Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA hali ya isiyokuwa ya kawaida,
uongozi wa klabu ya Simba, umewapiga marufuku benchi la ufundi na wachezaji
kuzungumza chochote katika kuelekea mechi yao na Yanga, inayotarajiwa kupigwa kesho
Jumapili, katika Uwanja wa Taifa.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.
Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu
imezidi kuleta msuguano, huku upande wa makocha ukitangaza hali ya hatari ya
kujiziba mdomo, badala yake jukumu la kuzungumza litabaki kwa viongozi wao.
Kwa wiki moja sasa, kumekuwa na siri
kubwa katika mazoezi ya Simba yanayofanyika Bamba Beach walipoweka kambi kwa
ajili ya kuwavaa watani wao Yanga.
Akizungumza mapema jana asubuhi,
kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo Julio, alisema kuwa benchi la ufundi
halitaweza kuzungumza chochote isipokuwa viongozi wao, akiwamo msemaji wa timu,
Ezekiel Kamwaga.
Alisema huo ni utaratibu
uliopitishwa na kocha wao, King Abdallah Kibadeni, huku akiamini kuwa ni mzuri
kwa ajili ya kuleta umoja na nguvu ya kukipiga na Yanga.
“Kila kunapokuja yoyote anayehitaji
kujua chochote anapaswa kuzungumza na viongozi, akiwamo Kamwaga ambaye ndio
msemaji wa timu ya Simba.
“Hali hii imepitishwa na kocha wetu
na sisi tumekubaliana kwa pamoja, hivyo sisi makocha tutafikisha ripoti na
maendeleo ya kambi yetu na kama kutakuwa na lolote waandishi watalipata huko,”
alisema Julio.
Uchunguzi uliofanywa jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa ajili ya kuficha siri zinazoweza
kutoka kwa makocha hao kusema kinachoendelea ndani ya kambi yao.
Uchunguzi huo unaonyesha kuwa uamuzi
huo umetolewa na viongozi wa klabu ya Simba kwa ajili ya kuwaziba mdomo makocha
wao na wachezaji juu ya kuelekea kwenye mchezo huo.
Juzi Kamwaga alisema kuwa jopo la viongozi wa Simba litatembelea katika kambi ya timu yao kwa
ajili ya kuzungumza na wachezaji wao ili kubaini matatizo yao kabla ya kuvaana
na Yanga, mechi yenye msisimko wa aina yake.
No comments:
Post a Comment