Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KOCHA wa masumbwi wilayani Muheza, mkoani Tanga,
Charles Muhiru, amemwita bondia Fransic Cheka ili aende kuhamasisha mchezo huo
wilayani humo.
Bondia Francis Cheka, pichani.
Cheka atakuwa wilayani humo ambapo pia kutakuwa
na mapambano kadhaa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa uwapo wake unakuwa na chachu
kwenye ngumi.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka wilayani
humo, Muhiru alisema kuwa Cheka ni miongoni mwa mabondia makini wenye uwezo wa
aina yake hapa nchini.
Alisema jambo hilo linamfanya amualike
mwanasumbwi huyo ili kuleta picha kamili kwa wadau wa ngumi na wenye hamu ya
kuona mchezo huo unasonga mbele.
“Tumepanga Cheka awepo hapa kwenye Sikukuu ya
Idd Pili katika viwanja vya Jitegemee, wilayani Muheza, mkoani Tanga ambapo
siku hiyo kutakuwa na mapambano ya ngumi na yeye kuhamasisha.
“Naamini mpango huu utakuwa na tija kwa kiasi
kikubwa kwa sekta ya masumbwi mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla, hivyo kila
kitu kitakwenda sawa,” alisema.
Sio mara ya kwanza kwa Cheka kukaribishwa katika
sehemu mbalimbali za Tanzania, ikiwamo katika Ukumbi wa Bunge Mjini Dodoma,
ikiwa ni njia ya kuthamini mchango wake katika tasnia ya masumbwi.
No comments:
Post a Comment