https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, March 29, 2016

Milioni 37 zatengwa kukarabati barabara ya Kata ya Panzuo/Mkuranga

Na  Mwandishi Wetu, Mkuranga
JUMLA ya Sh Milioni 37 zimetangwa kwa ajili ya kukarabati barabara ya Mbogo na Mbezi Muungwana, inayopita katika vijiji kadhaa vya Kata ya Panzuo, wilaya Mkuranga, mkoani Pwani kwa ajili ya kupunguza adha za ubovu wa barabara wanazokutana nazo wananchi wa maeneo hayo hali inayopelekea wakati mwingine akina mama kujifungulia njiani.
Mwendesha bodaboda Ramadhan Rajab akijaribu kupita katika barabara mbovu inayotokea Kimanzichana kuelekea vijiji vya Mnyonzole na Kibesa, Kata ya Panzuo, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.

Mapema mwezi uliopita baadhi ya wananchi wakiwamo akina mama walizungumza kwa uchungu juu ya ukosefu wa barabara katika maeneo hayo, jambo linalowanyima raha na ukosefu wa mbinu za kujikwamua kiuchumi kwa kukosekana barabara inayopitika kwa wakati.

Akizungumza juu ya ukosefu wa barabara na mipango yao, diwani wa Kata ya Panzuo, wilaya Mkuranga, mkoani Pwani, Juma Magaila, alisema kwamba kiasi hicho cha pesa kitaanzia kwanza kuweka kifusi katika maeneo mbalimbali ili wananchi wae ndelee na majukumu yao kwa kuhakikisha kwamba suala hilo la barabara mbovu linashughulikiwa.

Alisema ni kweli wananchi katika maeneo hayo wamekuwa wakiishi kwa mashaka hususan mvua zinapoanza kunyesha, ila tayari fedha zimetangwa kwa ajili ya kuanza ukarabati wa barabara hiyo inayotumiwa na wananchi wengi wilayani Mkuranga.
“Tunaendeelea na mikakati ya kuikwamua Kata yetu hususan katika changamoto kubwa za ubovu wa barabara wanazokutana nazo wananchi wangu wa Panzuo ambao wanashindwa kukuza uchumi wao kwasababu barabara haipitiki kirahisi wakati wote.

“Naamini kwa kutengwa kiasi cha Sh Milioni 37 kutachangia kwa kiasi kikubwa kuiweka barabara yetu katika kiwango cha kupitika huku tukielekea katika safari ya kuona tunafikia hatua ya kuiwekea changarawe na mengineyo,” Alisema.

Awali wananchi wa vijiji vya Kibesa wakiongozwa na mwenyekiti wao Khamis Ningwe walitumia muda mwingi kuilalamikia barabara hiyo sanjari na kuiomba serikali ya Halmashauri ya wilaya Mkuranga iliangalie suala hilo kwa jicho pevu.


Endapo barabara hiyo itakarabatiwa japo kwa kiwango cha kifusi, si tu akina mama wajawazito hawatajifungulia njiani kunaponyesha mvua, bali wananchi wanaweza kuingiza kipato kwa kuuza bidhaa zao mbalimbali kama vile nanasi na nyinginezo zinazopatikana katika maeneo hayo sanjari na kuleta urahisi watu kuingia na kutoka kwenye maeneo hayo.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...