Pages

Pages

Saturday, June 08, 2013

Makala kubwa kabisa ya jinsi Albert Mangweha alivyozikwa mkoani Morogoro na maelfu ya watu kukanyagana



Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Morogoro
SIKU ya Alhamisi ya Juni sita, mashabiki wa muziki Tanzania, ilikuwa chungu na yenye kumbukumbu mbaya kwao, hasa waliposhuhudia mwili wa mpendwa wao, Albert Mangweha (Ngwair), ukiingia katika nyumba yake ya milele.

Ngwair alizikwa katika makaburi ya Kihonda Kanisani na kuhudhuriwa na watu wengi, mkoa mzima ukitetemeka kutokana na umati wa watu waliokwenda kuhudhuria mazishi yake.


Ni tofauti na matarajio ya wengi, maana baadhi yao hawakutarajia mwingiliano wa watu wengi wenye mapenzi mema na soko la muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva.


 
 Waombolezaji wakitafakari jambo.


Albert Mangweha 'Ngwair', enzi za uhai wake.
Kila pande za mji wa Morogoro ulikuwa hautoshi. Kila shabiki alihitaji walau kushhiriki kwa karibu kwenye msiba huo. Marehemu Ngwair alifariki Jumanne iliyopita, nchini Afrika Kusini.

Msanii huyo alifia katika harakati zake za kimaisha, huku mwenzake Mgaza Pembe M t0 The P akirudi hoi baada ya kukaa hospitalini kwa siku kadhaa kutokana na matatizo yaliyowapata nchini humo.

Kabla ya kuelekea Morogoro, Ngwair aliagwa pia katika Viwanja vya Leaaders Club siku ya Jumatano na kushuhudia wapenzi wa muziki wakijitokeza kwa wingi kumuaga mpendwa wao.

Mwimbaji huyo wa Ghetto Langu, Mikasi na nyingine aliweza kutangaza uwezo wake kwa tasnia ya Hip Hop, huku akipendwa zaidi hata na wasanii wenzake kutokana na ushirikiano wake kwa vijana wenzake.

Mwili wa marehemu Ngwair ulifika Leaders Club saa mbili asubuhi ambapo baada ya kumalizika kwa taratibu mbalimbali, hatimae alianza kuagwa na wadau wake, wakiwamo wasanii.

Wa kwanza kuagwa walikuwa wasanii na kufuatiwa na viongozi, ndugu na Watanzania wote waliokwenda viwanjanai hapo kupata fursa ya kumuaga msanii huyo wa Hip Hop.

Mara baada ya kumalizika shughuli za kumuaga, mwili wake ulipandishwa tena kwenye gari na kuanza safari ya mkoani Morogoro, ambapo kuna maeneo ambayo watu walijikusanya barabarani kwa ajili ya kupata fursa ya kuona msafara wa msiba huo.

Hata hivyo, baada ya kufika mkoani Morogoro, taratibu za kumuaga nyumbani kwa mama yake, ziliachwa, baada ya kushuhudia makundi kwa makundi yakikimbilia eneo la msiba, hivyo kuonyesha kuwa eneo hilo lisingeweza kuwa salama.

Kikao cha dakika kadhaa, kilikuja na majibu kuwa mwili huo uende kuagwa katika Uwanja wa Jamhuri, ambapo maelewano yao yalikuwa na tija, baada ya kukubaliana juu ya suala hilo.

Asubuhi ya siku ya mazishi yake, bado nyumbani kwa mama wa maarehemu, kulikuwa na watu wengi, hasa pale Mkuu wa Mkoa Morogoro, Joel Bendera alipokwenda kuwapa pole wafiwa.

“Poleni sana jamani kwa msiba huu, maana umetokea wakati bado tulikuwa tunahitaji muda wa kuendelea kukaa na ndugu yetu, Mangwair, mmoja wa vijana mahiri katika muziki wa Hip Hop.

“Sisi sote safari ni moja, hivyo tunachopaswa kufanya ni kumuombea dua njema msanii huyu aweze kupokelewa vyema baada ya kumaliza maisha yake ya duniani,” alisema Bendera, akiwafiriji ndugu wa marehemu na Watanzania kwa ujumla.

