Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSUGUANO wa mbio za Urais katika Shirikisho la Soka nchini (TFF), umeendelea
leo baada ya mgombea wa nafasi hiyo kubwa katika ngazi ya mpira wa miguu
Tanzania, Athman Nyamlani kutaja vipaumbele tisa vya maendeleo ya soka, iwapo
atapata ridhaa ya wapiga kura kuliongoza Shirikisho hilo.
Mgombea nafasi ya Urais wa TFF, Athuman Nyamlani, akifanya mahojiano na waandishi katika moja ya matukio ya kimichezo Tanzania.
Maneno ya Nyamlani yamekuja baada ya kujitosa katika kinyang’anyiro
hicho cha Uchaguzi Mkuu wa TFF, akipambana na Jamal Malinzi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, katika Ukumbi wa Idara ya
Habari (MAELEZO), ikiwa sehemu ya uzinduzi wa kampeni zake za uchaguzi
utakaofanyika Jumapili, Nyamlani alisema akipewa nafasi hiyo, atainua kiwango
cha soka kwa kutekeleza msingi imara wa soka la Tanzania.
Nyamlani ambaye kitaaluma pia ni hakimu wa Mahakama ya Wilaya
Kinondoni, alisema katika kipindi cha miaka minne ataimarisha usimamizi na
Manejimenti ya soka katika ngazi zote kwa kupitia nafasi hiyo ya urais sanjari
na kushirikiana na viongozi wa klabu na vyama vya soka vya wilaya na mikoa kwa
ujumla wake.
Alisema ataimarisha usimamiaji na menejimenti ya soka katika ngazi
zote kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi na kusimamia sheria na
taratibu za uendeshaji wa soka la Tanzania na suala la viongozi kujiendeleza kielimu litapewa kipaumbele na
litakuwa ni agenda endelevu.
Nyamlani alisema suala lingine ambalo litakuwa katika utekeleza wake
ni rushwa katika soka nchini.
“Naomba nikiri kuwa kumekuwa na malalamiko na vitendo vya rushwa
ambavyo vinawahusisha viongozi wa soka. Hivyo basi kwa kushirikiana na serikali
na viongozi wa soka katika ngazi zote nitahakikisha naendeleza mapambano dhidi
ya rushwa,” alisema Nyamlani.
Kipaumbele cha tatu kitakuwa ni kukuza soka la watoto, vijana na
wanawake, akiwa kama Rais wa TFF, atalipa uzito wa kipekee soka la watoto wenye
umri wa miaka chini ya 16 na soka la vijana na kukuza vipaji kuanzia miaka tisa
hadi 12, 13-14, 15-17 na 18-21 na soka ya wanawake.
Nyamlani alisema kazi hiyo ataitekeleza kwa kuanzisha program mbali
za mashindano na za kukuza vipaji kwa makundi haya ya vijana kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali wa soka.
Kwa sababu kubwa ya kufanya hivyo ni ukweli kwamba haya makundi
ambayo yameonesha uwezo yatatoa mwanga jambo ambalo uongozi uliopita ulilifanya
na alihaahidi kuendeleza kulitekeleza kwa kushirikiana na viongozi wa soka
katika nagzi mbalimbali na serikali.
Kipumbele kingine muhimu ni Kuimarisha Uwezo wa Rasilimali Fedha wa
Shirikisho, kama Rais wa TFF atahakikisha kuwa TFF inapata vyanzo endelevu na
vya kuaminika ili kuweza kujenga uwezo wa shirikisho katika kutekeleza mipango
kikamilifu.
Nyamlani alisema ataimarisha idara ya masoko ili kuweza kupata
wadhamini zaidi na kuweza kuuza nembo za shirikisho.
Alisema kipaumbele kingine ni Kuongeza Idadi na Ubora Waamuzi,
Walimu wa soka na Wataalamu wa Afya ya Michezo.
Nyamlani alisema atahakikisha kunakuwa na program endelevu ya
mafunzo kwa makocha, waamuzi wa soka nchini na wataalamu wa afya ya michezo ili
kuongeza ufanisi wao katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na
taratibu zinazoongoza michezo wa soka, pia kufikia viwango vya kimataifa vilivywekwa
na Caf na Fifa.
Kipaumbele cha sita ni Kuongeza Ubora wa Ligi Kuu, Ligi Daraja la
Kwanza, Ligi za wilaya na mikoa, mashindano ya Ligi daraja la 1, ligi za
wilaya, mikoa na Ligi Kuu ni ngazi muhimu ya kukuza soka katika nchi.
Nyamlani alisema atashirikiana na viongozi wa soka na vyama vya
kitaalamu ili kuweza kuboresha kanuni mbalimbali zitakazowawezesha wachezaji
vijana kuwa wachezaji wa kulipwa.
Alitaja kipaumbele kingine ni Kuongeza Idadi ya Mawakala wa
Wachezaji ambao ni Watanzania, kama Rais wa TFF ana imani kwamba ili soka la
Tanzania likue kwa kasi ni lazima ataongeza idadi ya wachezaji na mawakala
wanaozingatia weledi.
Alisema ataimarisha
Ushirikiano wa TFF na Serikali, kama rais wa TFF atahakikisha anakuza na
kuendeleza mahusiano mazuri kati ya TFF na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa imani kwamba ni jambo hilo ni
muhimu kwa ustawi wa soka kwa sababu ni ukweli soka sasa ni ajira kwa
vijana ambao ni nguzo ya Taifa.
Kipaumbele cha tisa ni Kuimarisha Ushirikiano wa TFF, Caf na Fifa,
atahakikisha kuwa anakuza na kuendeleza mahusiano kati ya vyombo hivyo ili
kuongeza kasi ya ukuaji wa soka nchini, kufikia viwango vya kimataifa kwa
kutumia misaada mbalimbali ya kitaalamu na kifedha inayotolewa na Taasisi hizo
kubwa duniani.
No comments:
Post a Comment