Na Mathias Canal, Dodoma
UFUNGUZI wa siku ya wakulima Nane nane Kanda ya kati Dodoma mwaka 2016
umefanyika leo katika Uwanja wa Maonyesho ya kilimo Nzuguni Mkoani Dodoma huku kauli
mbiu ya mwaka huu ikiwa ni "Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ni nguzo ya
maendeleo, Kijana shiriki kikamilifu (Hapa Kazi Tu).
Mkuu
wa Mkoa wa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe (Kushoto) akisalimiana na Mkuu
wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya
Nane Nane katika uwanja wa maonyesho ya kilimo Nzuguni Mkoani Dodoma.
Baadhi
ya Wakuu wa Wilaya za Dodoma na Singida wakiongozwa na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa
wa Singida Mathew Mtigumwe wakikagua eneo la maonyesho ya bwawa la samaki lenye
samaki aina ya perege, kambare na kamongo liloandaliwa na Uongozi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Maonyesho haya yanahusisha shughuli za wakulima, wafugaji wa mifugo,
wafugaji wa nyuki, wavuvi, wanamazingira, wasindikaji wa bidhaa za mazao ya
kilimo na mifugo, wizara taasisi/makampuni ya umma, makampuni binafsi, mabenki,
taasisi za umma na za binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Akizungumza katika ufunguzi huo Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa
Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe
alisema kuwa sekta ya kilimo bado ni mhimili wa uchumi wa Tanzania kwa sababu
inaajiri zaidi ya asilimia takribani 80 ya watanzania na kwa kuzingatia malengo
ya maendeleo ya Taifa ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda
hivyo kilimo kikiboreshwa viwanda vitapata malighafi ya uhakika na kuimarisha
masoko kwa wakulima hivyo kuwepo na ajira ya kuaminika kwa vijana na watanzania
kwa ujumla.
RC Mtigumwe alisema kuwa wastani
wa ukuaji wa sekta ya kilimo unabadilika mwaka hadi mwaka kutokana na kilimo
kwa kiwango kikubwa kutegemea mvua ambazo zimekuwa zikinyesha kwa viwango na
mtawanyiko unaotofautiana kila mwaka ambapo kwa mwaka 2010 sekta ya kilimo
ilikuwa kwa asilimia 4 ikilinganishwa na asilimia 6.5 ya mwaka 2015.
"Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kanda ya kati ina
rasilimali ya maji yakutosha ya chini ya ardhi hivyo kuendelea kuitamka kama
kanda kame hakuna usahihi wa jambo hilo ipo haja ya kuona kuwa rasilimali hiyo
inapatikana kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji hivyo kupunguza
kilimo cha kutegemea mvua," Alisema
Mtigumwe.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida kabla ya kuwahutubia wananchi waliojitokeza
katika ufunguzi huo alitembelea baadhi ya mabanda ya maonesho na kuona shughuli
mbalimbali za uzalishaji wa mazao, ufugaji, uvuvi, usindikaji na wauzaji wa
zana na pembejeo za kilimo ambapo amejionea matokeo ya juhudi mbalimbali
zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kuinua ukuaji wa sekta ya
kilimo ambapo juhudi hizo zinajumuisha uzalishaji wa mbegu mbalimbali zinazostahimili
hali ya hewa ya maeneo ya kanda ya kati.
"Natoa wito maalumu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wajasiriamali na
wadau wa sekta zingine kuhakikisha kuwa bidhaa zenu zinafikia ubora wa hali ya
juu kuanzia shambani zinakozalishwa, zinakosindikwa na kuhifadhiwa na hadi
kumfikia mlaji, ikumbukwe kwamba kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya
juu kutawezesha bidhaa zetu kuhimili ushindani wa hapa nchini na nje ya nchi na
kuuzwa kwa bei nzuri," Alisema
Mtigumwe.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya waandaaji wa maonyesho ya Kilimo,
Mifugo na sherehe za nane nane, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa
hotuba ya Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida itakuwa ya mazingatio
ili kurahisisha na kuendeleza kasi ya serikali ya awamu ya Tano kwa vitendo
hususani katika kuakisi na kuwasaidia wananchi ambao ni wakulima na wafugaji
kupata mbinu bora za kufuga na kulima kisasa ili kupata mazao kwa wingi.
Hata hivyo DC Mtaturu alisema kuwa ana imani thabiti
kuwa baada ya kumalizika kwa maonyesho hayo wakulima, wafugaji na wananchi
washiriki watakuwa wamejifunza vyema mbinu bora za kukabiliana na changamoto za
kilimo na ufugaji hivyo kujikita zaidi katika mbinu bora na za kisasa za kilimo
na ufugaji pia.
DC Mtaturu alisema kuwa shughuli
kuu ya wakazi wa kanda ya kati inayoundwa na mikoa miwili ya Singida na Dodoma yenye
jumla ya Wilaya kumi na mbili na Halmashauri 15 shughuli zao kuu ni kilimo na
ufugaji.
No comments:
Post a Comment