* Atangaza nia kwa kutoa takwimu za umasikini na utajiri
*Asema viwanda, gesi, umeme utaipaisha Tanzania
Na Mwandishi Wetu, Musoma
WAZIRI
wa zamani wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo, ametangaza nia rasmi
ya kuwaomba Wana CCM kumteua kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mwezi Oktoba, huku akisema ni yeye pekee mwenye uwezo wa
kuikwamua nchi katika hali mbaya ya umasikini na ukosefu wa wataalamu,
hali inayoifanya nchi ishindwe kupiga hatua.
Profesa Sospeter Muhongo, pichani.
Pamoja na mambo
mengine, Muhongo alitumia muda mwingi kutoa takwimu hali ya umasikini na
utajiri kwa wananchi wa Tanzania, bila kusahau baadhi ya nchi ambazo
zimeweza kupiga hatua kubwa kwa kujikita kwenye kuzalisha wataalamu na
watafiti, akiwamo yeye, ambaye si tu ni Profesa, bali pia amebobea
kwenye nishati kwa miaka mingi.
Akizungumza kwa kujiamini mbele
ya wanachama wa CCM na Watanzania katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria,
Musoma Mjini jana, Profesa Muhongo alisema kwamba anayo tiba ya umasikini wa
Watanzania kwa kuhakikisha kwamba anatumia utaalamu wake kwa kusimamia
mambo ya gesi, mafuta, umeme, bila kusahau elimu kwa ajili ya kuwakwamua
wananchi wake.
“Nchi ina upungufu mkubwa wa takwimu hali
inayowafanya viongozi washindwe kujua namna gani wanaweza kuondoa
umasikini na kero zinazowakumba wananchi wake, hivyo hata wale wanaosema
wanataka uongozi, hawajui wangapi wenye uhitaji.
“Ukiacha
takwimu ambayo kwa Dunia ya sasa ni lazima, nchi yetu lazima ijiamini,
kuongeza ushindani, kuongeza upendo, bila kusahau rushwa ambayo kwa
uhakika inapaswa kupigwa vita kwa vitendo ili nchi yetu isonge mbele,”
alisema Muhongo.
Kuhusu uchumi, Profesa Muhongo alisema kwamba ni
aibu Tanzania kupitwa kiuchumi na Mataifa waliyokuwa nayo sawa,
akitolea mfano wan chi za Brazil, China, India na Kenya ambao wao
wamewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye elimu na utafiti.
Alisema
nchi ikiwa na watafiti, wananchi wao hawataishi kwa mashaka, huku
akisema endapo atapitishwa kuwania nafasi hiyo na kuwa rais wa Tanzania,
atahakikisha kwamba anakuza uchumi wan chi kutoka asilimia 7.5 hadi
asilimia 10 na 15 kwa kipindi cha miaka mitano hadi 10 ya urais wake.
“Nimeweza
kufanya kazi ya gesi na mafuta kwa miaka kadhaa kwenye nchi mbalimbali,
hivyo hakika kama chaguo ni wataalamu, basi mimi nastahili kwa sababu
sioni mwingine mwenye uwezo wa kutangaza kuondoa kero za Watanzania na
jinsi atakavyoziondoa.
“Ndio unaweza kusema utaondoa umasikini
kwa wananchi au kuongeza mishahara, lakini ili hilo liweze kufanikiwa
kwa vitendo, ni lazima pia katika kipindi cha uongozi wako uweze kukuza
uchumi wako kwa kiasi kikubwa, bila hivyo hakuna kitu,” alisema Muhongo.
Aidha
Profesa Muhongo alisema kwamba Duniani kote nchi zimepiga hatua kwa
kuwekeza kwenye wataalamu na viwanda, hivyo Tanzania inapaswa kuangalia
namna ya kuwekeza kwenye sekta hizo, bila kusahau sekta ya elimu yenye
umuhimu mkubwa.
Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo alisema
kwamba akiwa Waziri wa Nishati na Madini, ndio mtu ambaye alifanikiwa
kwa vitendo kutekeleza ilani ya CCM kwa kuhakikisha kwamba vijiji vingi
vinapata umeme kwa kuongeza bajeti na kusimamia kwa vitendo wakala wa
umeme vijijini (REA).
Alisema kusudio la kuhakikisha kwamba
wananchi wake wanaendelea kupata umeme kwa bei nafuu ni kati ya mambo
anayoona yanafaa kuongezewa chapuo na usimamizi wa aina yake, hivyo
mwenye uwezo wa kulitatua hilo ni yeye.
No comments:
Post a Comment