Amezaliwa bila sehemu ya haja kubwa
Ahitaji msaada wa kwenda India
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
INAPOTOKEA ndugu au sehemu ya familia yako amezaliwa mtoto
akiwa mwenye afya njema, hakika hilo
ni jambo la kumshukuru Mungu. Katika hilo,
kila mmoja huzaliwa kwa kudra za Manani na kuishi kupo mikononi mwake.
Wengi huzaliwa na mateso ya aina yake. Wanazaliwa wakiwa na
matatizo makubwa, jambo linaloweza kukufanya ujiulize maswali mengi juu ya
matakwa ya Mungu kumuumba mtoto huyo na kuzaliwa katika hali hiyo.
Katika kuwaza huko, binadamu tunatakiwa tumshukuru yeye
aliyeweza kuimba Dunia na kuufanya watu wauone usiku na mchana.
Binadamu pia wanatakiwa wamshukurru yeye maana ndio kila
kitu katika Dunia, huku ule msemo usemao hujafa hujaumbika ukitimia, kama sio kwake leo basi kwangu kesho.
Nimelazimika kuanza hivi baada ya kuona mateso ya mtoto
Godfrey John, mwenye umri wa mwaka mmoja, aliyezaliwa katika Hospitali ya
Mwananyamala, mwaka jana, huku akiwa hana sehemu ya haja kubwa, hivyo
kulazimika kuishi kwa tabu.
Mama mzazi wa John, Veronica Lawrant, alizungumza na
HANDENI KWETU, juzi kuwa mtoto wake alizaliwa akiwa hana njia
hiyo huku madaktari wakishindwa kubaini hilo
mapema, hadi baada ya siku tatu, alipoanza kujaa mwili wake.
“Nilishangaa mwanangu anavimba mwili wake ikiwa ni siku
chache baada ya kumzaa katika hospitali ya Mwanyamala, nikiwa na matumaini
makubwa dhidi yake, nikimshukuru Mungu baada ya kujifungua kwa njia ya kawaida.
“Hali yake ilinishtua sana,
hivyo kuamua kwenda katika hospitali ya Mnazi Mmoja kupata matibabu ya mtoto
wangu mpendwa, hata hivyo madaktari nao hawajabaini lolote zaidi ya kunipa dawa
ambazo hazikuwa na msaada,” alisema Veronica, mkazi wa Bunju, jijini Dar es Salaam.
Anasema kwamba baada ya kurudi nyumbani, usiku wake mtoto
wake alianza kupata haja kubwa kwa njia yam domo, jambo ambalo lilizidi
kumuumiza kichwa na kuamua tena kwenda tena katika Hospitali ya Mwanyamala.
Alipofika, alipata bahati ya kupokelewa vyema, ingawa
hakukaa zaidi ya kutakiwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu
zaidi, ikiwa ni baada ya daktari aliyempokea, aliyemjua kwa jina la Dk Isayo,
ingawa hakuwa wa watoto, lakini alijua tatizo kwa kumuangalia tu na kumtaka
apelekwe usiku huo.
Huku akiwa na masikitiko makubwa, mama huyo anasema alifika
Muhimbili saa saba za usiku na kupokelewa vizuri tayari kwa mtoto wake kuanza
kuchunguzwa juu ya afya yake, maana mwili wake ulianza kubadilika sambamba na
kujisaidia mara kwa mara kwa njia ya mdomoni, hivyo kuibua wasi wasi mkubwa
katika maisha yake.
“Dakika chache baada ya kufika, nilifuatwa na daktari
akasema kama nipo tayari nitie sahihi kwa
ajili ya mtoto wangu kufanyiwa upasuaji wa tumbo, maana waligundua kuwa hana
njia ya haja kubwa, jambo linalomfanya ajisaidie kwa mdomoni.
“Sikuwa na la kusema zaidi ya kukubaliana na uamuzi huo,
maana nilijua mwanangu atapata ahueni kama sio
kupona kabisa, jambo ambalo naweza kusema namshukuru Mungu kwakuwa yeye ndio
muweza wa yote,” alisema.
Kwa mujibu wa Veronica, mtoto wake anaweza kupona kabisa
kama atapata upasuaji katika hospitali za Nchini India, ukizingatia kuwa madaktari
wamemshauri hivyo ili kurudisha hali ya kawaida ya binadamu, juu ya upasuaji wa
Jonh.
Anasema huku akijua hata kula yake ni tabu, anajiuliza wapi
kwa kupata kiasi cha fedha cha kumpeleka mtoto wake India kwa matibabu zaidi, maana
maisha yake kwa sasa yamekuwa magumu kupita kiasi.