Mama wa marehemu, aliwashukuru Watanzania kwa kuonyesha upendo kwa mtoto wake, akiamini yote ni mipango ya Mungu, ukizingatia kuwa hakuna atakayeweza kubakia hapa chini ya jua.

Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, aliwataka wasanii kuendelea kushirikiana sambamba na kupigania vilivyo haki zao za msingi.

“Tusidanganyike na kuzikwa kwa mtindo huu wakati maisha yetu ni magumu licha ya kuwa na umaarufu wa aina yake, hivyo lazima tulipiganie suala hili kwa ajili ya maendeleo yetu.

“Wasanii wanakuwa na majina makubwa lakini hawana chochote mfukoni zaidi ya kusubiri kuzikwa kwa staili za kila aina, ikiwamo kukusanya Kamati za kuweka mambo sawa,” alisema Sugu.

Wakati mwili wa marehemu umefikishwa katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kwa ajili ya kuaga, uwanja huo ulikuwa na watu wengi mno, kila mmoja akiwa na hisia zake.

Hata hivyo, wapo wale waliokwenda kwa ajili ya kuangalia wasanii wanaoingia uwanjani hapo, jambo ambalo lilidhihirika pale waombolezaji hao, waliposhindwa kuvumilia na kujikuta wakipaza sauti zao juu na kuita majina ya wasanii wao.

Msanii kama vile Mr Blue, Afande Sele, Madee, Lady Jay Dee, Stamina, Chid Benz, TID na wengineo walionyesha kukubalika mno kiasi cha kushangiliwa kila wakati.

Hata hivyo, baada ya kugundua kuwa mashabiki hao waliokwenda kumuaga Ngwair walikuwa wanashangilia wasanii, mwanadada mwenye mvuto na jina la hali ya juu, Wema Sepetu, muda mwingi alikuwa amejichimbia katikati ya magari kwa ajili ya kukwepesha sura yake isionekane mbele ya mashabiki hao.

Ingawa ilishindikana, lakini ilisaidia kwa kiasi Fulani, maana ni mara nyingi wasanii wanapoonekana au kupita karibu na mashabiki wao, husababisha vurugu na mkanyagano wa aina yake.

Awali, msanii Kitale alipita pembeni kabisa ya jukwaa, hali iliyozua balaa kubwa, hadi askari walipomkimbilia kwa ajili ya kuokoa jahazi asizidi kuzongwa na mashabiki hao.

Kwa hakika watu walikuwa wengi, hivyo ilishindikana wote kufanikiwa kumuaga marehemu Ngwair, hivyo safari yaa kuelekea makaburi ya Kihonda Kanisani kuanza.

Kando ya barabara zote ambapo mwili huo ulipita, kulikuwa kumezagaa watu waliokuwa na lengo la kuona msafara wa Ngwair. Morogoro ilizizima kwa kiasi kikubwa mno.

Kule makaburini, ilikuwa inahitaji nguvu na ujasili wa aina yake kuweza kuingiza mguu, hasa kwa wale waliokuwa wanahitaji kupiga picha kwa wanahabari.

Ni kwa bahati mbaya tu, eneo alilozikwa Ngwair hakuna miti mingi, vinginevyo tungeshuhudia namna gani watu ni wajuzi wa kupanda miti wakitaka kuangalia hatua kwa hatua juu ya tukio zima la kumzika msanii Ngwair.

Majonzi makubwa yalitawala kwa kila mmoja wake, hasa kwa ndugu wa marehemu na wasanii waliofanya kazi kwa karibu na marehemu, akiwapo M to the P ambaye alikuja msibani hapo.

M to the P alilia sana, kila mmoja alimuonea huruma, hivyo kuonyesha kuwa aliguswa na kuumizwa mno na msiba huo. Pamoja na changamoto zote zilizojitokeza, ikiwamo jeshi la polisi kupwaya katika kuwapanga watu katika shughuli za kuaga na hata kuzika, lakini mambo yalikwenda vizuri, yakiratibiwa vyema na Kamati ya Mazishi.

Kamati hiyo ilifanya kazi zake kwa karibu zaidi na Shirikisho la Muziki Tanzania, chini ya Rais wake, Addo Novemba.
0712 053949, 0753 806087


No comments:

Post a Comment