Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
BAADA ya
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali nchini (PAC), Zitto Kabwe, ambaye
pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alipotoa hoja juu ya vyama vya siasa kutokaguliwa,
mengi yalisikika.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pichani.
Hasa ni pale
viongozi wa vyama vya siasa nchini kutumia muda mwingi katika vyombo vya habari
kukanusha na wengine kufika mbali kusema kuwa Zitto anapenda kujenga matukio
ili kuweka juu jina lake.
Mwenyekiti wa Chadema Arusha aliyesimamishwa, Samson Mwigamba, pichani.
Kwa wale
tunaomfuatilia Zitto kwa karibu tukagundua kuwa kuna kitu ndani yake na
kingetokea mapema iwezekanavyo. Ikumbukwe kuwa, Zitto mbali na kuwa mwenyekiti
wa PAC, pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Kama kweli
vyama siasa havijakaguliwa hususan Chadema, yeye pia yupo ndani ya chama hicho.
Je, hoja yake zaidi ilitokakana na kutaka kuinyuka Chadema?
Najikuta
najiuliza maswali hayo baada ya Chadema kumsimamisha Mwenyekiti wa mkoa wa
Arusha, Samson Mwigamba, kwa madai kuwa ametoa siri za chama chao hadharani.
Siri? Ni
siri gani hizo zinazofichwa kiasi cha kuwataka watu wengine wa nje wasijuwe?
Inashangaza mno. Ukijaribu kufuatilia suala hilo na kauli ya Zitto juu ya
mahesabu ya vyama vya siasa yanafanana.
Mwigamba
amemtuhumu Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake Dk Willbroad
Slaa juu ya mahesabu na matumizi yote ndani ya chama hicho.
Anafika
mbali zaidi kwa kusema kuwa kipengele cha ukomo katika Katiba yao kimeondolewa
kwasababu za watu wachache, akiwamo Mbowe na kundi lake.
Aidha anasema
pia fedha nyingi zinachotwa bila kufuata utaratibu, jambo linaloashilia uwapo
wa ufisadi usioweza kuvumiliwa na wanaokitakia kheri chama chao.
Inawezekana
kuwa ni uongo, lakini ni vyema pia viongozi walioguswa wasimame na kutoa tamko.
Lakini kumsimamisha Mwigamba bila kuelezea juu ya sakata lake ni kumuonea.
Yote
anayosema Mwigamba, ni kuonyesha mapenzi ya dhati kwa chama kinachovuna ruzuku
ya Watanzania, hivyo lazima kiendeshwe bila ubabaishaji.
Kwa mfano,
Chadema ndio chama kinachojipambanua kuupinga ufisadi, hivyo nao lazima wawe
wasafi. Mbowe anatajwa pia kuchota Milioni 80 kwa ajili ya kutengenezea kadi za
chama hicho, jambo ambalo halijafanikiwa hadi muda huu.
Hata kama
lingefanikiwa kupatikana kwa kadi hizo, lakini haikuhitaji kauli ya mtu mmoja
kutoa amri na kupewa fedha hizo. Kwani sheria za manunuzi katika chama hiki
zikoje?
Kuyasema
haya kwa kipindi hiki ambacho baadhi yao wanaona Chadema ndio mkombozi wao
kunahitaji moyo wa chuma kupita kiasi, ukizingatia kuwa wanaweza wakakuona
unakichukia.
Mara kadhaa
watu hao hawataki ukweli. Wakielekezwa jambo wanaona wanasemwa na eti
hawastahili kukosolewa hata kidogo. Hii sio haki kwa Chadema kinachoongozwa na
binadamu.
Chadema
hakiongozwi na malaika. Nao ni binadamu, hivyo kukosea kwao ni jambo la
kawaida, hivyo inapotokea wanashauriwa basi hakuna haja ya kuchukia.
Ni kweli
Chadema ni chama kilichopata umaarufu miongoni mwa Watanzania kiasi cha kuwa
chama Kikuu cha upinzani kwa sasa, kikiipoka nafasi hiyo Chama Cha Wananchi
(CUF).
Angalia,
kama leo chama kama Chadema hakuna mtu anayejua hivi fedha za chama
zinatumikaje zaidi ya watu wachache, yani Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu na
Mkurugenzi wa Fedha, unafikiri nini hatima yake?
Kama
maamuzi ya vikao hayaheshimiki isipokuwa ya wale watu wachache, ni mwelekeo mzuri
kwa chama hicho cha upinzani? Ifahamike kuwa Chadema wana vuna fedha nyingi za
rukuzu, ndio maana tulishuhudia wanavyopiga kelele baada ya kuitwa kwenye
Kamati ya Hesabu za Serikali, PAC, chini ya Zitto.
Mwigamba
anasema; “baada ya uchaguzi wa 2010 vikao halali vilielekeza kiasi na aina ya
fedha ambazo hazitaguswa bali zitunzwe kwenye akaunti maalum kwa ajili ya
uchaguzi wa 2015, lakini leo si tu akaunti hiyo haina fedha bali hakuna akaunti
yoyote yenye fedha.
