Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WENYEWE
wanaziita Kulwa na Dotto. Eti Yanga ni Kulwa na Simba ni Dotto. Kama
majina haya hayaendani nao, basi yanakaribia kabisa na tafsiri ya majina
yao haya.
Wanafanana mizengwe na ubabaishaji. Hata migogoro pia
hurithishana, ukitoka Simba, utahamia Yanga. Klabu mbili hizi ambazo ni
kongwe, hazijawahi kukaa miaka mitatu mfululizo bila migogoro. Na kwa
miaka ya karibuni, wamezidi.
Mbali na migogoro hiyo, klabu hizi
zimekuwa na kawaida ya kubadilisha makocha kama nguo za ndani. Labda
wanatafuta kocha mwenye mafanikio zaidi ya Sir Alex Ferguson, aliyewahi
kuwa kocha wa timu ya Manchester United ya nchini Uingereza.
Kama huo
ndio mtazamo wao, basi wanajidanganya. Wanajipotezea muda, maana ndani
ya timu hizi kongwe hakuna kocha mzuri. Hata akiwa mzuri, ataharibiwa
na mizengwe yao.
Hadi leo hawaheshimu makocha wao. Mwenyekiti au
kiongozi wa klabu anaingilia upangaji wa timu bila kuona athari
zinazoweza kujitokeza kwenye klabu yao.
Na ikitokea timu inafungwa,
wanajaribu kuwasumbua wataalamu hao ambao wengi wao wamekuwa wakiishi
kwa kubangaiza wasiojua kesho yao itakuwaje.
Hakika siwezi kuvumilia.
Ni wazi klabu hizi kongwe zinazoitwa dira ya soka la Tanzania kwa ngazi
ya klabu kuwa makini katika utendaji kazi wao na namna ya kusaka
mafanikio.
Huu ndio ukweli wa mambo. Kinyume cha hapo klabu hizi
zitaendelea kusua sua kwa sababu hawatakuja kuheshimu utaalamu wa
makocha wao, ambao ni watu wenye kupaswa kuheshimiwa na kusikilizwa
maoni yao kwa maendeleo ya timu zao.
Tanzania imeshindwa kupiga hatua
katika nyanja ya mpira wa miguu kwa sababu mbinu zinazotumika ni duni,
huku zikichagizwa na ubabaishaji mkubwa wa viongozi wa timu zetu,
hususan Simba na Yanga, zinazoitwa Kulwa na Dotto.
Tunataka ushindi.
Tunataka mafanikio. Mafanikio yanayoweza kuja kwa kujipanga kuanzia
utawala na ufundi, kwa kupitia makocha wetu wanaopaswa kulipwa vizuri na
kusikilizwa pia namna wanavyotaka kuziendesha timu zetu.
Tunaonane wiki ijayo.
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949
No comments:
Post a Comment