Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MBUNGE wa Bukoba
vijijini, Jasson Rweikiza, ameitaka serikali kuangalia upya utaratibu wa
utoaji vibali kwa walimu kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki.
Rweikiza alitoa
ombi hilo juzi, kwenye mahafal ya tatu ya kidato cha nne, shule ya
sekondari Brilliant, iliyopo Mbezi kwa Msuguri jijini Dar es Salaam,
ambapo mgeni rasmi alikuwa ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Alisema Tanzania
ina upungufu wa walimu zaidi ya 130,000, lakini shule binafsi haziwezi
kuagiza kutokana na urasimu na gharama kubwa za kibali cha kazi.
"Nchi ina uhaba
wa walimu, lakini wenzetu Kenya na Uganda wana idadi kubwa ya walimu
kuliko mahitaji, sasa unapoagiza mwalimu kutoka nchi hizo, kuna urasimu
mkubwa wa kupata kibali, na kikitoka hiyo gharama yake, utajuta,"
aliongeza Rweikiza ambaye ni mmiliki wa shule hiyo.
Alisema pamoja na
mambo mengi kuchangia matokeo mabaya kwa wanafunzi, lakini ukosefu wa
walimu ni sababu kubwa zaidi inayochangia matokeo hayo mabovu.
Aliitaka serikali kuruhusu walimu kutoka nchi hizo kuja kufundisha na nchi itakapojitosheleza basi waondoke.
Naye mbunge wa
Karagwe, Gosbert Blandes ambaye alikuwa ameambatana na Ngeleja, alisema
watalipigia kelele suala hilo pindi wakifika bungeni.
"Wenye mapenzi mema na taifa, tusukume jambo hili lifanikiwe ili kunusuru elimu,"alisema.
Ngeleja akijibu hoja hizo kwa majumuisho alisema watapigia debe uingiliano huru wa kazi kwa nchi za Afrika Mashariki
Aliahidi kutoa
mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kumpa nguvu Rweikiza katika
kukamilisha ujenzi wa shule, kwani uwekezaji kwenye elimu haumsaidii
yeye na familia yake tu bali taifa zima.
Ngeleja aliahidi
pia kwenda kuzungumza na Waziri wa Ujenzi, ili kushughulikia tatizo la
ubovu wa barabara zinazoingia shuleni hapo na nyingine zaidi ya sita
zinazozunguka eneo hilo.
No comments:
Post a Comment