https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, June 12, 2017

Kompyuta nane za Bayport zatua mkoani Tanga

Na Mwandishi Wetu, Tanga
TAASISI ya Kifedha ya Bayport Financial Services, imekabidhi kompyuta nane katika wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani zote za mkoani Tanga, ikiwa ni mwendelezo wa msaada wa kompyuta 205 zenye thamani ya Sh Milioni 500 kwa ajili ya ofisi za serikali nchini Tanzania, huku mpango huo ukiasisiwa mwishoni mwa mwaka jana.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Mwakufwe aliyeshika sehemu ya kompyuta akiwa na Mratibu wa Masoko wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa wa pili kutoka kulia pamoja na Meneja wa Bayport Handeni, Candy Masunzu. Kushoto ni Afisa Utumishi wa Wilaya ya Handeni, Noel Abel katika tukio la kupewa msaada wa kompyuta mbili kutoka Bayport wiki iliyopita wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Utaratibu wa makabidhiano ya kompyuta hizo ulianza Handeni Jumatatu ya Juni 5, huku wilaya ya Korogwe wakipokea Juni 6, Muheza Juni 7 kabla yakumalizia Pangani Juni 8, ambapo kila wilaya ilipokea kompyuta mbili kwa ajili ya kupunguza changamoto ya vifaa vya kiutendaji katika ofisi za umma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Korogwe, George Nyalonga mwenye koti jeusi naye akipokea kompyuta mbili kutoka Bayport wiki iliyopita.

Akizungumza mjini Tanga katika makabidhiano hayo, Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa, alisema ni furaha yao kuona mpango wao wa kutoa kompyuta kwa ofisi za umma unaendelea vizuri kwa Mkoa wa Tanga kufikiwa na msaada huo.
Mratibu wa Masoko wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa wa tatu kutoka kushoto waliosimama akimkabidhi sehemu ya kompyuta mbili Afisa Utumishi wa Wilaya ya Muheza, Godhope Ringo, akiwa na baadhi ya watumishi wa wilaya ya Muheza katika tukio hilo lililofanyika wiki iliyopita wilayani humo.

Alisema taasisi yao itaendelea kuwa karibu na serikali kwa kushiriki kutatua changamoto zilizokuwa ndani ya uwezo wao pamoja na kushirikiana na Watanzania wote kwa kupitia sekta ya mikopo ili kuhakikisha kwamba nchi yao inasonga mbele kimaendeleo.

“Tupo katika serikali ya Hapa Kazi Tu kama alivyoasisi Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli, hivyo kwa kuliona hilo taasisi ikaona ipo haja ya kusambaza kompyuta kwa ofisi za serikali ambazo hata hivyo utaratibu wa kutoa msaada huu ulipangwa na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, chini ya Waziri wake, Mh Angelllah Kairuki mwaka jana,” Alisema Mercy.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Korogwe, George Nyalonga, aliwapongeza Bayport kwa kuamua kujitoa katika jamii sambamba na serikali yao hususan baada ya kusambaza kompyuta huku wilaya yake ikipangwa kupokea kompyuta mbili.

“Hakika nawashukuru sana Bayport kwa kutusaidia kompyuta mbili kwenye Halmashauri yetu, nikiamini kuwa zitatusaidia kwa kiasi kikubwa mno na kufanikisha utendaji kazi bora kwa watumishi wa umma na kuwezesha ndoto za kuwaletea maendeleo wana Korogwe,” Alisema Nyalonga.

Wilaya ya Muheza kompyuta hizo zilipokewa na Afisa Utumishi wake Godhope Ringo, ambapo hakusita kuonyesha furaha ya vitendea kazi hivyo akisema kukua kwa sayansi na teknolojia ni sehemu ya kuhitajika kwa kiasi kikubwa matumizi bora ya kompyuta kwenye ofisi zote za umma.

“Kwa niaba ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Muheza, hakika tumepokea kwa shauku kubwa mashine hizi mbili na tunawaomba muendelee kushirikiana na sisi kwa namna moja ama nyingine hususan za kuhakikisha kwamba wilaya yetu na Tanzania kwa ujumla inasonga mbele,” Alisema Ringo, mbele ya wakuu wa Idara wa Halmashauri hiyo.


Kwa kusambaza kompyuta hizo nane katika wilaya nne za Mkoa wa Tanga, Bayport inaendelea kutimiza ndoto zake kuhakikisha kwamba wanashirikiana na serikali kuwapatia maendeleo Watanzania kwa sekta mbalimbali, ikiwamo ya mikopo ya fedha inayotoa kwa miaka 10 tangu kuanzishwa kwake nchini Tanzania mwaka 2006 na kuwawezesha watumishi wa umma kwa kiasi kikubwa ambao ndio wakopaji wake wakuu.


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...