“Watu
watatu ndo wanaamua fedha zitumikeje, pamoja na maamuzi ya kikao cha Baraza kuu
cha mwezi Januari kilichoamua kwamba kiasi cha fedha inayotoka serikalini
kipelekwe kwenye mikoa, wilaya na majimbo na kiasi kingine kipelekwe kwenye
kanda, ingawa sasa ni mwezi wa 10 maamuzi hayo hayajatekelezwa ipasavyo.”
Ilisema taarifa hiyo ambayo hata hivyo ilikuwa ngumu baada ya kusimamishwa.
Nafikiria
Chadema wanajidanganya katika suala hili kwakuona kuwa wakimsimamisha Mwigamba
ndio njia ya kutuliza moto huu ulioanza kufukuta. Najua ndio hatua hii ni sababu
ya mvutano wa nafasi za uongozi za Chadema.
Lakini
njia ni kukaa chini na kuangalia lipi tatizo. Uwekwe mfumo mzuri wa kiutawala
kwa chama hicho kinachojiona ni kisafi. Chama kinachoona kinastahili kushika
dola na kuwaongoza Watanzania.
Inashangaza
kuona mambo mabaya kama haya yakiendelea kutokea ndani ya Chadema. Hii inaweza
kuchukukuliwa kama tahadhari kwa ajili ya kukijenga na kukiimarisha zaidi. Ni
juzi tu wanachama wawili waliondoka, akiwamo Juliana Shonza na Mtela Mwampamba
ambao wote kwa pamoja walikimbilia kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa
wanaofuatilia mambo ya siasa wanakubaliana na mimi kuwa kuondoka kwa wanachama
hao na maneno waliyokuwa wanayatoa yanajibu hoja juu ya Chadema kuendeshwa na
kikundi cha watatu wasiozidi watatu.
Japo unaweza kuona ni masihala,
lakini kwa chama kama Chadema, Chama Kikuu cha Upinzani, kuondoa kipengele cha
kinachomzuia kiongozi kukaa madarakani kwenye nafasi moja zaidi ya vipindi
viwili vya miaka mitano mitano.
Hii ni kwa mujibu wa tamko la
Mwigamba, ambapo alisisitiza kuwa wakati wanafanya mabadiliko ya katiba mwaka
2006 hawakugusa kipengele hicho, hivyo wakati Katiba hiyo inachapwa chini ya
uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela.
Nadhani hapa kuna haja ya
kuliangalia kwa kina jambo hili. Halipaswi lipite hivi hivi. Kama Chadema
wamekuwa wakipigia kelele ufisadi wa viongozi wengine hasa waliokuwa ndani ya
serikali ya CCM, hata wao wanapaswa kunyooshewa vidole.
Na ndio maana wameona njia muafaka
kwao ni kumsimamisha Mwigamba, wakisema ametoa siri, hali ya kuwa hawataki
kilichopo ndani ya chama chao kionekane nje kwasababu za heshima ya chama chao.
Hiki si kitendo kidogo hata kidogo.
Kinapaswa kuchunguzwa kwa kina, na endapo kitaonekana ni kweli, basi viongozi
wa juu wa Chadema, akiwamo Mbowe, Slaa wanapaswa kujiuzuru kwa heshima ya kodi
za Watanzania.
Pamoja na kujiuzuru huko, pia ni
wakati wa Watanzania wote kukipiga jicho chama hiki kinachopigana usiku na
mchana ili kishike dola. Huu ndio ukweli wa mambo. Unapaswa kuangaliwa kwa
kina.
Bila kuangalia hisia juu ya chama
hiki, ila ni dhahiri kuwa kuna siku viongozi hao hao wanaweza kufanya mambo
mabaya zaidi, ukizingatia kuwa wanaonekana ndio wenye sauti na hawawezi
kukoselewa na mtu yoyote.
Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya
siasa, kadhia hii na mvutano huu unasababishwa na joto la wanaohitaji nafasi
hizo, hasa ya uenyekiti ambapo Mbowe sasa amejihalalishia kuongoza hadi
atakapotaka mwenyewe, ukizingatia kuwa kipengele hicho kwenye katiba yao hakipo
baada ya kuchomolewa kienyeji.
Kuondolewa kwa kipengele hicho
ndicho kinacholeta mpasuko kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania
uenyekiti na kama ni kweli basi sakata hili ni zaidi ya udikteta, hivyo wenye
chama chao lazima wahoji.
Mimi ni miongoni mwa Watanzania
wanaopenda kuhoji mambo mbalimbali ya vyama vya siasa, wakiwamo Chadema. Japo
wakati mwingine napata wakati mgumu, lakini ukweli unaonekana wazi wazi juu ya
mwenendo huu mbaya.
Ni vyema
viongozi wa Chadema wakajibu hoja hizi ili kutuliza mawazo na mfadhaiko juu ya
wanachama wao na wafuasi wao.
Mungu
ibariki Tanzania.
+255712053949
No comments:
Post a Comment