SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HUWEZI kumkataza mtu asitumie
nafasi yake kufanya kile anachokipenda katika tasnia ya michezo, ukiwamo mpira
wa miguu. Kila mtu anafanya kile anachokiona kwa manufaa yake na marafiki zake
anaokula nao.
Katika hilo,
hata kama watu wawe wakali vipi, lakini
itatungwa sababu, uongo wa kila aina kusafisha au kusawazisha kinachopingwa na
wadau wao. Kwangu mimi nasema, bebaneni mkikochoka mtaacha na kuendelea na
maisha mengine.
Nayasema haya kwa uchungu mkubwa
baada ya watu kulazimisha maji yapande mlima. Rais wa Shirikisho la Soka nchini
(TFF), Leodgar Tenga, juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa elimu kwwenye
kuongoza soka sio lazima.
Tenga anayasema haya huku akijua
wanachama wao wengi, wamelazimika kusimamisha chaguzi zao, au kusogeza mbele
ili wabadilishe katiba zao kwa ajili ya kuingiza kipengele cha elimu ya kidato
cha nne kuingizwa.
Wengi wamekutana na kadhia hii.
Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, amekumbana nayo na kuachia nafasi
yake ya uongozi wa Simba. Lakini leo hii kwakuwa kuna mtu anahitajiwa, ulazima
huo unafutwa.
Tenga amelazimika kusema haya
maana TFF inamuhitaji mgombea wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Amini Bakheresa.
Bakheresa amekuwa akiwekewa pingamizi na wadau mbalimbali wa michezo.
Hata hivyo, wanaomuwekea pingamizi
hushindwa baada ya watu wenye nafasi zao kuingilia kati kwa ajili ya kubebana.
Ndio maana nasema, kwangu mimi siumizwi na suala hilo la kuwasaidia marafiki zenu, ila sioni
haja ya kipengele cha elimu kuwa hoja.
Vinginevyo waheshimiwa
watajizalilisha tu. Tenga na jopo lake la TFF linajipaka kinyesi, maana
hawawezi kuwakataza wachache na kuwaruhusu wengine. Tangu mwanzo, sikuwahi
kukubali mabadiliko ya katiba ili kuingizwa kipengele cha elimu.
Nilifanya hivyo kwakujua uongozi
hausomewi kamwe. Uongozi ni kipaji na sio kila mtu anaweza kuwa viongozi.
Nilifanya hivyo kwakuangalia viongozi wengi mahiri katika Taifa hili ambao
hawak,uwa na elimu kubwa.
Hata kwenye soka, Dalali aliongoza
kwa mafanikio makubwa akiwa Simba.
Aliweza kuipa ubingwa timu yake bila kufungwa hata mechi moja. Lakini kipengele
cha elimu kikamuondoa, tena kwa kubarikiwa na TFF.
Leo hii vipi DRFA wembe huo
usitumike? Kuna nini hapo kwenye ofisi za TFF na DRFA? Aibu hii itakwisha lini?
Hakika siwezi kuvumilia. Aidha, iwekwe wazi kuanzia sasa kuwa yoyote anaweza
kuwa kiongozi hata kama akiwa hana elimu ya
kidato cha nne.
Kila mwenye uwezo huo wa kuongoza,
apewe nafasi na sio kwa watu wachache. Nalisema hili hadharani, maana kuna siku
kutatokea mkanganyiko wa kiuongozi na kuzua balaa. Hili linawekwa kwenye
kumbukumbu na vizazi vijavyo watalifanyia kazi.
Hakika siwezi kuvumilia na
nitaendelea kusubiri wenye mtazamo wao, harakati zao na wanaotaka kuweka
kumbukumbu sawa kuwa wakali zaidi katika hilo.
Kwakuwa mimi sina nia yoyote ya
kuwania nafasi hiyo kwa sasa, pia siwezi kulia wala kucheka ninapoona sheria
hazifuatwi, maana najua fika hata niseme vipi, wakubwa hao wakiamua lao hakuna
wa kuwazuia, ndio maana mbeleko yao
kwa maswahiba zao zipo pale pale.
Tena kwa dharau tele. Eti wanasema
kelele za chura hazimnyimi tembo kunywa maji na dua ya kuku haipati mwewe. Haya
bwana nyie endeleeni kubebana hadi mtakapochoka wenyewe na kuanza kufuata
sheria na taratibu mlizoweka wenyewe.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment