Na Mwandishi Wetu, Handeni
MKUTANO wa kwanza wa taasisi ya Handeni Kwetu Foundation
uliyofanyika jana Novemba 19, katika kijiji cha Misima, wilayani Handeni,
mkoani Tanga na kuwakutanisha wananchi wote umeibua kero nyingi za wananchi,
ikiwamo ya kijiji chao kuingizwa kwenye Halmashauri ya Mji bila ridhaa yao.
Mmoja
wa wakazi na wananchi wa kijiji cha Misima, akilalamikia eneo lao
kuingia kwenye Halmashauri ya Mji kinyume cha sheria ya utawala bora,
ikiwa ni pamoja na kutoshirikishwa kwa lolote na viongozi wa juu.
Taasisi hiyo ilianzishwa mapema mwaka huu na kuzinduliwa Mei
8 jijini Dar es Salaam, ilifanya mkutano mkubwa wa hadhara Misima, ambapo umati
wa wanchi ulihudhuria, huku kero nyingi zikiwasilishwa na kudhihirisha
changamoto za utawala bora zinazoathiri maendeleo ya Tanzania.
Wakizungumza kwa uchungu mkubwa, mwananchi wa Misima
aliyejitambulisha kwa jina la Mhina Ally, alisema viongozi wa Halmashauri kwa
kushirikiana na madiwani waliamua kuingiza kijiji chao katika Halmashauri ya
Mji bila ya kuwashirikisha, ikiwamo kubandika tangazo la pingamizi kwa siku 90
katika maeneo yao kama sheria inavyotaka.
Alisema kutoka Handeni Mjini hadi katika eneo lao ni kilomita
16 zilizozunguukwa na mapori yanayowafanya wananchi wajihusishe na kilimo kwa
asilimia 99, hivyo kuingizwa kwenye sheria za mji ni kusababisha ugumu wa
maisha.
“Inashangaza mno kusikia Tanzania kuna utawala bora wakati
viongozi wachache wanaweza kufanya watakavyo; hali inayoweza kuleta mapigano
makubwa, endapo wananchi tutasimama kidete kudai haki zetu zinazokandamizwa na
viongozi kila siku,” alisema.
Ally alifika mbali zaidi kwa kusema walisikia tangazo redioni
la kuingizwa kwenye Halmashauri ya Mji, huku tangazo la pingamizi likishindwa
kuwekwa kijijini kwao kwa hofu ya kupingwa na wananchi wao.
“Viongozi wa serikali ya kijiji waliamua kutoliweka tangazo
la pingamizi kijijini kwetu kwasababu wanajua fika tusingekubali, hivyo
inashangaza malalamiko yetu kufumbiwa macho na serikali inayoitwa sikivu, licha
ya kuzunguuka sehemu nyinyi, kama kwa Mkuu wa wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa
Tanga, alipokaimu DC Halima Dendego, ambaye sasa amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,”
aliongeza.
Naye Naye Idd Kisege alisema kuwa ili kuona viongozi
wanaogopa kufika Misima, hata namba kwenye nyumba zao hakuna ingawa wanatangaza
uchaguzi kwa sheria za mji katika kijiji chao, jambo lisiloweza kuvumiliwa na
kila mpenda maendeleo ya Misima.
“Watu wa Misima tunaambiwa sisi ni watata, wakorofi tunapodai
haki zetu, ili waendelee kutuburuza, ndio maana kwenye ziara ya Mheshimiwa
Rais, Profesa Jakaya Mrisho Kikwete waliniburuza Polisi kwasababu ya kuonyesha
bango kwa mheshimiwa ili kuona kero zetu,” alisema Kisege.
Naye Mkomwa Athuman alisema kuwa Misima haipo tayari
kutumikia sheria za Mji kwakuwa ni mapema mno kwao, hivyo wanaomba serikali,
ikiwamo ofisi ya Waziri kulifuatilia suala hilo kwa kina.
“Mzozo huu umeshakuwa mkubwa na kuondoa ushirikiano kabisa
kwa viongozi na wananchi wa hapa Misima, hivyo tayari malalamiko yetu
yamefikishwa Ofisi ya Waziri Mkuu kulishtakia suala hilo kwasababu sheria ya
kuingia kwenye Mamlaka ya Mji Handeni haijafuatwa na imeanzishwa na watu
wachache ili kuzima uozo wa ardhi waliyoufanya kwenye kijiji chetu,” alisema.
Katika kila mwananchi aliyezungumza kwenye mkutano huo
alionyesha kuguswa na kero hiyo ya mji, huku wakisema kutoka Handeni Mjini hadi
Misima ni mbali pamoja na viongozi kushindwa kufuata sheria za utawala bora.
Awali, mkutano huo ulioanza saa tisa alasiri ulifunguliwa na
mtoa mada wa kwanza, Kambi Mbwana, ambaye ndiye Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo, aliyejikita
sababu na dhamira kuu ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Mbwana alisema kuwa sababu kubwa ya kuanzishwa kwa taasisi
hiyo ni kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha utawala bora, ikiwa ni njia moja
wapo ya kuwafanya Watanzania wote wajiletee maendeleo kwa kushirikiana baina yao
na viongozi wote.
Akizungumzia utawala bora, Makamu Mwenyekiti wa taasisi hiyo,
Adam Malinda, alisema kwamba matatizo mengi katika jamii yamekuwa yakichangiwa
na viongozi wasiojua nini maana ya utawala bora.
“Utawala bora ni somo muhimu na lazima lipigiwe kelele na
watu wote, maana malalamiko mengi ya watu wa Misima yamesababishwa na tatizo hilo,
ndio maana unaona kero zimepamba moto,” alisema.
Malinda aliwataka viongozi wa juu, wakiwamo wa Halmashauri ya
Wilaya ya Handeni kuzungumza na wananchi wa Misima ili kutatua mtafaruku huo
kwa ajili ya kuwafanya wananchi waendelee na shughuli za kujiletea maendeleo,
sambamba na serikali kuwafanyia kazi watendaji wabovu.
Kuhusiana na mzozo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Mji wa Handeni, Thomas Mzinga, alikaririwa akisema kuwa utaratibu ulifuatwa,
ikiwamo kutoka kwa siku 60 za pingamizi, ingawa wananchi hao walishindwa kupita
njia hiyto kwa ajili ya kufanikisha malengo yao.
No comments:
Post a Comment