https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, May 11, 2017

Serikali kujenga nyumba za askari magereza 9500 nchini



Na Mwandishi Wetu, MOHA
Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Benki ya Exim inatarajia kujenga nyumba 9500 za askari magereza ili kukabiliana na changamoto za makazi ya askari  wa jeshi hilo hapanchini.

Naibu Waziri wa Wizaraya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akishirikiana na Viongozi wengine kufungua Gereza la Wanawake wilayani Mpwapwa lililojengwa na wataalamu ambao ni askari magereza kwa kushirikiana na wafungwa. Ufunguzi huo umefanyika wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma. Picha na Wizara ya  Mambo ya Ndani ya Nchi



Akizungumzia changamoto za makazi ya askari wa Jeshi la  Magereza Nchini, wakati wa uzinduzi wa Gereza la Wanawake wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, alisema Serikali inatambua changamoto za makazi kwa askari magereza na tayari iko katika mazungumzo na benki ya Exim ili iweze kujenga nyumba hizo.

“Nawaomba  askari wetu nchi nzima  wawe na subira  Serikali inatambua na  inashughulikia changamoto ya makazi ya  askari na tayari tuko katika mazungumzo na wadau ikiwemo benki ya Exim kuanza mradi wa ujenzi wa nyumba takribani 9500, lengo ni kukidhi kiu ya makazi ya askari na familia zao,” alisema Masauni.

Awali akitoa maelezo ya ujenzi wa Gereza hilo, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, Dk. Juma Malewa alisema ujenzi wa Gereza hilo umefanywa na wataalamu ambao ni askari Magereza kwa  kushirikiana na wafungwa kama sehemu ya utekelezaji wa  amri ya Mh. Rais Dk. John Magufuli ya kutaka wafungwa watumike katika kazi za uzalishaji ikiwemo kilimo,ujenzi na ufundi mbalimbali.

Ujenzi wa Gereza hilo umegharimu jumla ya shilingi milioni 65 na litasaidia pia kuhifadhi wafungwa 148 na hivyo kupunguza msongamano wa wafungwa katika Gereza la Kongwa mkoani Dodoma pamoja na kuepuka usumbufu wa  ndugu wa wafungwa kusafiri mpaka wilayani Kongwa kwenda kuwaona ndugu zao.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...