https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, October 31, 2016

Mkutano wa wadau wa pamba wafanyika mkoani Singida

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe akifungua Mkutano wa wadau wa pamba wenye dhamira ya kujadili maendeleo ya kilimo cha zao la Pamba katika mkoa wa Singida.
 Wadaau wa kilimo cha Pamba Mkoa wa Singida wakifuatilia kwa makini Mkutano wa kujadili namna bora ya kuimarisha kilimo cha zao hilo katika Mkoa wa Singida.
 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akisisitiza jambo wakati wa Mkutano wa wadau wa pamba Mkoa wa Singida
 Wadaau wa kilimo cha Pamba Mkoa wa Singida wakifuatilia kwa makini Mkutano wa kujadili namna bora ya kuimarisha kilimo cha zao hilo katika Mkoa wa Singida

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bi Rustika Turuka akisisitiza jambo wakati wa Mkutano wa wadau wa kilimo cha Pamba Mkoa wa Singida
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe Elias Choro Tarimo akisisitiza jambo wakati wa Mkutano huo
 Moja ya wakulima wa Kilimo cha pamba Wilayani Ikungi Timoth S. Nkulu akimuomba Mkuu wa Wilaya kuzisimamia Wilaya zote kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa uzalishaji wa kilimo hicho.
 Wadau wa kilimo cha pamba wakihakiki maazimio waliyoyapitisha

Na Mathias Canal, Singida

Zao la Pamba ni miongoni mwa mazao ya kipaombele ya biashara yanayozaliswa Mkoani Singida kwa kuwa linastahimili hali ya hewa ya Mkoa ya uwepo wa mvua zenye mtawanyiko usioridhisha kwa baadhi ya maeneo ambapo kutokana na hali hiyo Mkoa unaendelea kuhimiza wakulima kuzalisha zao hilo kwa kiasi kikubwa ili waweze kuongeza kipato na usalama wa chakula.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa wadau wa kilimo cha pamba Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe wakati akifungua Mkutano huo iliokuwa na dhamira ya kujadili maendeleo ya kilimo cha zao la Pamba katika mkoa huo.

Mhe Mtigumwe amesema kuwa Katika Mkoa wa Singida Kampuni ya Biosustain Ltd inayojishughulisha na Kilimo cha Mkataba imeweza kusaidia zao la Pamba kwa kuanzisha kiwanda cha kuchambua Pamba chenye uwezo wa kuchambua Tani 16,000 kwa mwaka ambapo kupitia kilimo cha mkataba wakulima wa Mkoa wa Singida wamepata pembejeo, Mafunzo ya kilimo bora na soko la uhakika ambapo katika utekelezaji wa kilimo cha mkataba msimu wa mwaka 2015/2016 wakulima 4,204 wamepatiwa mafunzo.

Kwa msimu huu wa Mwaka 2016/2017 Mkoa umepata mgao wa mbegu za Pamba kutoka Bodi ya Pamba jumla ya Tani 120 (Wilaya ya Iramba na Mkalama Tani 80, Wilaya ya Manyoni Tani20 na Wilaya Ikungi na Singida Tano 20) ambazo zinaendelea kusambazwa kwa wakulima.

Imeelezwa kuwa zao la Pamba linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo tija ndogo katika uzalishaji (200 kg/ekari) kutokana na wakulima kutozingatia kanuni bora za kilimo cha pamba, matumizi ya viuatilifu ambavyo havina uwezo wa kudhibiti wadudu waharibifu wa zao la pamba (Feki), Matumizi ya mbegu zisizoota vizuri (Feki), Kubadilika kwa bei ya pamba mwaka hadi mwaka, Mvua zenye mtawanyiko usioridhisha kwa baadhi ya maeneo kwa mfano maeneo ya Bonde la Ufa ya Iramba, Mkalama na Manyoni.

Rc Mtigumwe amesema kuwa Mkutano wa wadau wa kilimo cha Pamba ni fursa nzuri ya kuwakutanisha wadau muhimu wa zao la pamba na kujadiliana mafaniko, Changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kufanikisha kuongeza kwa tija na faida katika uzalishaji wa zao la pamba.
Ameeleza malengo ya kimkoa kulima zao hilo kwa kiwango  kikubwa cha Hekta 8,510 kwa Mwaka 2016/2017 na matarajio ni kuzalisha Tani 8,075.

