Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Morogoro
SIKU ya Alhamisi ya Juni sita, mashabiki wa muziki Tanzania,
ilikuwa chungu na yenye kumbukumbu mbaya kwao, hasa waliposhuhudia mwili wa
mpendwa wao, Albert Mangweha (Ngwair), ukiingia katika nyumba yake ya milele.
Ngwair alizikwa katika makaburi ya Kihonda Kanisani na
kuhudhuriwa na watu wengi, mkoa mzima ukitetemeka kutokana na umati wa watu
waliokwenda kuhudhuria mazishi yake.
Ni tofauti na matarajio ya wengi, maana baadhi yao
hawakutarajia mwingiliano wa watu wengi wenye mapenzi mema na soko la muziki wa
kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva.
Waombolezaji wakitafakari jambo.
Albert Mangweha 'Ngwair', enzi za uhai wake.
Kila pande za mji wa Morogoro ulikuwa hautoshi. Kila shabiki
alihitaji walau kushhiriki kwa karibu kwenye msiba huo. Marehemu Ngwair alifariki
Jumanne iliyopita, nchini Afrika Kusini.
Msanii huyo alifia katika harakati zake za kimaisha, huku
mwenzake Mgaza Pembe M t0 The P akirudi hoi baada ya kukaa hospitalini kwa siku
kadhaa kutokana na matatizo yaliyowapata nchini humo.
Kabla ya kuelekea Morogoro, Ngwair aliagwa pia katika
Viwanja vya Leaaders Club siku ya Jumatano na kushuhudia wapenzi wa muziki
wakijitokeza kwa wingi kumuaga mpendwa wao.
Mwimbaji huyo wa Ghetto Langu, Mikasi na nyingine aliweza
kutangaza uwezo wake kwa tasnia ya Hip Hop, huku akipendwa zaidi hata na
wasanii wenzake kutokana na ushirikiano wake kwa vijana wenzake.
Mwili wa marehemu Ngwair ulifika Leaders Club saa mbili
asubuhi ambapo baada ya kumalizika kwa taratibu mbalimbali, hatimae alianza
kuagwa na wadau wake, wakiwamo wasanii.
Wa kwanza kuagwa walikuwa wasanii na kufuatiwa na viongozi,
ndugu na Watanzania wote waliokwenda viwanjanai hapo kupata fursa ya kumuaga
msanii huyo wa Hip Hop.
Mara baada ya kumalizika shughuli za kumuaga, mwili wake
ulipandishwa tena kwenye gari na kuanza safari ya mkoani Morogoro, ambapo kuna
maeneo ambayo watu walijikusanya barabarani kwa ajili ya kupata fursa ya kuona
msafara wa msiba huo.
Hata hivyo, baada ya kufika mkoani Morogoro, taratibu za
kumuaga nyumbani kwa mama yake, ziliachwa, baada ya kushuhudia makundi kwa
makundi yakikimbilia eneo la msiba, hivyo kuonyesha kuwa eneo hilo lisingeweza
kuwa salama.
Kikao cha dakika kadhaa, kilikuja na majibu kuwa mwili huo
uende kuagwa katika Uwanja wa Jamhuri, ambapo maelewano yao yalikuwa na tija,
baada ya kukubaliana juu ya suala hilo.
Asubuhi ya siku ya mazishi yake, bado nyumbani kwa mama wa
maarehemu, kulikuwa na watu wengi, hasa pale Mkuu wa Mkoa Morogoro, Joel
Bendera alipokwenda kuwapa pole wafiwa.
“Poleni sana jamani kwa msiba huu, maana umetokea wakati
bado tulikuwa tunahitaji muda wa kuendelea kukaa na ndugu yetu, Mangwair, mmoja
wa vijana mahiri katika muziki wa Hip Hop.
“Sisi sote safari ni moja, hivyo tunachopaswa kufanya ni
kumuombea dua njema msanii huyu aweze kupokelewa vyema baada ya kumaliza maisha
yake ya duniani,” alisema Bendera, akiwafiriji ndugu wa marehemu na Watanzania
kwa ujumla.
