https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, October 21, 2011

Pigania ndoa yako mwanamama


NIANZE kwa kukushukuru wewe uliyepata nafasi ya kusoma kazi zangu, ikiwamo hii inayoelezea mambo ya uhusiano na maisha, yanayogusa hisia za wengi duniani.
Nasema hivyo maana suala la uhusiano ni zito kuliko inavyochukuliwa na baadhi ya watu. Baadhi yao wanafikiri kuwa wakiachana na waume zao leo, basi kesho atapata mwingine.



Sawa, ila sio jambo zuri. Sio njia nzuri katika maisha yako. Ni tabia mbaya inayotakiwa ipingwe na wote. Utajisikiaje ukiwa na umati wa watu ambao uliwahi kuwa na uhusiano nao?
Sio ajabu unaweza kuonekana wewe ni muhuni, maana kwanini uachwe na waume zaidi ya watano? Kwanini? Kuna nini hapo? Je, wewe ndio tatizo au mwenzako?
Haya ni maswali tunayotakiwa kujiuliza wote kwa pamoja ili kulinda ndoa zetu au uhusiano sisi wote. Msomaji wangu mpendwa, binadamu wengi tabia zao hufanana japo sio sana .
Japo kuwa kuna tabia mbaya na nzuri, ila mwisho wa siku, kwako wewe zinaweza kuwa kero. Hivyo, ukiona mwenzako anakwenda njia tofauti, unaweza kumuweka chini.
Lakini sio sababu ya kuvunja uhusiano wako haraka, maana umekutana na mtu njiani amekuvutia zaidi ya yule uliyekuwa naye. Ukifanya hivyo, ni kujiweka matatani.
Nasema hivyo maana unaweza kuondoka na kwenda kwa mwingine, ila ukakuta kasumba kubwa mno. Hapo hutafurahia zaidi ya kulia na kusaga meno. Ni baada ya kujidanganya mwenyewe.
Utashangaa kwanini ulifanya hivyo? Siku zote majuto ni mjukuu. Huna haja ya kulia. Ni wakati wako wa kuangalia mwenzako anakwendaje kwa kumuweka chini.
Ndio anaweza kuwa mnywaji sana wa pombe. Kwa bahati mbaya tabia yake ya ulevi wewe huitaki. Nadhani kwa kupitia wewe mwenyewe anaweza kuacha.
Ni baada ya kumwambia kistaarabu na kumuelezea jinsi gani anatakiwa awe ili aweze kuwa na wewe. Endapo yupo kwenye msingi wa kujenga nyumba yenu ya upendo anaweza kupunguza kama sio kuacha.
Nadhani hiyo ni tabia nzuri mno inayotakiwa ifanywe na wote, maana mapenzi mazuri siku zote ni kusikilizana. Hakuna njia ya mkato katika hilo . Ndio maana nasema pigania uhusiano wako.
Na kwa yule aliyejaliwa kufunga ndoa, basi ahakikishe kuwa analinda ndoa yake kwa kuzima zile dosari zinazoweza kuhatarisha usalama wa ndoa yake kwa sababu moja ama nyingine.
Wapo watu ambao kosa kidogo tayari wamedai talaka. Kwao wao ni bora wakimbilie talaka maana wameona mitaani wapo watu wanaoweza kuishi naye na kuendelea kujaza idadi ya wapenzi.
Inakera mno. Inatia aibu kama mtaa mzima umeumaliza kwa njia hiyo hiyo. Tabia ambazo baadhi yao zinaepukika endapo kwa mikono yako, mdomo wako na miguu yako itapigania kwa dhati suala hilo .
Watu watakucheka. Mwanamke kubadilisha wanaume zaidi ya watano kwa kipindi kifupi huo ni uhuni. Unajipakaza matope na kuonekana kituko mtaani na kuitwa majina mengi ya karaha.
Hutaweza kuwakataza watu kukuita wewe ni cha wote, jamvi la wageni na mengine lukuki. Kwanini uwakataze wakati ni kweli? Ajabu, utakapoitwa hivyo, watu watakusikia na kukuonea huruma.
Sio wote wanaweza kuwapenda wasichana wenye sifa mbaya kama hizo, hivyo ni wakati wako kujifunza kutokana na makosa. Muweke chini mtu wako kwa ajili yako.
Mfundishe tabia nzuri na upiganie kikweli uhusiano wako kwa faida yako na sio kukimbilia talaka au kuvunja mkataba wenu, maana sio vizuri na hakuna haja ya kujaza wanaume.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...