Mama huyo mzaliwa wa Kitiongoji cha Buru,
Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, anasema kwamba mtoto huyo analea peke
yake kwa kusaidiwa na baadhi ya Watanzania wanaojitolea walichokuwa nacho.
Baba yake Godfrey (John) alimkataa mtoto huyo siku chache
baada ya ujauzito huo na hata alipozaliwa, hasa alipogundua kuwa mtoto wao
amezaliwa na matatizo ya kukosa njia ya haja kubwa, hivyo kuishi kwa mashaka
makubwa.
“Sikujali tangu zamani juu ya kutekelezwa na baba watoto
wangu, ila naumia kwa kukosa kazi ya kuniingizia kipato hata ya kumudu dawa ya
kumsafishia mwanangu anapomaliza kujisaidia au mifuko ya kumvalisha, maana kwa
sasa kukosa maradhi ni kudra zake Manani peke yake, ukizingatia kwamba namfunga
kitambaa tumbo mwake.
“Wapo wadudu wakali wa bacteria wanaweza kuingia na
kumshambulia mwanangu, lakini nabaki sina la kufanya, maana hata ndugu zangu
nao hawana cha kunisaidia zaidi ya kuniacha kama
nilivyo na kuhangaika na mtoto wangu John,” alisema Veronica.
Veronica anasema kabla ya kupata ujauzito huo, alikuwa
akifanya kazi kwa Muhindi mmoja, anayejulikana kwa jina la Ghafur, maeneo ya
Kisutu, jijini Dar es Salaam,
alipofanya kazi kwa miaka mitatu, huku akilipwa Sh elfu 60,000 kwa mwezi.
Baada ya kujifungua mtoto huyo na kuwa kwenye tatizo hilo, bosi wake alimwambia
apumzike ahangaikie afya yake, jambo ambalo lilizidi kumchanganya, ukizingatia
kwamba maradhi ya mtoto wake yanahitaji fedha.
Mama huyo anasema anaomba msaada kutoka kwa Watanzania wote
wenye moyo wa huruma juu ya kumsaidia mtoto wake ili apate mwarobaini wa tatizo
lake, ukizingatia kwamba wataalamu wa afya
wamesema uwezekano huo upo akifika India.
“Wamesema utaalamu huu upo India
hivyo kunitaka niende kama uwezo ninao, lakini mimi maisha yangu ni magumu na
wakati mwingine nabangaiza hata kula yangu, sasa hiyo hela ya kunifikisha huko India
nitapata wapi?
“Naomba waandishi mfikishe maombi yangu, maana mwanangu anateseka na inapofikia wakati wa
mawingu mazito analia na kuumia sana
au pale anapotaka kupata haja kubwa,” alisema.
Veronica anasema kwamba anaowaomba watu wote wajitolee
chochote walichokuwa nacho, au afikishwe India
na kugharamiwa mahitaji yote, ili afya ya mtoto wake iwe kama ya watoto wengine
wenye amani katika maisha yao.
Veronica amemzaa mtoto wake huyo Oktoba 23 mwaka 2011 katika
Hospitali ya Mwanyamala, jijini Dar es Salaam, alipomzaa kwa njia ya kawaida.
Anachokumbuka, ni kwamba ujauzito wa mtoto wake ulimpa tabu,
ikiwamo kutokwa na damu puani pamoja na kugundulika kuwa ana ugonjwa wa
malaria, ambapo baadaye damu zilikata.
Mama huyo mwenye miaka 29, licha ya kukosa uwezo wa
kumsaidia mtoto wake, pia maisha yake ni magumu, ingawa mwenyewe hayo ameyaweka
pembeni zaidi ya kuangalia kwanza afya ya mtoto wake na awe kwenye afya njema.
“Najua kwa sasa sina kazi wala biashara yoyote, ila haya
yatakwisha kama nitaingia kwenye shughuli zangu, ukizingatia niliachishwa kazi
kwa Muhindi, akiwa na nia njema tu ya kunipa nafasi ya kuhangaikia afya ya
mwanangu, lakini hakujua kama uamuzi ule ni
mchungu mno, ukizingatia kwamba hata huo mshahara mdogo kutoka kwake
niliukosa,” alisema Veronica.
Watanzania wenzangu, sambamba na Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto chini ya waziri wake, Sophia Simba, Wizara ya Afya na
kampuni mbalimbali nchini tuna kila sababu ya kumsaidia mtoto huyu ili aweze kupelekwa nchini India
kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.
Kama unahitaji kujua
chochote juu ya mtoto Godfrey John, wasiliana na mama yake kwa namba 0715
837700.
No comments:
Post a Comment