Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SITAKI kusikia nani ameshinda nafasi za Uchaguzi Mkuu wa
Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwakuwa kuna uwezekano mkubwa uwapo wa mabwana
wakubwa hao ukawa kazi bure.
Kikosi cha Twiga Stars
Siku zote wamekuwa wakitogotea pale pale. Mawazo au juhudi za
kuokoa soka letu huwa zinaishia hewani. Ingawa kwa siku za hivi karibuni soka
linaonekana kufika mbali, ila upande wa wanawake hakuna kitu.
Kila siku ya Mungu kilio kinakuwa kile kile. Wasichana ambao
ndio wahusika wakuu wanaocheza mpira huo, wanaishia kulalama wakiangalia jinsi
wanavyosuswa.
Kama hivyo ndivyo, kwanini nibabaike na majina ya wagombea wa
TFF, katika Uchaguzi uliofanyika jana Jumapili? Nasema hivyo kwasababu juhudi
nyingi zinaishia njiani.
Tumebakia watu wa siasa. Tunapenda sana kuzungumza mdomoni
wakati vitendo vyetu vina matege. Ndio maana naona tunadanganyana tu,kwani nani
anajali kuona soka letu linaanguka?
Nimefanikiwa kuzungumza na wachezaji mpira wa miguu wanawake
kwa nyakati kadhaa na kuona jinsi wanavyolalamika. Hata maisha yao ya baadaye
hawajui wataishi vipi.
Wengi wanaingia kwenye soka lakini hakuna mashindano yoyote
yenye nguvu kiasi cha kukuza uwezo wao. Hakuna ligi yoyote inayoashiria kuwa ni
njia ya kukuza soka letu.
Nini hatma ya maisha yao? Wanacheza mpira ili wapate nini?
Nani wa kuwainua kiuchumi, kama ajira yao inatia mashaka? Ni tofauti na soka la
wanaume, ambao tunasikia wanavyovuna utajiri mkubwa mno.
Leo tunashuhudia jinsi Mrisho Ngassa anavyoweza kuvuna fedha
nyingi, wakati mwenzake Sophia Mwasikili hana anachopata.
Timu ya Taifa, Taifa Stars inalala hoteli ya nyota tatu hadi
nne wanapoweka kambi yao, lakini ndugu zangu wa Twiga Stars wananyang’anyana
maji ya kunywa.
Wadhamini wanapigana vikumbo Taifa Stars, lakini Twiga wao
wanabembeleza bila mafanikio. Hii ni laana. Na ni unafiki uliopitiliza.
Na ndio maana siwezi kuvumilia hadi nichekee Uchaguzi wa TFF
usiokuwa na dhamira, kama waliochaguliwa watapita njia ile ile iliyotufikisha
hapa.
Jambo jema ni kutambua makosa yetu. Sitaki kuamini kwamba
wadau wa soka, wakiwamo TFF wenyewe kama wamejitambua.
Mara kadhaa TFF wanachojua wao ni kuandaa mechi kubwa zenye
kugusa watu wengi na sio kuboresha ligi zinazoweza kutoa wachezaji mahiri.
Mpira unalipa mno. Tukiwa makini, kila anayejihusisha nao kwa
asilimia zote basi lazima anufaike nao. Ukiacha sasa wanaonufaika ni viongozi
wanaofikia kugawana mapato ya milangoni.
Najua ni mapema kuanza kulaumu juu ya nani ametangazwa jana
kuwa mshindi wa nafasi ya Urais wa TFF au makamu wa Rais, ila kwasababu
watendaji wapo ndani ya Shirikisho hilo, bado hawawezi kukwepa lawama zangu.
Ni ukweli huu japo ukiusema wadau baadhi yao wanakataa kwa
kudhani labda tuna ajenda za siri juu ya viongozi hao. Tusipokuwa makini,
tutaishia kupiga porojo kila siku ya Mungu.
Wenzetu wanasonga mbele, sisi tunaishia kupiga soga katika
vijiwe vya kahawa, jambo ambalo kamwe haliwezi kuwa mkombozi wa soka letu.
Hakika siwezi kuvumilia. Tunapaswa kuzinduka, hasa kwa
kuandaa ligi za wanawake, ligi daraja la kwanza yenye nguvu pamoja na
mashindano mbalimbali ya vijana katika mikoa ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Huu ndio ukweli wa mambo. Kinyume cha hapo, tutaishia kuwa
wajuaji wa kupiga kampeni za uchaguzi, kutoa ahadi za uongo zisizotekelezwa kwa
vitendo na kutufanya tuwe kama majuha.
Kwanini? Nadhani huu ni wakati wa kuangalia nyendo zetu na
kukumbusha safu mpya ya uongozi iliyopatikana jana katika Uchaguzi wa TFF.
Mungu ibariki Tanzania.
+255712053949
No comments:
Post a Comment