WAZEE wa zamani walikuwa
na makusudi yao kuweka msemo usemao sikio la kufa halisikii dawa. Na wakati
mwingine wanasema siku ya kufa nyani miti yote huteleza. Misemo hii na mingine
mingi inaelezea namna gani hutokea matatizo yanayokosa jinsi ya kuyatatua.
Ninaposema hili,
najikuta nikikosa hamu ya kusikiliza au kusikia porojo zinazoitwa kuendeleza soka
la Tanzania, chini ya Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi. Malinzi aliyeingia madarakani
hivi karibuni akirithi mikoba ya Leodgar Tenga, amekuwa akikabiliwa na matizo
mengi, kiasi cha kuamini kuwa sikio la kufa halisikii dawa.
Hakika siwezi kuvumilia;
TFF eti inajaribu kuangalia namna ya kuboresha jezi za timu ya Taifa, Taifa
Stars. Sasa jezi zinasaidia nini? Hata tukivaa jezi za aina gani, kama hatuna
soka zuri tunanufaika na kitu gani?
Huu ni ubabaishaji
uliyoje? Malinzi na jopo lake kubwa analoteua kila uchao anapaswa kuwa makini
mno ili asiharibu mwenendo wake mzuri. Kinyume cha hapo ni hasara tupu. Wizara
ya Habari, Utamaduni na Michezo iliwahi kutangaza mchakato wa vazi la Taifa.
Hadi leo haijulikani mchakato huo umeishia wapi?
Eti mshindi wa jezi ya
nyumbani atapewa Sh Milioni moja kama atakavyopewa mshindi atakayebuni jezi za
ugenini. Huku ni kupotezeana muda. Hizo Milioni 2 kama zipo TFF si alete
mashindano japo ya Kata au wilaya?
Hizo Milioni 2 zinaweza
kununulia vifaa vya michezo na kuwapa vijana wanaopenda kucheza soka ili hali
hawana vifaa vya michezo? Hakika siwezi kuvumilia. Kwa upande wangu sikuwa na
hamu kabisa ya kumlaumu Malinzi. Lakini kadri muda unavyosonga mbele
kunafanyika matatizo yanayovunja ukimya.
Au pia wakati mchakato
huo unaundwa, pengine kumeshapatikana mshindi na kuna kitu kinataka kufanywa.
Malinzi, jezi hazina manufaa kwa sasa. Wala usisimbuke kuzibadilisha au
kuziboresha maana zipo.
Watanzania wanataka soka
safi. Soka la kuvutia litakalotupandisha chati na kuwaita mawakala wa Kimataifa
kwa ajili ya wachezaji wetu. Huu ndio ukweli unaonifanya nishindwe kuvumilia
mchana na usiku.
Kinyume cha hapo,
utendaji kazi wa TFF ya sasa ni kuboresha jezi na kuhama ofisi kama vile mambo
hayo hayakuwapo kabla ya uongozi wao.
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949
No comments:
Post a Comment