Na Jonathan Tito, Dar es Salaam
KWA wadau wa muziki wa Bongo Fleva,
watakuwa wameusikia vizuri wimbo mpya wa Elibariki Emanuel ‘Ney wa Mitego’ na
kuutafakari kwa kina.
Madame Rita, Mkurugenzi wa Benchmark Production ambao ndio waratibu wa shindano la Bongo Star Search Tanzania.
Katika mashairi ya wimbo huo uitwao ‘Salamu
Zao’, msanii huyo amezungumza mengi akitaka salamu zake zifikishwe kwa watu
mbalimbali.
Ney alimtaka Diamond afikishe ujumbe
wake kwa Zitto Kabwe, amwambie aachane na Bongo Fleva, aendelee na siasa, maana
Kigoma Stars amewatelekeza.
Salamu nyingine ni kwa Madam Rita
Paulsen, zikihusu ‘kufulia’ kwa washindi wa shindano la Bongo Star Search
(BSS).
Pia Ney alizungumza na Ridhiwani
akimtaka amueleze baba yake, Rais Jakaya Kikwete kwamba masela hawamuelewi na
Wamakonde wa Mtwara hawataki tena korosho, bali gesi na anaweza kuwaua kwa
mkong’oto.
Mwandishi wa makala haya, Jonathan Tito. Ni mtazamo wake binafsi, si msimamo wa Mtandao huu wa Handeni Kwetu Blog.
Ney alikwenda mbali na kumtafuta
rafiki wa Edward Lowasa ili amfikishie salamu kuwa anamtaka agombee urais 2015,
akiahidi kumpigia kampeni.
Chakushangaza anataka salamu
nyingine zifikishwe hadi kwa marehemu Steven Kanumba na Albert Mangwear, kwamba
atakayetangulia kufa akawambie wasanii hao kuwa wakati wa misiba yao kuna watu
waliiba fedha za rambirambi.
Naamini salamu zote zitakuwa
zimefikishwa kwa wahusika, hata zile za Kanumba na Ngwear, huenda ikawa Mack 2B
aliyefariki mwezi uliopita, akawa ameshazifikisha.
Jukumu la kumfikishia salamu Mkurugenzi
Benchmark Production, Madam Ritha, mwandaaji na mratibu wa shindano la BSS,
alipewa mshindi wa mwaka jana wa shindano hilo, Walter Chilambo.
Lakini, hakuna ubaya wengine tukajaribu
kuzifikisha kwa Madam, tena kwa maandishi.
BSS, imekuwa ikifanyika kila mwaka
washindi wakipewa fedha taslimu kila mwisho wa shindano.
Lakini Ney na wadau wengine wana
wasiwasi kama kweli washindi hao wanapewa fedha kutokana na washindi hao
kutokuwa na tofauti kimuziki au kimaisha pamoja fedha hizo.
Mshindi wa kwanza wa shindano hilo lililofanyika
mwaka 2007, Jumanne Iddi, ninaweza kumuondoa kwenye mlonongo huu wa washindi ‘waliofulia’.
Yeye alikabidhiwa gari, lililodaiwa
kuwa na thamani ya shilingi milioni 10.
Mshindi wa mwaka 2008, Misoji
Nkwabi, hakuna anayejua yuko wapi kwa sasa na hatujawahi kusikia hata wimbo
wake mmoja ukifanya vizuri kwenye redio, wala hatuna taarifa kuwa aliwahi
kualikwa kwenye onyesho lolote.
Paschal Casian, mshindi wa mwaka
2009 aliyepewa Shilingi milioni 30, pamoja na uwezo mkubwa wa kuimba,
ameshindwa kutamba kabisa kwenye muziki.
Hilo linalompa hofu Ney na wadau
wengine wa muziki. Iweje mwimbaji mzuri, ashinde BSS, apate mamilioni ya fedha,
lakini asiwe na maisha mazuri na hata kwenye muziki asifanye vizuri?
Je wanaridhika na fedha wanazopata
na kuamua kuachana na muziki au ni kitu gani kinatokea? Fedha wanazopewa zinatosha
kujiendeleza kisanii, lakini wengi wao wanashindwa kutamba.
Baada ya Paschal, mwaka 2010
alishinda Mariam Mohamedi ‘Mariamu BSS’ akaondoka na Shilingi milioni 30,
lakini hajang’ara kwenye fani na kuishia akihangaika kwenye bendi za taarabu.
Mariamu na Paschal wana maelezo ya
kufanana, kila mmoja akidai kununua nyumba. Ni kweli?
