa, rushwa na ufisadi ni miongoni ma matatizo makubwa yanayovikabili,” alisema.

Wasira alisema kutokana na hali hiyo, vita dhidi ya rushwa na ufisadi inapaswa kuwa katika misingi ya hoja na uthubutu wa kuidhibiti badala ya kumlenga mtu binafsi.


Alisema Tanzania ina taasisi imara ambazo zikitumika ipasavyo zitachochea kuwatambua washukiwa wa ufisadi,  vitendo vinavyoashiria uhalifu huo na kuchukua hatua kwa ukali na haraka.

Wasira alisema ikiwa CCM itamteua kuwania na hatimaye kuwania Urais, imani yake ni katika kutoa uhuru na mamlaka zaidi kwa vyombo husika vikiwamo vya sheria, kutekeleza majukumu bila kuoneana aibu.

Alisema, “ninapozungumzia ufisadi sizungumzii mtu au watu, tunauzungumza ufisadi kama hoja, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba hata ndani ya CCM kuna viashiria vya ufisadi, lakini haimaanishi kwamba CCM ni chama cha kifisadi.”
Aliongeza, “hata kwa upinzani kuna ufisadi pia, hivyo ufisadi ni tatizo kubwa katika jamii yetu, kama nitapata fursa ya kuliongoza Taifa letu nitahakikisha tunaukabili kwa nguvu zote ili kurejesha heshima na hadhi ya nchi yetu,” alisema.

Alisisitiza umuhimu wa kupiga hatua katika kilimo na viwanda ikiwa ni moja ya njia kuu za kukuza uchumi na kuboresha maisha na ustawi wa wananchi.

Kwa mujibu wa Wasira, kilimo pekee ndicho kinaweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana kuliko sekta nyingine pamoja na kuliingizia Taifa pato kubwa zikiwamo fedha za kigeni.

Wasira alizungumzia ajira kwa vijana na kusema hivi sasa kuna kasi ya vijana wengi kukimbia kutoka vijijini kutokana na umasikini unaowakabili, na kwenda kukutana na umasikini mwingine mijini.

Alisema uboreshaji wa kilimo, uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya kuongeza thamani za mazao kutatoa hamasa kwa vijana kushiriki kilimo na kutengeneza ajira.

Leo Wasira anatarajiwa kuwasili mkoani Kigoma kutafuta wadhamini, ukiwa ni mkoa wa 30 tangu aanze safari ya kutafuta wadhamini Juni 3, mwaka huu ambapo alianzia mkoani Dodoma.

Vikao vya uteuzi vinatarajiwa kuanza mjini Dodoma Julai 5, mwaka huu, ambapo mgombea urais kwa tiketi anatarajiwa kupatikana Julai 11, na Uchaguzi Mkuu umepangwa kufanyika mwezi Oktoba.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...