Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akiangalia bidhaa mbalimbali
zinazotengenezwa na akinamama wa kikundi cha Jitegemee wakati wa
maonyesho yaliyofanyika mjono Njombe kwa ajili ya sherehe za uzinduzi
rasmi wa mkoa wa Njombe huku kiongozi wa kikundi hicho Mama Leokadia
Kaduma akimfafanulia juu ya bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na
wanakikundi hao.
Na Anna Nkinda – Maelezo, Njombe
TAASISI ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imeahidi kukipatia kituo cha afya
Lupembe na Hospitali ya Makambako iliyopo wilayani Njombe vitanda vya
kujifungulia kina mama wajawazito viwili ili kupunguza tatizo la vifo
vyao na watoto wachanga vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo
alitoa ahadi hiyo jana mara baada ya kupokea ombi la Mbunge wa jimbo la
Njombe Kaskazini Deo Sanga kwa taasisi ya WAMA ili iweze kuwasaidia kina
mama wanaopata huduma katika hospitali hizo vitanda viwili vya
kujifungulia.
Akiongea
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Wanginyi
kata ya Lupembe wilaya ya Njombe katika mkoa mpya wa Njombe Mama
Kikwete alisema jitihada za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha kuwa
vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyotokea wakati wa
kujifungua vinapungua hapa nchini.
“Nimekubali
ombi la Mbunge wenu na ninawaahidi nitawapatia vitanda viwili vya
kujifungulia kina mama wajawazito kama alivyoniomba, mimi ninataka kina
mama hawa wajifungue katika mazingira salama ili vifo vyao na vya
watoto wachanga vipungue”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema takwimu zinaonyesha kuwa miaka mitatu iliyopita
tatizo la vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano lilikuwa juu
kwani walikuwa wanakufa watoto 578 kwa kila vizazi hai 100000 lakini
hivi sasa tatizo limepungua na kufikia vifo 454 kwa kila vizazi hai
100000
hii ni kuonyesha kuwa uongozi wa Serikali ya awamu ya nne unafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa tatizo hili linapungua.
Mama
Kikwete pia aliwataka wakazi wa mkoa huo kujikinga na ugonjwa wa
Ukimwi kwani maambukizi yako juu kwa asilimia 14.8 ukilinganisha na
maambukizi ya kitaifa ambayo ni asilimia 5.1 na kusisitiza kuwa hali
hiyo haikubaliki hivyo basi kila mtu achukue hatua kwani Tanzania bila
Ukimwi inawezekana.
Taarifa
ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika mkoa huo inaonyesha
kuna jumla ya Hospitali 11, vituo vya afya 21 na zahanati 190
zinazomilikiwa na Serikali, Taasisi za dini na watu binafsi huku idadi
ya wakazi ikiwa ni 702,097 kati ya hao wanaume ni 329,359 na wanawake
ni 372,728.
Mama
Kikwete ameambatana na mmewe Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete katika
ziara ya kikazi ya siku saba mkoani humo ambapo jana Rais Kikwete
amezindua mkoa mpya wa Njombe, amezindua kiwanda cha chai cha Ikanga
na kuongea na wananchi wa wilaya ya Njombe.
No comments:
Post a Comment