https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, January 14, 2015

Bayport yaja na ‘Chagua chochote unachotaka Bayport italipia’

Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo kushoto, akizungumza jambo na waandishi wa habari hawapo pichani katika uzinduzi wa huduma mpya ya 'Chagua chochote Bayport italipia' jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Meneja Biashara, Thabit Mndeme.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAASISI ya kifedha ya Bayport Financial Services, imezindua tena huduma mpya inayojulikana kama ‘Chagua chochote unachotaka Bayport italipia’, ikiwa na lengo la kuwapatia mikopo ya bidhaa mbalimbali wateja wao na Watanzania kwa ujumla.


Huduma hiyo ni mwendelezo wa ile 'Mikopo ya Bidhaa' ambapo watu wanakopeshwa bodaboda, sambamba na Bima ya Elimu iliyozinduliwa pia mapema mwaka jana kwa ajili ya kuleta urahisi katika mfumo wa maisha ya Watanzania wengi.


 Ngula Cheyo anazungumza jambo na kulia kwake ni Thabit Mndeme.
Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hiyo mpya, Meneja Biashara wa Bayport Financial Services, Thabit Mndeme, alisema huduma hiyo sasa itawapatia fursa wateja wao kukopeshwa magari, nyumba, vifaa vya ujenzi, pembejeo za kilimo, ada ya shule, pikipiki, bajaj, tv, injini ya boti na nyinginezo kwa ajili ya kuwapatia mwangaza mzuri wa kimaisha na kiuchumi.

Alisema kuwa kuanzisha huduma hiyo mpya imetokana na ile ya mikopo ya bidhaa kufanya vizuri tangu ilipozinduliwa mwishoni mwa mwaka jana na kupatikana nchi nzima kwa kupitia matawi yaliyosambaa katika mikoa mbalimbali.
Meneja Biashara wa Bayport Financial Services, Thabit Mndeme kulia akizungumza jambo katika uzinduzi wa huduma mpya ya 'Chagua chochote Bayport italipia', ikiwa ni mwendelezo wa huduma ya mikopo ya bidhaa, ambapo wateja wa Bayport wanapata fursa ya kukopeshwa bidhaa mbalimbali, kama vile nyumba, magari, vifaa vya ujenzi na nyinginezo.
Picha zote na Mpiga Picha Wetu.

 “Bayport ilifanya mazungumzo na wateja wake mbalimbali baada ya kuzindua huduma ya Mikopo ya Bidhaa na kuona mafanikio makubwa waliyopata, hivyo mwaka huu tumeona tufike mbali zaidi kwa kuangalia namna gani Watanzania wanaweza kukopeshwa bidhaa nyingi kwa ajili ya kukuza uchumi wao.

“Ni rahisi mno kupewa mkopo wa chagua chochote unachotaka Bayport italipia kwasababu anachotakiwa kufanya mteja ni kuchagua bidhaa anayoitaka katika duka au msambazaji yoyote aliye karibu naye, kisha atapewa fomu ya malipo na kuipeleka kwenye tawi la Bayport lililo karibu yake ili apate mkopo aliyohitaji,” alisema Mndeme.
Alisema kuwa baada ya kuzinduliwa huduma hiyo ya Mikopo ya Bidhaa, wengi waliipenda na kunufaika nayo, hivyo aliwaomba wateja wao na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuiunga mkono Bayport Financial Services kwa ajili ya kuwapatia maisha bora, maana ndiyo kusudio lao.


Naye Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba taasisi yao inayojihusisha na mambo ya mikopo inatambua namna bora ya matokeo mbalimbali ya kuwaendeleza kiuchumi, hivyo huduma hizi ni mwendelezo wa juhudi za kukuza uchumi wa watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni zilizoidhinishwa.


“Tunajivunia kufanya kazi kwa bidii na kupanua wigo wa huduma zetu kwa matawi 80 nchi nzima, jambo linalotupa shauku ya kuona nchi yetu inapiga hatua kiuchumi kwa kuwawezesha watumishi wa umma na kampuni zilizoidhinishwa na Bayport kwa kuwapatia mikopo waipendayo, huku pia tukiwaeleza kwamba tumehamia jengo jipya la Bayport House, Morocco kwa ajili ya kuwahudumia vizuri zaidi," alisema Cheyo.

Aidha, Cheyo aliwashukuru wateja wao na Watanzania kwa ujumla kwa kuwaunga mkono miaka 9 tangu walipoanza kutoa huduma ya mikopo, huku akisema kuwa taasisi yao itaendelea kufanya kazi kwa moyo wote ili kuhakikisha kwamba pato la wananchi linakuwa kwa kuwakopesha ili wajikwamue kiuchumi.

Bayport Financial Services ni taasisi ya isiyokuwa ya kibenki inayoongoza kutoa mikopo barani Afrika na Amerika ya Kusini, huku ikianzishwa mwaka 2001 na umiliki wake ukiwa nchini Mauriritius, ambapo pia kwa Tanzania ilianzishwa rasmi mwaka 2006, huku ikiwa na matawi 80 nchi nzima.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...