Mama wa marehemu, aliwashukuru Watanzania kwa kuonyesha
upendo kwa mtoto wake, akiamini yote ni mipango ya Mungu, ukizingatia kuwa
hakuna atakayeweza kubakia hapa chini ya jua.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina
la Sugu, aliwataka wasanii kuendelea kushirikiana sambamba na kupigania vilivyo
haki zao za msingi.
“Tusidanganyike na kuzikwa kwa mtindo huu wakati maisha yetu
ni magumu licha ya kuwa na umaarufu wa aina yake, hivyo lazima tulipiganie
suala hili kwa ajili ya maendeleo yetu.
“Wasanii wanakuwa na majina makubwa lakini hawana chochote
mfukoni zaidi ya kusubiri kuzikwa kwa staili za kila aina, ikiwamo kukusanya
Kamati za kuweka mambo sawa,” alisema Sugu.
Wakati mwili wa marehemu umefikishwa katika Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro kwa ajili ya kuaga, uwanja huo ulikuwa na watu wengi
mno, kila mmoja akiwa na hisia zake.
Hata hivyo, wapo wale waliokwenda kwa ajili ya kuangalia
wasanii wanaoingia uwanjani hapo, jambo ambalo lilidhihirika pale waombolezaji
hao, waliposhindwa kuvumilia na kujikuta wakipaza sauti zao juu na kuita majina
ya wasanii wao.
Msanii kama vile Mr Blue, Afande Sele, Madee, Lady Jay Dee,
Stamina, Chid Benz, TID na wengineo walionyesha kukubalika mno kiasi cha
kushangiliwa kila wakati.
Hata hivyo, baada ya kugundua kuwa mashabiki hao waliokwenda
kumuaga Ngwair walikuwa wanashangilia wasanii, mwanadada mwenye mvuto na jina
la hali ya juu, Wema Sepetu, muda mwingi alikuwa amejichimbia katikati ya
magari kwa ajili ya kukwepesha sura yake isionekane mbele ya mashabiki hao.
Ingawa ilishindikana, lakini ilisaidia kwa kiasi Fulani,
maana ni mara nyingi wasanii wanapoonekana au kupita karibu na mashabiki wao,
husababisha vurugu na mkanyagano wa aina yake.
Awali, msanii Kitale alipita pembeni kabisa ya jukwaa, hali
iliyozua balaa kubwa, hadi askari walipomkimbilia kwa ajili ya kuokoa jahazi
asizidi kuzongwa na mashabiki hao.
Kwa hakika watu walikuwa wengi, hivyo ilishindikana wote
kufanikiwa kumuaga marehemu Ngwair, hivyo safari yaa kuelekea makaburi ya
Kihonda Kanisani kuanza.
Kando ya barabara zote ambapo mwili huo ulipita, kulikuwa
kumezagaa watu waliokuwa na lengo la kuona msafara wa Ngwair. Morogoro
ilizizima kwa kiasi kikubwa mno.
Kule makaburini, ilikuwa inahitaji nguvu na ujasili wa aina
yake kuweza kuingiza mguu, hasa kwa wale waliokuwa wanahitaji kupiga picha kwa
wanahabari.
Ni kwa bahati mbaya tu, eneo alilozikwa Ngwair hakuna miti
mingi, vinginevyo tungeshuhudia namna gani watu ni wajuzi wa kupanda miti
wakitaka kuangalia hatua kwa hatua juu ya tukio zima la kumzika msanii Ngwair.
Majonzi makubwa yalitawala kwa kila mmoja wake, hasa kwa
ndugu wa marehemu na wasanii waliofanya kazi kwa karibu na marehemu, akiwapo M
to the P ambaye alikuja msibani hapo.
M to the P alilia sana, kila mmoja alimuonea huruma, hivyo
kuonyesha kuwa aliguswa na kuumizwa mno na msiba huo. Pamoja na changamoto zote
zilizojitokeza, ikiwamo jeshi la polisi kupwaya katika kuwapanga watu katika
shughuli za kuaga na hata kuzika, lakini mambo yalikwenda vizuri, yakiratibiwa
vyema na Kamati ya Mazishi.
Kamati hiyo ilifanya kazi zake kwa karibu zaidi na
Shirikisho la Muziki Tanzania, chini ya Rais wake, Addo Novemba.
0712 053949, 0753 806087
No comments:
Post a Comment