Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSANII wa muziki wa mashairi, Said
Machenje, amesema ameanza mazoezi rasmi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa anakuwa
mmoja wa wasanii watakaotoa burudani kali katika tamasha la NSSF Handeni Kwetu,
linalotarajiwa kufanyika katika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio,
mjini Handeni, mkoani Tanga.
Machenje anayeshindana vilivyo na mkali wa muziki huo, Mrisho
Mpoto alisema kuwa maandalizi yake yanakwenda sambamba na shauku ya kutembelea
kwa mara ya pili wilayani Handeni.
Akizungumzia hilo jijini Dar es Salaam, Machenje alisema kwamba mwaka
jana alipanda jukwaani kuimba kwa kushirikiana na kikundi cha Naukala Ndima,
ila msimu huu amefanikiwa kupata mwaliko wake binafsi.
Mwimbaji huyo wa 'Kajenge kwa Mumeo' na 'Mila', alisema kwa kualikwa binafsi, kunamfanya apate hamu ya kujiandaa
kwa ajili ya kufanya mambo makubwa zaidi ili kuonyesha umahiri wake katika
tasnia ya muziki wa mashairi.
“Nashukuru Mungu kwa kupangwa kuwa mmoja wa wasanii watakaotoa
burudani katika tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014, wilayani Handeni mkoani
Tanga kwakuwa ni mwelekeo mzuri katika maisha yangu ya sanaa.
“Nafanya mazoezi makali kwa ajili ya kujiweka sawa ili nifanye
shoo nzuri Desemba 13, katika Uwanja wa Azimio, ukizingatia kuwa nina uzoefu
sasa na jukwaa la tamasha hili la aina yake,” alisema.
Wadhamini tamasha hilo ni Shirika la Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo
chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa,
Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex
Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media
Group.
No comments:
Post a Comment