Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
INAHITAJI
akili za kiuwendawazimu kukubali mwenendo mbovu wa soka la Tanzania,
linaloendeshwa kwa mizengwe mizengwe. Leo mtu anaweza kuharibu mkataba
wa kisheria kwa makusudi na bado asiburuzwe katika vyombo vya sheria.
Ndio,
maana tumeshuhudia Shirikisho la Soka nchini (TFF) kulimaliza sakata la
mchezaji wa Simba, Ramadhan Singano ‘Messi’, kitu ambacho wengi
walikitarajia. Hii ni aibu kubwa, maana TFF waliamua kulifunika funika.
Mwenyewe
Singano anasema anamuachia Mungu. Pengine aliyasema haya kwa sababu
alijua kwamba hawezi kuipata haki aliyokusudia. Kama hivi ndivyo,
nakumbuka msemo mmoja wa Kiswahili usemao ‘Fisi akiwa hakimu, mbuzi
sheria hana’. Ndio, TFF wao wanamtaka Singano na klabu yake warekebishe
mapungufu kwenye mkataba wao.
Kurekebishwa kunaashiria kuwa kuna
tatizo kubwa. Lipi hilo? Kwanini tatizo hilo lisiwekwe hadharani ili
kila mmoja alijuwe? Hii inaonyesha kwamba kuna dalili za kulindana. Ni
wazi kati ya Simba au Messi, kuna mmoja anatatizo.
Ila kulifumba
fumba si njia ya kusuluhisha mzozo huo. Hata kama leo hili likiisha,
vizazi vinavyo vitaendelea kuwa na kasumba hii. Hapa ndipo nisipoweza
kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kuona soka letu linaendelea kuendeshwa
kienyeji na kiubabaishaji.
Hatuwezi kuendelea kamwe. Tunahitaji
kutunga sheria na kanuni na kuziishi. Hii kuziba ziba na kulindana
kutaliweka soka letu kwenye mashaka makubwa. TFF inapoamuru kurekebisha
mapungufu kwenye mkataba wa Singano, kunamaanisha kubariki uozo wowote
uliokuwapo kwenye pande hizo.
Kwanini tusizidi kubaki kama
tulivyo? Bado tutalalamika kwamba soka letu haliendelei? Hatuwezi kupiga
hatua kamwe. Singano analalamika mkataba wake umechezewa. Badala ya
kuangalia umechezewaje, tunakuwa bubu kwa sababu tunazojua wenyewe.
Kesho
mkataba huo utachezewa tena na tena. Kama Singano amedanganya,
tunapaswa kuchunguza kwanini amedanganya ili apewe adhabu. Haya sasa,
siku moja baada ya uamuzi huo kutoka, Simba hao hao wanaibuka tena na
kusema hawawezi kufanya lolote likiwamo kuangalia marekebisho hayo kwa
sababu wana mkataba halali na Singano.
Huu ni ujinga wa karne.
Nathubutu kusema kuna dalili za wazi za kuharibu kipaji cha kijana huyu
ambaye Taifa linamtegemea kutokana na kipaji chake. Kama TFF ingekuwa
makini, siku ile ile ya kikao chao cha kuangalia suala hilo, wangebaini
tatizo na kulitatua.
Ipi kazi ya TFF? Au ndio fisi akiwa hakimu,
mbuzi hana sheria? Hatuwezi kuendelea kwa ubabaishaji huu katika nyanya
ya mpira wa miguu kwenye nchi yetu na siwezi kuvumilia.
Tuonane wiki ijayo.
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949
No comments:
Post a Comment