Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAMASHA kubwa la umataduni linalojulikana kama 'Handeni Kwetu'
limepangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio, wilayani
Handeni, mkoani Tanga.
Mratibu Mkuu wa Tamasha la Handeni Kwetu, Kambi Mbwana, akizungumza jambo katika tamasha la mwaka lililofanyika Desemba 14. Mwaka huu tamasha hilo litafanyika Desemba 13, Siku ya Jumamosi, katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, mkoani Tanga. Picha na Maktaba Yetu.
Wasanii wa kundi la ngoma za asili la Mgambo JKT, wilayani Handeni, mkoani Tanga, wakitoa burudani katika tamasha hilo mwaka jana. Mwaka huu litafanyika Desemba 13, Siku ya Jumamosi, katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, mkoani Tanga. Picha na Maktaba Yetu.
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu (katikati), akifurahia katika tamasha hilo mwaka jana lililofanyika Desemba 14. Mwaka huu litafanyika Desemba 13, Siku ya Jumamosi, katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, mkoani Tanga. Kulia kwake ni Afisa Utawala wa wilaya ya Handeni, Upendo Magashi. Picha na Maktaba Yetu.
Katika tamasha hilo linalofanyika kwa mara pili, burudani
mbalimbali za ngoma za asili zinatarajiwa kuonekana jukwaani, ambapo pia
vikundi kutoka nje ya Handeni, mkoani Tanga navyo vitaalikwa kwa ajili ya kwenda kutoa burudani wilayani humo.
Akizungumzia hilo, jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkuu wa
tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa maandalizi ya tamasha hilo yanawekwa
ili kuliweka katika kilele cha ubora na kuchangia maendeleo ya sanaa na uchumi
kwa ujumla.
Alisema kuwa mwaka jana tamasha hilo lilianza kwa mafanikio
makubwa, ambapo wageni mbalimbali walifika wilayani humo, jambo lililochangia
pia kuitangaza Handeni na mkoa mzima wa Tanga.
“Mwaka huu tumeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa
tamasha letu linaendelea kukua kwa kasi baada ya kuanzishwa kwa mafanikio
makubwa mwaka jana.
“Naamini kuwa haya ni matunda ya kushirikiana kwa pamoja na
wadau wote, ikiwamo serikali kwa kupitia ofisi zote za wilaya ya Handeni, hivyo
watu wajiandae mambo mazuri na makubwa kutoka kwenye tamasha hili,” alisema
Mbwana.
Tamasha la utamaduni la Handeni, linalojulikana kama Handeni
Kwetu, ni miongoni mwa matamasha yenye mchango mkubwa, ambapo kwa mwaka jana
Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ndio waliokuwa wadhamini wakuu na kufanikiwa
kwa kiasi kikubwa kuliweka katika mguso wa aina yake.
No comments:
Post a Comment