Na Mwandishi Wetu, Handeni
SHIRIKA la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF Tanzania,
limejitokeza tena kudhamini Tamasha kubwa la Utamaduni linalojulikana kama ‘Handeni
Kwetu’, lililopangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio (Kigoda
Stadium), wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Huduma kwa Wateja kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Eunice Chiume, pichani.
Hii ni mara ya pili kwa mfuko huo wa hifadhi kudhamini
tamasha hili la utamaduni lilioanza mwaka jana, ambapo lilifanyika kwa mafanikio
makubwa kwa kushirikisha vikundi vya ndani na nje ya Handeni, wakiwamo wa
jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia hilo, Mratibu Mkuu wa Tamasha
hilo, Kambi Mbwana, alisema kujitokeza kwa NSSF ni kitendo cha kiungwana
kinacholiweka tukio lao katika kiwango kizuri na mafanikio makubwa.
Alisema kwa kuliangalia hilo, wameamua kutoa haki ya jina,
ambapo sasa tamasha lao litakuwa linajulikana kama NSSF Handeni Kwetu,
wakiamini kuwa ni ishara nzuri ya ushirikiano baina yao na wadau wote wa
shirika hilo.
“Yapo mashirika mengi Tanzania bila kusahau kampuni ambazo
zingeweza kudhamini matukio ya aina hii ambayo yana mchango mkubwa kwa taifa
letu, lakini baadhi yao yamekuwa magumu mno kudhamini au hata kuyasaidia kwa
namna moja ama nyingine.
“Shirika kama NSSF linapoamua kuingia kudhamini ni kuonyesha
jinsi wanavyoithamini jamii yao, jambo ambalo kwetu sisi ni furaha kubwa na
kuona ipo haja ya kutafuta namna ya kurudisha fadhira kwa wadau hawa muhimu
nchini Tanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Mbwana, siku ya tamasha, kutakuwa na shughuli
ya kusajili wanachama wapya wa kujiunga na NSSF, ili waweze kunufaika na huduma
za mafao kwenye Shirika hilo kubwa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii hapa nchini.
Wadhamini wengine wa tamasha hilo ni pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa
Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu
Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of
Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.
No comments:
Post a Comment