https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, December 07, 2014

Tamasha la NSSF Handeni Kwetu sasa Desemba 20



Na Mwandishi Wetu, Handeni
TAMASHA la Utamaduni la NSSF Handeni Kwetu, sasa litafanyika Desemba 20, badala ya Desemba 13, kama ilivyotangazwa hapo awali, huku sababu kubwa ikiwa ni kuwaachia Watanzania washiriki katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika Jumapili ya Desemba 14 nchini kote.
Mratibu Mkuu wa Tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014, pichani akizungumza jambo katika tamasha la mwaka jana lililofanyika kwa mafanikio makubwa wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Akizungumzia hilo leo mjini Handeni, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kwamba hatua ya kusogeza mbele kwa wiki moja, ni kutokana na mguso wa tukio lenyewe na nia ya kuwashirikisha Watanzania wote ili kuliweka tamasha lao katika kiwango cha juu.

Alisema kuwa Desemba 13 ni siku ya mwisho kwa kampeni za ugombea uenyekiti wa serikali za mitaa, vitongoji na mitaa, hivyo kwa kushauriana na jeshi la Polisi wilayani Handeni, wamekubaliana kulifanya Desemba 20.

“Tumeangalia mambo mengi sana hadi kukubaliana lifanyike Desemba 20, ikiwa ni kukosekana kwa wengi, wakiwamo Wakurugenzi ambao kimsingi wao ndio wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo mengi.

“Tunaamini kwa kufanyika Desemba 20, tamasha litakuwa kwenye mvuto pamoja na kukwepa malalamiko kwa baadhi ya wanasiasa ambao huenda wangelalamika endapo lolote lingetokea huku wao kushindwa uchaguzi wao,” alisema Mbwana.

Mbwana alitumia muda huo kuwaomba radhi wadau wote, wakiwamo wasanii, wadhamini na wale waliokuwa wamepanga kutembelea Handeni Desemba 13, huku akiwataka safari yao ifanyike kwa ajili ya Desemba 20, ukizingatia kuwa wote wanaweza kushiriki chaguzi zao na kupata muda mkubwa wa kutembelea wilayani Handeni na mkoa mzima wa Tanga kumaliza mwaka wao vizuri.

 Wadhamini tamasha hilo ni Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.



No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...