Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Maji, Dk. Mary Nagu (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu Serikali kutoa mapema vibali vya uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi ili kuweza kuziba upungufu ya bidhaa hiyo nchini. Kulia ni Mjumbe wa Kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa.
Na Dotto Mwaibale
KAMATI ya Bunge ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Maji, imeitaka Serikali kutoa mapema vibali vya uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi ili kuweza kuziba upungufu ya bidhaa hiyo nchini.
Pia imeitaka Serikali kudhibiti bandari bubu na njia za panya ambazo huingiza sukari kinyume cha sheria na kuua viwanda vilivyopo na kuifanya Tanzania kununua sukari kutoka nje ya nchi na kuua uchumi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dk.Mary Nagu alisema kwa sasa upatikanaji wa sukari ni mdogo ukilinganisha na mahitaji ambapo kunamapungufu wa tani 80,000 hadi 100,000.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Maji, Dk. Mary Nagu (katikati), akiwa na wajumbe wa kamati hiyo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Mwanahabari kutoka TBC, Angela Msangi (kulia), akiuliza suala katika mkutano huo.
Alisema mapungufu hayo yanatokana na viwanda vinavyozalisha sukari nchini kuzalisha tani 302,0000 huku mahitaji ya sukari kwa nchi nzima ni tani 402,0000.
Alisema kwa sasa kuna viwanda vitano tu ambavyo huzalisha sukari ambayo haitoshi kwa matumizi ya wananchi nchini hapa na kusababisha mapungufu hayo.
Hata hivyo alisema pamoja na viwanda hivyo kuzalisha chini ya kiwango kinacho hitajika katika kipindi hiki cha mwezi Machi hadi Juni viwanda hivyo hufungwa kwaajili ya kupisha ukarabati hivyo kwa kipindi hicho sukari inayotumika ni ile ambayo ilizalishwa katika kipindi kilicho pita.
Alisema kutokana na hali hiyo ni vema Serikali ikahakikisha inaagiza sukari hiyo mapema ili kuweza kuziba pengo la mapungufu ya sukari katika kipindi muafaka ili isiweze kugongana na sukari iliyopo na kusababisha kuua uzalishaji nchini.
"Hivyo kutokana na mapungufu hayo ili kufidia mapungufu hayo kati ya utumiaji na uzalishaji sukari inaagizwa kutoka nje, hivyo ikiagizwa tani 80,000 hadi 100,000 kuna kuwa hakuna mapungufu.
"Baada ya kupata taarifa ya mapungufu hayo kutoka katika bodi ya sukari tukaona humuhimu wa kumuomba Rais, kutoruhusu mapungufu ya sukari yatokee katika kipindi hichi ambacho viwanda vya sukari vinafungwa na kusimamisha uzalishaji kuanzia mwezi Machi hadi Juni kwa kuagiza mapema," alisema.
Hata hivyo alisema kuwa pamoja na mapungufu hayo lakini pia kumekuwa na wafanyabiashara wabinafsi wamekuwa wakitumia vibaya mapungufu hayo kwa kuingiza sukari zaidi ya kiwango kinacho hitajika bila kujali uchumi wa nchi unavyodidimia.
"Katika wafanyabiashara hao wapo ambao wanaingiza sukari kwaajili ya kupeleka katika nchi nyingine lakini sukari hiyo inabaki humuhumu bila kuuza na baadae kuuza kwa bei kubwa hivyo kuua uchumi wa nchi," alisema.
Alisema ni vema Serikali kuhakikisha hairuhusu mapungufu ya sukari kwani mapungufu hayo kwa kuingiza sukari hiyo kwa wakati kwani usheleweshwaji unaweza kusababisha kuuzwa kwa bei ya juu na hivyo kuua uchumi, pamoja na kuifanya nchi ya kununua sukari kutoka nje.
Aidha Kamati hiyo iliitaka Serikali kufunga bandari bubu na kudhibiti njia za panya za uingizaji wa sukari, kutobakiza sukari zinazotakiwa kuuzwa nje ya nchi kubaki nchini na kuwekwa mahali ambapo hapajulikani na baadae kuuzwa kwa bei ya juu kunapokuwa na mapungufu ya sukari.
"Sisi kama kamati tunaendelea kumshukuru rais na tutaendelea kuisaidia Serikali kusisitiza uzalishaji wa sukari ya kutosha na ziada ya kupata sukari kutoka nje uwezekano upo.
"Hivyo tumeapa katika kumsaidia rais katika kuhakikisha sukari inazalishwa ya kutosha na inakuwa na tija, viwanda vinafanya kazi, na nahakika siku moja Tanzania itakuwa nchi ya kuuza sukari nje na badala ya kununua," alisema.
Pamoja na hilo lakini pia ni vema ikahakikisha Tanzania isiwe eneo la kuuza sukari za nchi nyingine na kuua uchumi uliopo na kukuza wa nchi hizo.
Alisema pia Serikali inawajibu wa kufuatilia utaratibu za uingizaji wa sukari kwani kamati hiyo imegundua tatizo hilo lisipotatuliwa bei ya sukari haiwezi kudhibitiwa kutokana na hali ya kisoko.
Alisisitiza kuwa pia ni vema wazalishaji kutumia muda mwingi wa kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji na kununua miwa kutoka kwa wakulima.
Hivyo alisema kama kamati imeona umuhimu wa kuwawezesha wakulima kulima ili viwanda vinapopanua uzalishaji kupata malighafi za kutosha.
No comments:
Post a Comment