Kama kweli Mariamu alinunua nyumba, kwanini
aishi kwenye nyumba ya kupanga Mabibo, tena isiyo na hadhi ya mshindi wa BSS?
Huenda nyumba yake kapangisha,
lakini kwanini anaonekana kuwa na maisha magumu. Kwa sasa anajipatia riziki kutoka
bendi ya Five Star.
Kama kweli walipewa milioni 30, wangeweza
kutayarisha albamu zao na fedha zilizobaki wangefanya biashara nyingine na maisha
yao yangekuwa mazuri.
Kuna taarifa kuwa Paschal
ametayarisha albamu ya muziki wa Injili, lakini hakuna hata wimbo mpya unaofanya
vizuri katika redio za dini, huku Mariam hajarekodi wimbo hata mmoja wa taarabu!
Mwaka 2011 mshindi alikuwa Haji
Ramadhani, ambaye Ney anasema yuko ‘kitaani’ amechoka.
Ingawa Haji hajachoka mtaani, lakini
maisha yake hayatokani na fedha za ushindi kwani wakati wa fainali hiyo
alitunzwa fedha nyingi sana.
Ndio maana amenunua gari ya
kutembelea na anamudu kupata fedha ya kuweka mafuta kwa kuwa anafanya kazi
Twanga Pepeta, ukichanganya na anacholipwa na kutunzwa na mashabiki wa bendi hiyo,
maisha yake ni tofauti na washindi wengine wa BSS.
Walter, mshindi wa mwaka jana,
hajafikisha hata mwaka, lakini kwa mujibu wa Ney, amepigika na hilo linaweza kuwa
kweli kwani kila siku husema kwamba fedha zake ziko benki huku mama yake akiishi
nyumba ya kupanga eneo la Forest ya zamani mjini Mbeya!
Walter ameonyesha uhai na nyimbo
zake zinafanya vizuri na angekuwa na fedha za kutosha, angekuwa juu zaidi
kimuziki kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuimba.
Kila baada ya shindano, washindi
wamekuwa na porojo za hapa na pale, kila mmoja akijifanya kuelezea matumizi ya
fedha alizopata, lakini baada ya muda unamuona anaendelea na maisha yale yale
ya zamani.
Hapo ndipo Ney anauliza, hizo fedha
zinakwenda kwa nani? Hii si hoja ya kupuuziwa! Inastahili majibu stahiki.
Isije ikawa kuna watu wanafaidika
kwa kupitia shindano hilo na kuwatosa wasanii!
Madam Rita amekuwa akidai kuwaibua
wasanii na sasa wamejiunga bendi mbalimbali, bila kujua kuwa walikuwapo huku
hata kabla ya kwenda BSS.
Afike mahali aanze kuwasaidia hao
washindi kufikia malengo yao kisanii.
Ikiwezekana basi, kabla ya kuwapa
fedha wapewe kwenza elimu ya ujasiriamali au kama fedha haziwasaidii, ipo haja
ya kubadili zawadi kwa washindi.
La sivyo, wadau wataendela kuwa na
hofu kuwa kuna ‘magumashi’.
Wakati wasanii wakisota, hali
kimaisha kwa ‘wakubwa’, Madam Rita, Master Jay na Salma Jabir ni tofauti
kabisa, wao wanazidi kung’ara tu.
Master Jay, anaendelea kuajiri watu
kwenye ofisi yake, huku mwenyewe akiendelea na ‘ofisi kubwa’, BSS.
Tulisikia Salma alienda kusoma
Afrika Kusini, lakini msimu wa mwaka juzi wa BSS ulipokaribia, alirejea kuja
kuwa jaji huku akizuga na kipindi chake cha runinga cha Mkasi ambacho
hakijawahi kumuhoji hata mshindi mmoja wa BSS kuzungumzania mafanikio yake.
Master Jay naye hajamsaidia ‘kutoka’
hata mshiriki mmoja wa BSS kwenye studio yake walau kuonyesha kweli wamelenga
kuinua vipaji wao na bosi wao.
Sawa, inawezekana wanaibua vipaji, lakini
tujiulize, Diamond, Rich Mavoko, Ommy Dimpoz na wengine, wamepata majina na
mafanikio wakitokea BSS?
Hizi ni salamu tu za Ney wa Mitego
kwa Madam Rita, nimetumika kama njia rahisi ya mawasiliano na ninatarajia
mshindi wa mwaka huu atajengewa misingi bora kimaisha na kimuziki.
No comments:
Post a Comment