Rais wa FM Academia, Nyosh el Sadaat
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
RAIS wa bendi ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa
Ngwasuma, Nyosh el Sadaat, amesema mwanamuziki ambaye hana nidhamu hawezi kuwa
na mafanikio katika maisha yake ya sanaa.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika onyesho lao la kila
Jumapili katika Ukumbi wa New Msasani Club, Nyosh alisema kwamba kwa sababu
hiyo, ipo haja ya wanamuziki kujifundisha nidhamu.
Alisema hata katika baadhi ya shoo, mwanamuziki mwenye
nidhamu anakuwa nyuma ya jukwaa na sio kuzurula ovyo ovyo kiasi cha kushindwa
kujipanga anapohitajika jukwaani.
“Jamani hatuwezi kufanikiwa katika maisha ya muziki kama
nidhamu zetu ni ndogo, hivyo naomba sisi ambaye tunaishi kwa kazi hii tujifunze
jambo hilo maana ni muhimu mno.
“Nasikitika kuona wanamuziki wangu, wakiwamo marepa
wanazagaa tu wakati wanastahili kutulia nyuma ya jukwaa kwa pamoja, maana hii
ni kazi na lazima tuiheshimu,” alisema Nyosh.
Maneno ya Nyosh yalitokana na kuwapandisha wanamuziki wake
mmoja baada ya mwingine kuonyesha uwezo wao, hasa kwa nafasi za marepa ambazo
kwa Wazee hao wa Ngwasuma, kumekuwa na ushindani wa aina yake na kuleta
burudani za aina yake.
No comments:
Post a Comment