Na Mwandishi Wetu, Morogoro
TAASISI ya
Kifedha ya Bayport Financial Services inayojihusisha na mikopo imekabidhi
kompyuta sita kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro, kwa kupitia Mkuu wake wa Mkoa,
Mheshimiwa Dkt Stephen Kebwe, ili zisaidie utendaji kazi wa watumishi wa umma
katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya Mvomero, Manispaa ya Morogoro Mjini
pamoja na Morogoro Vijijini.
Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo mwenye miwani akifurahia jambo na Mkuu wa Mkoa Morogoro, Mheshimiwa Dkt Stephen Kebwe mwenye suti nyeusi. Kulia kwa Cheyo ni Afisa Tawala wa Mkoa Morogoro, Victor Ndiva na nyuma ni Mercy Mgongolwa, Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services.
Hapa ni Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo mwenye miwani akipiga picha ya furaha na Mkuu wa Mkoa Morogoro, Mheshimiwa Dkt Stephen Kebwe mwenye suti nyeusi. huku akiwa ameshikana mkono na Afisa Tawala wa Mkoa Morogoro, Victor Ndiva. Nyuma kwa Cheyo ni Mercy Mgongolwa, Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services.
Akizungumza
katika makabidhiano hayo, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial
Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba wamejisikia furaha kufikisha vitendea
kazi hivyo kwa serikali ya mkoa wa Morogoro.
Alisema
taasisi yao inafanya kazi ya utoaji wa mikopo ya fedha taslimu kwa watumishi wa
umma na wafanyakazi wa kampuni binafsi zilizoidhinishwa pamoja na ile mikopo ya
viwanja kwa Watanzania wote, wakiwamo wajasiriamali.
“Bayport
tumejipanga kuhakikisha kwamba tunaboresha utendaji kazi wa watumishi wetu wa
umma kwenye ofisi za mikoa na wilaya, hivyo zoezi la kutoa kompyuta litakuwa
endelevu kadri tulivyoelekezwa na serikali baada ya kuwapelekea wazo letu la
kununua na kusambaza msaada huu kwao.
“Pamoja na
kutoa misaada mbalimbali ya kijamii, tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii
ya kutoa huduma bora ya mikopo kwa watumishi wa umma, ambapo kusudio letu ni
kuona wateja wetu wanajikwamua zaidi kwa kuanzisha au kuendeleza biashara zao
ili waongeze vyanzo vya kipato na kuacha kutegemea mishahara,” alisema Cheyo.
Naye Mkuu wa
Mkoa Morogoro, Dkt Kebwe, aliwashukuru Bayport kwa kujitolea kwenye jamii na kuwakabidhi
kompyuta sita ili ziwasaidie mkoani kwao, akiamini kuwa zitachangia utendaji
uliotukuka kwa watumishi wa umma.
“Tunawashukuru
Bayport kwa kuona tunastahili msaada huu mkubwa kwetu, tukiamini kuwa watumishi
wetu watafanya kazi kwa moyo ili kuhakikisha kuwa kila mtu anatimiza wajibu
wake ipasavyo kama wote tunavyokusudia,” alisema Dkt Kebwe na kuwasihi Bayport waendelee kujitoa kusaidia matatizo yanayoikabili jamii ya Morogoro na Tanzania kwa ujumla.
Kwa mujibu
wa Kebwe, Mkoa wao upo kwenye mchakato mkubwa wa kupambana na changamoto
mbalimbali zinazowakabili ili kuupatia maendeleo Mkoa wao wa Morogoro.
Mikoa na
wilaya mbalimbali za Tanzania Bara zinatarajiwa kunufaika na misaada ya
kompyuta kwa ofisi za umma kama dira na dhamira ya taasisi ya Bayport
kurahisisha utendaji kazi utakaochangia kuleta maendeleo hapa nchini.
No comments:
Post a Comment