https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, February 20, 2017

Mbunge wa Mkuranga aongoza tukio la kuchangia damu Dar es Salaam

Mgeni rasmi wa kongamano la kuchangia damu lililoandaliwa na Tanzania Yemen Professional Foundation (TYPF), Abdallah Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga akizungumza umuhimu wa kila Mtanzania kujitolea damu ili kuinusuru jamii yake. Picha zote na Mpiga Picha Wetu.


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MBUNGE wa Mkuranga, Mheshimiwa Abdallah Ulega, mwishoni mwa wiki aliongozana na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jasem Al Najem, katika tukio la uchangiaji wa damu lililoandaliwa na Taasisi ya Tanzania Yemen Professional Foundation (TYPF), lililofanyika katika Ukumbi wa City Garden, jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo, watu mbalimbali walishiriki katika uchangiaji damu kama sehemu ya kutatua changamoto ya upungufu wa damu kwa wenye uhitaji, wakiwamo akina mama wajawazito, ajali za barabarani na majanga mengine.
Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, H.E Jasem Al Najem akitolewa damu katika tukio la kuchangia damu lililofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa City Garden, jijini Dar es Salaam.


Akizungumza katika uchangiaji huo, Mbunge Ulega alisema kwamba jukumu la kuchangia damu linamuhusu kila Mtanzania, huku akiwataka watu kujenga mazoea ya kujitolea damu ili kuondoa upungufu wa damu.

Alisema kwamba mahitaji ya damu kwa nchi yetu ni makubwa, hivyo amefarijika kwa kupata mwaliko wa kuwa mgeni rasmi sambamba na kuongoza tukio hilo la uchangiaji wa damu, akiamini amejitolea jambo la msingi na la lazima.
Mbunge wa Mkuranga mkoani Pwani, Abdallah Ulega, akizungumza na Balozi wa Kuwait, Jasem Al Najem wakati wanatoa damu kwenye tukio lililoandaliwa na TYPF mwishoni mwa wiki.

Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jasem Al Najem wakati anapima uzito dakika chache kabla ya kutoa damu katika tukio lililofanyika mwishoni mwiki.


“Nimefarijika kwa mwaliko wenu na jinsi nilivyoshiriki juu ya utoaji wa damu nikiamini kwamba naweza kusaidia wenye uhitaji wanapokuwa Hospitalini ambapo juu ya damu inayohitajiwa kwa kiasi kikubwa ili kuwanusuru wagonjwa wetu,” Alisema Ulega na kuwataka TYPF kuelekea jimboni kwake Mkuranga kwa ajili ya kuandaa matukio ya aina hiyo ili waendeleze juhudi zao za kuchangia damu.

Naye Balozi Najem alisema kuchangia damu ni sehemu ya malengo yake binafsi pamoja na ofisi yake, hivyo yupo tayari kusaidia kwa namna moja ama nyingine ili kuwasaidia watu wote wenye uhitaji wa damu nchini Tanzania.

“Nimejiwekea utaratibu wa kujitolea katika jamii yakiwamo haya mambo ya damu, hivyo pamoja na kuwashukuru waandaaji wa tukio hilo pamoja na mliohudhuria kuja kutoa damu, naomba niwaambie bado nipo tayari kujitolea wakati wowote itakapohitajika,” Alisema Balozi Najeem.


Awali Mtendaji Mkuu msaidizi wa TYPF, Swalehe Jabri, aliwashukuru waliojumulika nao kutoa damu, akisema wamefanya jambo kubwa linalohitaji kuungwa mkono na kila Mtanzania mpenda maendeleo, akiamini utaratibu huo umelenga kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji wa damu kwenye hospitali nchini.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...