Katika Mkutano huo kwa umoja wao wadau wa kilimo cha Pamba wamepitisha maazimio 17 kama ifuatavyo:

  1. Wataalamu wa kilimo wa ofisi ya mkuu wa Mkoa na halmashauri za wilaya  watafute ufafanuzi wa deni kwakushilikiana na Biosustain kumpatia Katibu Tawala wa Mkoa ndani ya mwezi mmoja.
  1. Katibu Tawala wa Mkoa awaandikie barua uongozi wa Kampuni ya Quton kuitwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuja kutoa maelezo kwanini hawahudhurii vikao na walete ufafanuzi wa deni wanalodaiwa na namna ya kulilipa.
  1. Halmashauri ya Wilaya ya Singida inatakiwa ilejeshe fedha za ushuru  wa Pamba  kwa halmashauri ya Ikungi iliyolipwa kwao kwa makosa ndani ya miezi sita (6). 
  1. Elimu juu ya Matumizi ya mizani iendelee kutolewa ili kuongeza uelewa na ufanisi kwa wakulima.
  1. Kila halmashauri itoe taarifa ya maendeleo ya zao la Pamba kwenye eneo lake kwenye vikao vya wadau wa Pamba.
  1. Bodi ya Pamba ilete wakaguzi wa Pamba wasiopungua  wawili kwa Mkoa wa Singida ndani ya miezi miwili kuanzia sasa.
  1. Wakurugenzi wapitie na wasimamie mikataba inayoingiwa kati ya Makampuni na wakulima ili kuepuka malalamiko yasiyo yalazima wakati wa utekelezaji.
  1. CDTF wawe ni wajumbe kwenye kikao hiki  na waalikwe kuanzia kikao kijacho ili watoe mchango wao kwa maendeleo ya Pamba katika Mkoa wa Singida.
9)      Bodi ya Pamba iangalie uwezekano wa kuwahusisha watafiti watoe mbegu bora inayostahimili ukame na kutoa mazao mengi.
 
10)   Katibu Tawala wa Mkoa aiandikie Wizara ya Kilimo kuikumbusha kuimarisha udhibiti wa ubora wa viuatilifu.
 
11)   Wakurugenzi wa halmashauri, Bodi ya Pamba na kampuni ya Biosustain waendelee kutoa Elimu stahiki ili kukuza uzalishaji wa Pamba.
 
12)   Kila kaya lazima ilime ekari mbili za Pamba ili tupate Pamba yakutosha kuanzisha kiwanda cha nguo. 
 
13)   Kila shule ya msingi na sekondari lazima iwe na ekari mbili (2) za zao la Pamba ili zitumike kama shamba darasa kwa wanafunzi na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani. 
 
14)   Wakurugenzi wahakikishe vitabu vya mwongozo wa kilimo na mifugo vinapatikana na kuwafikia wakulima, kila kijiji kipate nakala tano (5) kabla ya Januari, 2017.
 
      15) Jalada la usajili lenye orodha ya wakulima na ekari zao kiujumla na mazao wanayoyalima     kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata na Wilaya lifunguliwe na lianze kutumika kuanzia msimu wa 2016/2017.

      16) Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zote ziwe na mashamba darasa ya kilimo cha Pamba.

17) Katibu Tawala Mkoa amwandikie katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo kujua matokeo ya uchunguzi   uliofanywa na TPRI wa Viuatilifu ambavyo havikufanya kazi msimu wa 2015/2016 na hatua zilizochukuliwa.


Wakiwasilisha taarifa ya Kilimo cha zao la Pamba kwa mkataba wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Singida kwa pamoja wamesema kuwa kumekuwa na changamoto nyingi zilizosababisha kupata mavuno machache ya kilimo hicho ikiwemo ubora hafifu wa uzalishaji wa uzalishaji hivyo wameeleza mikakati katika kutimiza malengo waliyojiwekea kwa Mwaka 2016/2017 kuwa ni pamoja na Usimamizi wa karibu wa maafisa ugani, Kusimamia kwa karibu zoezi la ugawaji wa mbegu za pamba, kufanya ziara za hamasa katika maeneo ya wakulima wa zao la Pamba, Kuhamasisha wakulima wengi kulima zao la pamba na kuongezwa vituo vya ununuzi wa pamba.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Suingida Mhe Elias Choro Tarimo amesema kuwa ili kukabiliana na uzalishaji duni wa zao la pamba ni vyema watafiti wakaanza mapema kufanya utafiti juu ya mbegu bora za pamba zenye uwezo wa kuhimili ukame.

Tarimo Amependekeza Kampuni zote zinazoingia mikataba ya kusambaza dawa za pamba na kusambaza dawa feki wafutwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ili kudhibiti dawa feki.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amependekeza kila Halmashauri Kupitia upya ukubwa wa uzalishaji wa kilimo cha pamba ili kuwa na malengo ya kuzalisha zaidi tofauti na mapendekezo yaliyotolewa na Wakurugenzi wa Halmashauri kwani bado yapo kwenye kiwango cha chini cha uzalishaji.

Atoa taarifa ya Kampuni ya BIOSUSTAIN alisema kuwa kampuni hiyo imejipanga kulifanya zao la pamba kuwa zao muhimu kwa wakulima wa mkoa wa Singida kwa msimu wa mwaka 2016/2017 kwa kutoa elimu na kuongeza uzalishaji kutoka kilo 300 hadi kilo 600.

Alisema kuwa lengo kubwa la kampuni hiyo ni kuanzisha kiwanda cha nguo endapo kutakuwa na uzalishaji Mkubwa.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...