Na Oscar Assenga, Muheza.
MKUU wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa ameziagiza
Halmashauri zote mkoani hapa kuelekeza msukumo mkubwa kwenye ujenzi wa maabara
tatu kila shule ili kuwawezesha wanafunzi kupenda kusoma masomo ya sayansi na
kuweza kufanya vizuri.
Gallawa ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea
shule ya seminari ya wavulana ya Livingstone iliyopo wilayani hapa pamoja na
kuzindua jengo la maabara ya kompyuta iliyojengwa kwa thamani y ash. 149,000,000
ikiwemo ununuzi wa vifaa vya ndani.
Amesema ujenzi huo wa maabara kwa vyumba vitatu kila
shule ni agizo la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania,Dokta Jakaya Mrisho
Kikwete hivyo kuzitaka halmashauri hizo kutilia mkazo suala hilo kwenye maeneo
yao.
Ameongeza kuwa maabara hizo zinapaswa kuwepo kwenye
shule za sekondari kuanzia za kata na zile za binafsi kwani hakuna maendeleo
yanayoweza kupatikana bila ya kuwepo wanasayansi.
Aidha amesema katika hilo inabidi itumike nguvu
kubwa ikiwemo hata kuhairisha miradi mengine ili kuzielekeza kwenye ujenzi wa
maabara kwenye shule hizo.
"Halmashauri zote zinatakiwa kujenga maabara tatu tatu kila shule na sio
mbili kwani hilo ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Jakaya
Mrisho Kikwete.
Amezitaka halmashauri kupitia ofisa elimu kupita
kwenye shule za binafsi kuwasisitizia suala hilo la ujenzi wa maabara kwani ni
muhimu sana hasa kwenye maendeleo ya nchi yetu.
Mkuu huyo wa mkoa ameziagiza pia shule za sekondari
na msingi mkoani hapa kupanda zao la mkonge kwenye mipaka yao ili kuwezesha
wanafunzi kufundishwa jinsi ya kupanda zao hilo.
No comments:
Post a Comment